Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za TRA jijini Dar es Salaam kuhusu mamlaka hiyo kukusanya ushuru wa bidhaa Shilingi billioni 42.8 kwa mwezi machi 2019 ukilinganisha na shilingi bilioni 39.3 zilizokusanywa kipindi kama hicho mwaka 2018 ambapo ongezeko hilo limetokana na utekelezaji wa Mfumo wa Stempu za Kodi za Kielektroniki uliotozwa kwenye Sigara, Mvinyo, Pombe Kali, Bia na aina zote za vileo ambao ulianza rasmi tarehe 15 Januari, 2019. Wengine katika picha ni Bw. Abdul Mapembe Kamishna wa Kodi za Ndani (kushoto) na Bw. Richard Kayombo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi (kulia).

Na Veronica Kazimoto, Dar es Salaam.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya ushuru wa bidhaa shilingi bilioni 42.8 kwa mwezi Machi, 2019 ukilinganisha na shilingi bilioni 39.3 zilizokusanywa kipindi kama hicho mwaka 2018 ambacho ni sawa na ongezeko la shilingi bilioni 3.5 au ukuaji wa asilimia 9.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo Charles Kichere amesema kuwa, ongezeko hilo limetokana na utekelezaji wa Mfumo wa Stempu za Kodi za Kielektroniki uliotozwa kwenye Sigara, Mvinyo, Pombe Kali, Bia na aina zote za vileo ambao ulianza rasmi tarehe 15 Januari, 2019.

“Mfumo huu mpya wa stempu za kielektroniki umeonyesha mafanikio makubwa sana. Mwezi Machi mwaka huu tumekusanya ushuru wa bidhaa jumla ya shilingi bilioni 42.8 kutoka kwenye sigara, mvinyo, pombe kali, bia na aina zote za vileo wakati mwaka jana kipindi kama hicho tulikusanya shilingi bilioni 39.3. Kiwango hiki kinatarajiwa kuongezeka maradufu kwani idadi ya viwanda vinavyoendelea kufungiwa mfumo huu mpya vinazidi kuongezeka”, alisema Kichere.

Kichere ametolea mfano wa mzalishaji wa pombe kali aliyekuwa akilipa ushuru wa bidhaa kati ya shilingi milioni 140 hadi 160 kwa mwezi lakini baada ya kufunga mfumo wa stepu za kielektroniki amelipa shilingi milioni 274.

“Pia wapo waliokuwa wanalipa kati ya shilingi milioni 20 hadi 30 lakini kwa sasa wanalipa shilingi milioni 85 hadi 172 kwa mwezi,” aliongeza Kichere.

Alibainisha kuwa, mfumo wa stempu za kodi wa kiektroniki unatekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza inahusisha bidhaa za sigara, mvinyo, pombe kali, bia na aina zote za vileo wakati awamu ya pili ikihusisha bidhaa za vinywaji baridi, maji, juisi na CD/DVDs ambapo kwa sasa TRA inatekeleza awamu ya kwanza ambayo ilianza rasmi tarehe 15 Januari, 2019 na awamu ya pili itaanza rasmi tarehe 01 Mei, 2019.

“Kama nilivyotangulia kusema kuwa, sasa hivi tuko kwenye utekelezaji wa awamu ya kwanza, hivyo basi bidhaa zote za awamu hii ambazo ziko sokoni na zimebandikwa stempu za zamani na zile ambazo hazijabandikwa stempu za ushuru wa bidhaa kabla ya kuanza kwa mfumo huu wa stempu za kielektroniki, zinaruhusiwa kuendelea kuwepo sokoni hadi tarehe 30 Aprili, 2019, na baada ya hapo zitatakiwa kubandikwa stempu za kodi za kielektroniki kabla ya kuuzwa”, alisema Kichere.

Awali, Kamishna mkuu huyo alizitaja changamoto za stempu za kodi za karatasi zilizopelekea kuanzishwa kwa stempu za kodi za kielektroniki. Alisema changamototo hizo ni pamoja na upotevu wa mapato ya Serikali kutokana na udanganyifu katika taarifa za uzalishaji zinazotolewa na wazalishaji pamoja na kuibuka kwa wimbi la wadanganyifu waliotumia madhaifu ya mfumo wa stempu za karatasi na kuiibia Serikali kwa kutengeneza stempu za kughushi.

Changamoto nyingine ni uwezekano mdogo wa kutambua stempu za kughushi unaochangia uwepo wa bidhaa zisizokidhi viwango vya ubora na zinazoweza kuathiri afya za binadamu pamoja na kutokuwa rahisi kutambua uhalali wa bidhaa iliyoko sokoni kuwa imetengenezwa na mzalishaji halali wa bidhaa hiyo.

Kwa upande wa faida za mfumo wa stempu za kodi za kielektroniki, Kamishna Mkuu Kichere amesema kuwa ni pamoja na kuongeza mapato yanayotokana na ushuru wa bidhaa, kuondoa malalamiko ya kutokutendewa haki ya makadirio ya kodi zinazosimamiwa na TRA, kuwezesha ufuatiliaji wa bidhaa kutoka viwandani, mipakani, bohari zilizoruhusiwa, majengo ya kutunzia bidhaa, sokoni hadi kwa mlaji na kuiwezesha Serikali kutambua mapema kiasi cha ushuru wa bidhaa kitakacholipwa.

Faida nyingine ni kuziba mianya ya uingizaji bidhaa kiholela nchini ambazo hazijalipiwa ushuru stahiki, kuongeza uhiari wa ulipaji kodi kwa kutengeneza wigo sawa wa ushindani baina ya wazalishaji na waingizaji wa bidhaa hususan kwa zile zilizopo sokoni na zinazopaswa kubandikwa stempu za kodi za kielektroniki na kulinda afya ya mlaji kwa kumuwezesha mtumiaji au msambazaji kutambua bidhaa yenye stempu halali na isiyokuwa halali.

Ushuru wa bidhaa unatozwa kwa mujibu wa kifungu cha 124 cha Sheria ya Ushuru wa Bidhaa Sura ya 147 inayoainisha aina za bidhaa zinazotozwa ushuru huu kwa mujibu wa Jedwali la nne (4) la sheria hii sambamba na marekebisho yanayofanyika kupitia Sheria ya Fedha.

ufuatia sheria hiyo, Kanuni za Stempu za Kodi zilitungwa ili kuhakikisha kuwa, utaratibu wa kutambua kiwango cha uzalishaji na uingizaji wa bidhaa nchini unakuwa ni wa uwazi na unafuatwa kwa lengo la kutoza kodi stahiki.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: