Articles by "HABARI ZA BIASHARA"
Showing posts with label HABARI ZA BIASHARA. Show all posts

Na Mwandishi Wetu

DAR ES SALAAM: Wafanyakazi wa Puma Energy Tanzania wamekutana jijini Dar es Salaam kusherehekea hatua ya kampuni hiyo kufikisha vituo 100 vya mafuta na huduma za ziada nchini, huku wakitambua mchango wao katika mafanikio hayo.

Tukio hilo lililofanyika Septemba 19, 2026, liliwakutanisha wafanyakazi kutoka idara na maeneo mbalimbali ya kampuni, ambapo walipata fursa ya kuimarisha ushirikiano na mshikamano, pamoja na kujadili mwelekeo wa kampuni na mipango ya ukuaji wa biashara.

Hatua ya kufikisha vituo 100 imekuja wakati Puma Energy Tanzania ikiendelea kutambuliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kwa nafasi yake katika soko la mafuta nchini kwa miaka minne mfululizo.
Akizungumza katika tukio hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatma M. Abdallah, alisema mafanikio hayo ni matokeo ya juhudi na ushirikiano wa wafanyakazi katika maeneo mbalimbali ya kampuni.

“Kufikisha vituo 100 vya mafuta na huduma za ziada ni hatua muhimu katika ukuaji wa biashara yetu, lakini pia ni matokeo ya kazi ya watu walio nyuma ya mafanikio haya. Tumefikia hapa kutokana na kujituma na ushirikiano wa wafanyakazi katika maeneo mbalimbali ya kampuni,” alisema.

Alisema tukio hilo ni fursa ya kutambua mchango wa wafanyakazi, kuimarisha mahusiano ya kikazi na kuangalia kwa pamoja hatua inayofuata katika ukuaji wa kampuni.
 
“Tunapoadhimisha kufikisha vituo 100, tunatambua pia kuwa kila hatua ya mafanikio huleta majukumu mapya. Sasa tunalenga kujenga zaidi juu ya tulichokifikia, kuimarisha ushirikiano wetu na kuendelea kuwahudumia wateja kwa ufanisi. Wafanyakazi wetu wataendelea kuwa sehemu muhimu ya safari hii,” alisema.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kufikisha vituo 100 si tu ishara ya kupanuka kwa mtandao wa huduma za Puma Energy Tanzania, bali pia ni matokeo ya mchango wa wafanyakazi katika kuhakikisha shughuli za kampuni zinaendeshwa kwa ufanisi na huduma zinawafikia wateja katika maeneo mbalimbali nchini.

Katika tukio hilo, uongozi pia uliwashirikisha wafanyakazi kuhusu vipaumbele vya kampuni katika kipindi kijacho, hatua iliyowapa nafasi ya kuelewa mwelekeo wa biashara na nafasi yao katika kutekeleza mipango hiyo.
Puma Energy Tanzania inaendesha shughuli mbalimbali katika sekta ya nishati, ikiwemo uendeshaji wa vituo vya mafuta, usambazaji wa mafuta, huduma za mafuta ya ndege, vilainishi, LPG na lami, pamoja na nishati safi na suluhisho zinazolenga kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.

Puma Energy ni kampuni ya kimataifa inayojihusisha na huduma za nishati katika zaidi ya nchi 35, hasa Amerika ya Kati na Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Na Mwandishi Wetu.

Dar es Salaam-Tanzania, 17 Septemba 2026: Je, umekwama katika ufanyaji wa kazi ambayo unajua kabisa hiyo siyo kwa ajili yako, na umewahi kujiuliza kama kitu ambacho una uwezo nacho ni kile ambacho unakifanya kila siku ukiwa nyumbani, njiani au kwa ajili ya kujifurahisha tu, kinaweza kuwa zaidi ya burudani?

Serengeti Lite, kinywaji pendwa cha Kampuni ya vinywaji ya Serengeti, kwa kushirikiana na KUNTA Africa, wanataka kupata jibu la swali hilo, kwa kutangaza rasmi ujio wa awamu nyingine ya Nyota Bigi msimu wa pili, ambayo inalenga kusaka nyota mkubwa ajaye wa Tanzania, katika mikoa ya Dar es salaam, Mwanza, Arusha na Dodoma. Usaili utaanza jijini Dar es salaam kuanzia tarehe 3 Oktoba, tarehe 10 safari itaendelea katika mkoa wa Mwanza, Arusha tarehe 17, na Oktoba 24 itakuwa jijini Dodoma.

Msimu wa pili wa Nyota Bigi unatafuta waimbaji, wacheza mziki, waigizaji, wachekeshaji, wabunifu, wana mitindo, na vipaji vingine vya ubunifu ambavyo Tanzania bado haijavivumbua. Mpango huu ni sehemu ya Kampeni ya Serengeti Lite ya “Lite your Imagination” inayolenga kuwahamasisha vijana kuchukulia ubunifu wao kwa uzito, kujieleza na kuona kipaji chao kinaweza kuwafikisha wapi.

Akizungumza katika uzinduzi wa msimu wa pili wa Nyota Bigi jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Masoko na Ubunifu wa Kampuni ya vinywaji ya Serengeti, Henry Esiaba, alisema jukwaa hili lipo kwa ajili ya kuthibitisha kwamba vipaji viko kila mahali na Nyota Bigi ipo wa ajili ya vipaji hivyo. 

“Tuna vipaji vingi katika kila kona ya nchi hii. Ila kinachokosekana wakati mwingine ni nafasi ya kuonekana. Nyota Bigi ipo kwa ajili ya kuwapa vijana wa Tanzania jukwaa hilo. Tumerudi kwa msimu wa pili, pamoja na washirika wetu KUNTA Africa, kwa sababu tunataka kugundua vipaji zaidi, kuviweka mbele ya hadhira kubwa na kuvipa msukumo unaostahili, popote vilipo,.” Alisema Esiaba.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Bia wa Kampuni ya vinywaji ya Serengeti, Rhona Namanya, amesema kuwa msimu huu wa pili ni mkubwa zaidi na kuwa wamejikita katika kutafuta vipaji mbalimbali katika miji zaidi Tanzania kulinganisha na msimu wa kwanza mwaka jana. 
“Mwaka huu tunafurahi kuwajulisha Watanzania kuwa msimu wa pili utakwenda katika miji mbalimbali Tanzania ukilinganisha na mwaka jana ambapo tulitafuta vipaji hapa Dar es Salaam tu.  Msimu huu wa pili tutakwenda kwenye miji mingine ikiwepo Arusha, Mwanza na Dodoma. Hii inaonyesha dhamira yetu ya kukuza vipaji zaidi hapa Tanzania.” Alisema Rhona.

Usajili tayari umefunguliwa kupitia msimbo wa QR wa Nyota Bigi, tovuti ya Nyota Bigi, WhatsApp au simu. Waombaji wanapaswa kuwa na umri wa miaka 18 hadi 35, kuwa na kitambulisho halali na kuwasilisha video fupi inayoonyesha kipaji chao. Usaili utafanyika ana kwa ana na mtandaoni, hivyo kutoa njia mbalimbali kwa wenye vipaji kujitokeza.

Kwa watakaofanikiwa kuvuka hatua hiyo, Nyota Bigi inatoa fursa ya kuingia katika tasnia pana ya ubunifu, huku nafasi zikiongezeka zaidi ya mashindano yenyewe. Washiriki wanaweza kupata fursa za kuunganishwa na maeneo mbalimbali ya masoko kupitia mitandao ya kijamii, uanamitindo, burudani, usimamizi wa vipaji na studio za kurekodi, na hivyo kupata nafasi yakufanikiwa zaidi.

Kwa Serengeti Lite, Nyota Bigi inaweka “Lite Your Imagination” katika vitendo kwa kuwapa vijana nafasi ya kutoka kwenye kufikiria tu kile wanachoweza kufanya na kuanza kukiweka wazi kupitia vipaji vyao. Jukwaa hili ni sehemu ya mwendelezo wa Serengeti Lite katika kukuza ubunifu wa vijana nchini Tanzania.

Mkuu wa Idara ya Masoko na Uwezeshaji, Vodacom Business, Joseph Sayi, akizungumza na wafanyabiashara wa rejareja wa bidhaa za Tanzania Breweries PLC (TBL) wakati wa semina ya kuwajengea uwezo kupitia Mpango wa Maendeleo ya Wafanyabiashara wa Rejareja (GRIT), iliyofanyika jijini Mwanza jana. Mafunzo hayo yaliyowashirikisha wafanyabiashara 150 yalilenga kuwaongezea ujuzi katika usimamizi wa biashara, fedha na matumizi ya suluhisho za kidijitali. Semina hiyo ni sehemu ya ushirikiano wa miaka miwili kati ya TBL na Vodacom Tanzania unaolenga kuwafikia zaidi ya wafanyabiashara 24,000  nchini.
Zaidi ya wafanyabiashara 150 jijini Mwanza leo wamefanya mafunzo yanayolenga kuwajengea uwezo ili kuwasaidia kuendesha biashara zao kwa ufanisi zaidi, kusimamia fedha na kuongeza faida, kupitia Mpango wa Maendeleo ya Wafanyabiashara wa Rejareja (GRIT) unaotekelezwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa ushirikiano na Vodacom Tanzania Plc yamewaleta pamoja wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali ya jiji la Mwanza kwa ajili ya kujifunza namna ya kuboresha usimamizi wa biashara, ikiwemo kupanga matumizi ya fedha, kudhibiti bidhaa na kufanya maamuzi yanayoweza kusaidia biashara zao kukua.

Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Michelle Kilpin, alisema kuwa GRIT ni sehemu ya juhudi za kampuni hizo ili kuwawezesha wafanyabiashara wanaofanya kazi nazo kwa kuwapatia maarifa na ujuzi unaoweza kuwasaidia kusimamia biashara zao kwa ufanisi zaidi. Alisema uwezo wa kusimamia fedha, bidhaa na shughuli za kila siku ni muhimu katika kuweka biashara katika nafasi nzuri ya kukua na kuchangia maendeleo ya jamii.

Miongoni mwa wakufunzi katika mafunzo hayo ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Dkt. Patrokil Kanje, aliyewafundisha washiriki namna ya kuendesha biashara kwa ufanisi, kusimamia gharama na kutambua maeneo yanayoweza kusaidia kuongeza faida.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Dkt. Kanje aliwasisitiza wafanyabiashara kuwa na uelewa wa kina kuhusu biashara zao, hasa katika kufuatilia mauzo, gharama na faida. 
Alieleza kuwa mfanyabiashara anapaswa kufahamu si tu kiasi anachouza, bali pia gharama anazotumia na faida anayobaki nayo, kwa kuwa taarifa hizo ni muhimu katika kufanya maamuzi sahihi, kudhibiti matumizi na kupanga ukuaji wa biashara.

Kwa mfanyabiashara, changamoto ya kila siku si kuuza bidhaa pekee. Ni kuhakikisha fedha zinazopatikana zinatumika kwa uangalifu, bidhaa zinaendelea kuwepo, gharama zinasimamiwa na biashara inabaki na faida. 

Hivyo, mafunzo hayo yanaweka mkazo kwenye maarifa ambayo mfanyabiashara anaweza kuyatumia moja kwa moja katika biashara yake.Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Masoko na Uwezeshaji wa Vodacom Tanzania Plc Joseph Sayi, amewahimiza wafanyabiashara kutumia suluhisho za kidijitali katika shughuli zao za kila siku, akieleza kuwa teknolojia inaweza kurahisisha miamala, kusaidia usimamizi wa fedha na kuimarisha mawasiliano na wateja.

Sayi alisema matumizi sahihi ya suluhisho za kidijitali yanaweza kuwasaidia wafanyabiashara kurahisisha baadhi ya shughuli za biashara, kupata huduma kwa urahisi na kutumia taarifa katika kufanya maamuzi yanayolenga kuimarisha biashara zao.
Mafunzo haya ni sehemu ya mpango wa miaka miwili kati ya TBL na Vodacom Tanzania unaolenga kuwafikia zaidi ya wafanyabiashara 24,000 wa TBL nchini.

Kupitia GRIT, wafanyabiashara wanatarajiwa kupata ujuzi katika maeneo mbalimbali muhimu kwa uendeshaji wa biashara, ikiwemo usimamizi wa mtaji na mtiririko wa fedha, udhibiti wa bidhaa, huduma kwa wateja, ukuaji wa biashara pamoja na matumizi ya teknolojia na suluhisho za kidijitali.

Kwa wafanyabiashara walioshiriki jijini Mwanza, mafunzo hayo yanatoa fursa ya kuangalia biashara zao kwa mtazamo mpana zaidi, si kwa kuzingatia mauzo ya siku hiyo pekee, bali namna ya kujenga biashara inayoweza kusimamiwa vizuri, kukabiliana na changamoto na kukua kwa muda mrefu.

Mpango huo unatarajiwa kuendelea kuwafikia wafanyabiashara katika maeneo mbalimbali nchini, ukiweka mkazo katika kuwapa maarifa na zana zinazoweza kuwasaidia kufanya biashara kwa ufanisi zaidi katika mazingira yanayozidi kubadilika.

Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando (kushoto) akimkabidhi zawadi ya ukumbusho Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Breweries Limited (TBL) Bi. Michelle Kilpin (kulia) mara baada ya hafla ya kusainiwa kwa Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) kati ya kampuni hizo mbili, iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Septemba 11, 2026. Kupitia ushirikiano huo, zaidi ya wafanyabiashara 26,000 wa TBL nchini watanufaika na mafunzo ya biashara pamoja na suluhisho za kidijitali za Vodacom kupitia Mpango wa Maendeleo ya Wafanyabiashara wa Rejareja (Retailer Development Programme).

●Ushirikiano huu wa kimkakati utawawezesha wafanyabiashara wa TBL kupata suluhisho za kidijitali za Vodacom unatarajiwa kuzinduliwa rasmi jijini Mwanza Septemba 16.

Dar es Salaam, Septemba 11, 2026: Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na Vodacom Tanzania PLC leo zimeingia makubaliano ya ushirikiano (MoU) ya muda wa miaka miwili, yenye lengo la kuimarisha uwezo wa wafanyabiashara nchini kupitia Mpango wa Maendeleo ya Wafanyabiashara wa Rejareja (Retailer Development Programme), uliobuniwa mahususi ili kuwapatia ujuzi wa vitendo katika usimamizi wa biashara, fedha na matumizi ya teknolojia vitakavyopelekea kukuza biashara zao.

Ukiendeshwa chini ya kaulimbiu ya ‘Growing Innovatively Together’ (GRIT), mpango huu unadhihirisha azma ya pamoja ya taasisi zote mbili za kuwasaidia wafanyabiashara wanaoshiriki kwa kiwango kikubwa katika mnyororo wa thamani wa TBL pamoja na mchango wao katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi wa Masuala ya Kisheria na Uhusiano wa Kampuni wa TBL Neema Temba, alisema ushirikiano huu unaonesha umuhimu wa kushirikiana katika kuimarisha uwezo wa wafanyabiashara na kuwawezesha kukua kwa muda mrefu.

"Kwa TBL, wafanyabiashara ni nguzo muhimu ya biashara na ukuaji wa uchumi. Kupitia ushirikiano na Vodacom Tanzania, tunawekeza katika ujuzi, teknolojia na uendelevu wa biashara ili kuwawezesha kukuza shughuli zao na kunufaika na fursa mpya. Hivyo tunajenga thamani inayonufaisha biashara, familia na jamii kote nchini,” alisema Bi Temba.


Ushirikiano huu utaunganisha mtandao mkubwa wa TBL wa zaidi ya wafanyabiashara 26,000 na uzoefu wa Vodacom katika mawasiliano, ubunifu wa kidijitali na huduma za kifedha kimtandao, kwa lengo la kuwasaidia wafanyabiashara kuboresha ufanisi, uimara na uendelevu wa biashara zao.

Kupitia mpango huo, wafanyabiashara watapatiwa mafunzo katika maeneo mbalimbali muhimu ya uendeshaji wa biashara, ikiwemo usimamizi wa biashara na fedha, mtiririko wa fedha, usimamizi wa bidhaa, mauzo na masoko, huduma kwa wateja, ujasiriamali, biashara inayozingatia uwajibikaji pamoja na matumizi ya teknolojia za kidijitali.

Mbali na mafunzo, washiriki watawezeshwa kupata uelewa na matumizi ya suluhisho za kidijitali na kifedha zinazoweza kuwasaidia kuongeza ufanisi wa biashara, kuboresha faida na kuimarisha mahusiano na wateja.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando, alisema ushirikiano huo ni sehemu ya dhamira ya Vodacom ya kutumia teknolojia na ubunifu kusaidia wafanyabiashara na kuchochea ukuaji wa biashara nchini.

"Biashara ndogo ni muhimili wa uchumi wa Tanzania. Kupitia ushirikiano wa TBL na Vodacom Tanzania, wafanyabiashara wanapatiwa zana, maarifa na teknolojia za kuboresha biashara, kuongeza tija na kufungua fursa za ukuaji endelevu. Kwa pamoja, tunachochea ujumuishaji wa kidijitali na kifedha, na kuwawezesha kustawi katika uchumi unaoongozwa na teknolojia,” alisema Bw Nguvu.

Katika utekelezaji wa mpango huo, Vodacom itawapatia wafanyabiashara fursa ya kufahamu na kutumia suluhisho mbalimbali za biashara na huduma za kidijitali, ikiwemo SME Bomba, M-Wekeza, Lipa kwa M-Pesa na M-Koba, zinazolenga kusaidia ujumuishaji wa huduma za kifedha, ufanisi wa biashara na matumizi ya teknolojia katika shughuli za kila siku.

Kadhalika, ushirikiano huu utakuza ubunifu, ujasiriamali na uwajibikaji katika biashara kupitia mafunzo ya ana kwa ana na majukwaa ya kidijitali. TBL na Vodacom Tanzania pia zitashirikiana katika mawasiliano, ushirikishwaji wa wadau, ufuatiliaji na tathmini ili kuhakikisha matokeo yanayopimika na yenye manufaa ya muda mrefu. Mafunzo ya kwanza chini ya Mpango wa Maendeleo ya Wafanyabiashara wa Rejareja yatafanyika Mwanza Septemba 16, yakiwapa wafanyabiashara ujuzi wa usimamizi wa biashara, fedha na matumizi ya teknolojia kwa ajili ya kuboresha utendaji na ukuaji endelevu. 

Kupitia ushirikiano huu, TBL na Vodacom zinaendelea kuimarisha ujasiriamali, matumizi ya huduma za kidijitali na kuwawezesha wafanyabiashara kuchangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Washirika wa Nyerere Cycling Tour, wakiongozwa na Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania PLC, Zuweina Farah (wa nne kulia), ambaye aliwakilisha Vodacom Tanzania PLC kama mdhamini mkuu wa msafara huo, wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa mkutano na waandishi wa habari na wadau wa msafara huo uliolenga kutangaza rasmi washirika wa zamani na wapya wa msafara huo. Katika picha kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Afroil, Mohamed Al-Jabry(wa pili kushoto) Meneja wa Uendelevu wa Stanbic Bank Tanzania, Annette Nkini (wa tatu kushoto), Mkuu wa Masoko na Mauzo wa BYD, Samwel Msonsa (wanne kushoto), Mwanzilishi wa Nyerere Cycling Tour, Gabriel Landa, Meneja wa Akaunti wa Vodacom Huawei, Victor Wang, na Katibu Mtendaji wa Coca-Cola Tanzania, Yvette Gadi. Mkutano huo ulifanyika jijini Dar es Salaam, Septemba 11, 2026.
Baadhi ya washiriki wa msafara wa Nyerere cycling tour wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari na wadau wa msafara huo uliolenga kutangaza rasmi washirika wa zamani na wapya wa msafara huo.
Mwanzilishi wa Nyerere Cycling Tour Gabriel Landa (wa kwanza kulia) akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari na washirika wao. Majadiliano hayo yalihusu namna gani watajumuika katika msafara huo.
 Washirika, Washiriki na Wadau wa Nyerere Cycling Tour wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kuhitimisha mkutano wa waandishi wa habari uliopangwa kwa ajili ya kutangaza rasmi washirika wapya na wa zamani wa msafara huo.
Mwanzilishi wa Nyerere Cycling Tour Gabriel Landa akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari na wadau wa msafara. Mkutano huo ulilenga kutangaza rasmi washirika wa zamani na wapya wa msafara huo.

Na Mwandishi Wetu.

Nyerere Cycling Tour Watangaza Washirika wao wa mwaka 2026Nyerere Cycling Tour Imetangaza washirika wa safari ya mwaka huu itakayokuwa na umbali wa kilomita 1,500 hadi Butiama, huku Vodacom Tanzania ikiendelea kuwa mshirika mkuu wa msafara huo, ikishirikiana na Afro Oil, Stanbic Bank Tanzania, BYD, ABC Bicycle, Coca-Cola na Huawei.

Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Zuweina Farah, alisema Vodacom itaendelea kushirikiana na Nyerere Cycling Tour kama mshirika mkuu, akieleza kuwa ushirikiano huo unaonesha dhamira ya kampuni ya  kuendelea kuunga mkono mipango yenye kuleta matokeo chanya kwa jamii nchini. Alisema Vodacom pia inafurahia kuwapokea washirika wapya ambao ushiriki wao utaongeza thamani katika safari ya mwaka huu na kusaidia kupanua wigo na matokeo ya msafara huo.

Msafara huo utafanyika kuanzia tarehe 5 hadi 14 Oktoba 2026, ukiwa na mkazo katika elimu, afya na uhifadhi wa mazingira, sambamba na kuhamasisha wanafunzi, hususan wasichana, kushiriki katika michezo ya kuendesha baiskeli. Katika safari ya mwaka huu, Vodacom wanatarajia kutoa madawati 1,000 kwa shule 10, kukarabati madarasa 40 na kujenga madarasa mapya 10, huku shughuli hizo zikitarajiwa kuwafikia zaidi ya wanafunzi 25,000. Katika safari zilizopita, Nyerere Cycling Tour ilifikia  shule 107 na zaidi ya wanafunzi 75,000 walinufaika.

Akizungumzia ushirika wao, Meneja wa Uendelevu wa Stanbic Bank Tanzania, Annette Mkini, alisema benki hiyo itatumia msafara huo kuhamasisha elimu ya fedha kwa wanafunzi na vijana, ili kuwajengea uelewa itakayowasaidia kufanya maamuzi bora kuhusu matumizi na usimamizi wa fedha. Kwa upande wake, Afro Oil imesema ushiriki wake unatokana na dhamira ya kampuni ya kurudisha kwa jamii, huku Samwel Msonsa kutoka BYD alisema kampuni hiyo itashiriki katika uzalishaji na uhamasishaji wa msafara huo, pamoja na shughuli za uhifadhi wa mazingira ikiwemo upandaji miti.

Msafara huo hadi sasa umesajili waendesha baiskeli 213, huku wengine wakitarajiwa kujiunga njiani. Waendesha baiskeli kutoka nchi 12 wanatarajiwa kushiriki, zikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Malawi, Zambia, Afrika Kusini, Australia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Uholanzi. Aidha, wanawake 23 tayari wamesajiliwa kushiriki katika msafara huo.

Vodacom pia ilitoa taarifa kuhusu Vodacom Coastal Classic, ambayo hadi sasa imeandikisha washiriki 147. Na washindi wa nafasi ya kwanza kwa wanawake na wanaume watapata Sh milioni 10 kila mmoja, nafasi ya pili Sh milioni 7 na nafasi ya tatu Sh milioni 5. Waendesha baiskeli watakaomaliza nafasi ya nne hadi ya kumi watapata Sh milioni 1 kila mmoja.

Vodacom Tanzania imewekeza Sh milioni 160 katika Msafara wa Baiskeli wa Nyerere, huku Vodacom Foundation ikichangia zaidi ya Sh milioni 300 kwa shughuli za kijamii zitakazotekelezwa katika maeneo yatakayopitiwa na msafara huo, ikiwemo uboreshaji wa shule na utoaji wa madawati. Safari hiyo itahitimishwa Butiama, nyumbani kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania Stanley Kafu (wa pili kulia) wakipeana mikono na Diwani wa Kata ya Kawe Mheshimiwa Fabian Malima (katikati) baada ya kukabidhi vifaa vya kufanyia usafi wa jiji. Shughuli hiyo imefanyika kama kilele cha kusherehekea miaka 29 ya Benki ya Exim toka uanzishwaji wake nchini ambapo, walishiriki pia katika usafi wa fukwe za bahari katika maeneo ya Kawe. Tukio hilo limefanyika  tarehe 5 Septemba 2026, jijini Dar es salaam na kushuhudiwa na Meneja Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania, Kauthar D'souza (kulia), Mkuu wa Kituo cha Polisi Kawe ASP Ally Liviga (kushoto) na Afisa Usafishaji Manispaa ya Kinondoni Alban Mugyabuso wa pili Kulia.

Na Mwandishi Wetu.

Dar es Salaam-Tanzania, 22 Agosti 2026: Benki ya Exim Tanzania inaadhimisha miaka 29 tangu kuanzishwa kwake chini ya kaulimbiu "Miaka 29 ya Ubora kwa Vitendo," ikisherehekea karibu miongo mitatu ya ukuaji, uhusiano na wateja, ushirikiano na mchango kwa jamii inazozihudumia.

Mwaka 1997, Benki ya Exim Tanzania ilianza safari yake ikiwa na idadi ndogo ya wateja, na hatua kwa hatua ikajenga uwepo wake katika soko la Tanzania. Kwa kipindi cha miaka 29, Benki imekua na kuwa mojawapo ya taasisi za kifedha zinazoongoza nchini Tanzania, ikitambulika kwa ubunifu wake, suluhisho zinazomlenga mteja na mchango wake mkubwa katika ukuaji wa kiuchumi wa nchi, ikiwa na zaidi ya matawi 30 nchini kote na uwepo nje ya Tanzania katika masoko ya Comoro, Djibouti, Uganda na Ethiopia.

Kama sehemu ya safari hii, Benki ya Exim ilikuwa benki ya kwanza ya Tanzania kufungua matawi nje ya nchi, na kuifanya kuwa mojawapo ya benki chache za Tanzania zilizofanikiwa kupanua shughuli zake nje ya mipaka ya taifa hili. Kupitia mtandao wake mpana wa matawi na mifumo ya kisasa ya kibenki ya kidijitali, Benki inaendelea kuwawezesha watu binafsi na wafanyabiashara kwa suluhisho za kifedha zenye kutegemewa, nyumbufu na zinazolenga mustakabali, ikithibitisha dhamira yake ya kuchochea ukuaji endelevu na ustawi katika ukanda huu.

Safari ya Benki hii, hata hivyo, imekwenda mbali zaidi ya kutoa huduma za kifedha. Kwa miaka mingi, Benki ya Exim imewekeza katika mipango inayochangia ustawi na maendeleo ya jamii kupitia jukwaa lake la Exim Cares, likiwa na programu zinazogusa afya, elimu, ustawi wa vijana, uwezeshaji wa wanawake na uhifadhi wa mazingira. Mipango hii ni pamoja na msaada wa muda mrefu kwa kampeni za uchangiaji damu, ushirikiano na Young Scientists Tanzania (YST), Women Empowerment Program, pamoja na afua mbalimbali za kusaidia taasisi za afya na uhifadhi wa mazingira.
Mwaka huu, Benki inafanya maadhimisho yake kwa namna tofauti kwa kuupeleka mkondo huo moja kwa moja kwa jamii inazozihudumia. Kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 29, Benki ya Exim imekuwa ikifanya shughuli za usafi wa mazingira na kukabidhi vifaa vya usafi katika maeneo mbalimbali kupitia mtandao wake wa matawi, ikiwemo masoko, hospitali na shule katika mikoa mbalimbali, kwa lengo la kuhakikisha kunakuwa na mazingira safi, salama na yenye afya kwa jamii.

Jijini Dar es Salaam, shughuli hizo ni pamoja na ukabidhi wa vifaa vya usafi kwa Manispaa ya Kinondoni na zoezi la usafi wa jamii katika Fukwe ya Kawe, likikutanisha wafanyakazi wa Benki ya Exim, wadau na wanajamii katika kuchangia maeneo safi na yenye afya zaidi.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania, Bw. Stanley Kafu, alisema maadhimisho ya miaka 29 yanatoa fursa ya kuwathamini watu na jamii ambazo zimekuwa muhimu katika safari ya Benki, huku ikithibitisha dhamira yake ya kuendelea kuleta thamani zaidi siku zijazo.
"Safari yetu ya miaka 29 imejengwa pamoja na wateja wetu, wafanyakazi, washirika na jamii tunazozihudumia. Kila mteja aliyetuamini, kila biashara tuliyoisaidia na kila ushirikiano tulioujenga umechangia kuifanya Benki ya Exim kuwa taasisi iliyopo leo. Maadhimisho haya kwa hiyo si tu kuhusu kusherehekea Benki ya Exim; ni kuhusu kusherehekea kila mmoja aliyekuwa sehemu ya safari yetu," alisema Bw. Kafu.

Aliongeza kuwa uamuzi wa kuadhimisha maadhimisho hayo kupitia shughuli za kijamii unaakisi imani ya Benki kwamba dhamira yake inakwenda mbali zaidi ya huduma za kifedha.

"Tunafanya maadhimisho kwa namna tofauti mwaka huu kwa kuubadilisha mkondo huu kuwa kitu chenye maana kwa jamii zinazotuzunguka. Usafi wa mazingira ni jukumu la pamoja, na kupitia shughuli hizi na ukabidhi wa vifaa vya usafi, tunachangia kwa vitendo huku tukihamasisha watu wengi zaidi kumiliki maeneo tunayoyashiriki sote. Hii ndiyo maana halisi ya Ubora kwa Vitendo, kubadilisha dhamira kuwa hatua za vitendo zenye thamani kwa jamii zinazotuzunguka," alisema.
Akizungumza kwa niaba ya jamii, Diwani wa Kata ya Kawe, Bw. Benard Fabian Malima, alipongeza Benki ya Exim kwa kuchagua Kawe kama mojawapo ya maeneo ya shughuli zake za maadhimisho.

"Kwa niaba ya wakazi wa Kawe, napenda kuishukuru Benki ya Exim kwa mpango huu. Fukwe ya Kawe ni eneo linalotumiwa na watu wengi katika jamii hii kila siku, na kuliweka safi ni jambo linalonufaisha sote. Ukabidhi wa vifaa vya usafi kwa Halmashauri yetu utasaidia sana jitihada zetu za kuendelea kuweka mazingira safi, na tunatarajia taasisi nyingine zaidi zitafuata mfano huu," alisema Bw. Malima.

Shughuli hizo za kijamii zilifanyika katika maeneo mbalimbali kupitia mtandao wa Benki ya Exim, zikiwawezesha wafanyakazi na wadau katika jamii mbalimbali kushiriki katika mpango huu wa maadhimisho.

Aidha, Benki ya Exim inapoelekea mwaka wake wa 30, inaendelea kuwa na dhamira ya kujenga juu ya safari yake ya miaka 29 kwa kuendelea kubuni, kuboresha uzoefu wa wateja, kusaidia biashara na kuleta thamani zaidi kwa wateja wake, wadau na jamii.

Mkurugenzi wa Vodacom Business Nguvu Kamando (kushoto), akisalimiana na Mkurugenzi wa Programu za Afrika wa Bridge for Billions, Liliosa Mbirimi (kulia), muda mfupi baada ya kutangazwa kwa ushirikiano wa miaka mitatu kati ya Vodacom Digital Accelerator (VDA) na Bridge for Billions. Ushirikiano huo unalenga kuimarisha mfumo wa ujasiriamali nchini kwa kuwafikia zaidi ya wajasiriamali na wabunifu 1,000 na kusaidia zaidi ya biashara 40 kukua na kupanuka, ushirikiano huu ulitangazwa wakati wa Wiki ya Ubunifu Tanzania (IWTz) 2026, Septemba 3 jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Programu za Afrika wa Bridge for Billions, Liliosa Mbirimi (kulia), akizungumza wakati wa kutangazwa kwa ushirikiano wa miaka mitatu kati ya Vodacom Digital Accelerator (VDA) na kampuni hiyo unaolenga kuimarisha mfumo wa ujasiriamali nchini kwa kuwafikia zaidi ya wajasiriamali na wabunifu 1,000 na kusaidia zaidi ya biashara 40 kukua na kupanuka. Ushirikiano huo ulitangazwa wakati wa Wiki ya Ubunifu Tanzania (IWTz) 2026, Septemba 3 jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa Vodacom Business Nguvu Kamando.

Mkurugenzi wa Programu za Afrika wa Bridge for Billions, Liliosa Mbirimi (kulia) akifafanua kuhusu ushirikiano mpya wa miaka mitatu kati ya Vodacom Digital Accelerator (VDA) na kampuni hiyo unaolenga kuimarisha mfumo wa ujasiriamali nchini kwa kuwafikia zaidi ya wajasiriamali na wabunifu 1,000 na kusaidia zaidi ya biashara 40 kukua na kupanuka. Ushirikiano huo ulitangazwa wakati wa Wiki ya Ubunifu Tanzania (IWTz) 2026, Septemba 3 jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa Vodacom Business Nguvu Kamando.

Baadhi ya washiriki na wabunifu wakifuatilia uzinduzi wa ushirikiano wa miaka mitatu kati ya Vodacom Digital Accelerator (VDA) na Bridge for Billions unaolenga kuimarisha mfumo wa ujasiriamali nchini uliotangazwa wakati wa Wiki ya Ubunifu Tanzania (IWTz) 2026, Septemba 3 jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Vodacom Business Biashara Nguvu Kamando, akizungumza wakati wa kutangazwa kwa ushirikiano mpya wa miaka mitatu kati ya Vodacom Digital Accelerator (VDA) na Bridge for Billions, unaolenga kuimarisha mfumo wa ujasiriamali nchini na kuwawezesha wajasiriamali na wabunifu kukua. Ushirikiano huo ulitangazwa wakati wa Wiki ya Ubunifu Tanzania (IWTz) 2026, Septemba 3 jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa Programu za Afrika wa Bridge for Billions, Liliosa Mbirimi.

Na Mwandishi Wetu.

● Ushirikiano huu kupitia taasisi zinazosaidia wajasiriamali vyuoni unalenga kuwafikia zaidi ya wajasiriamali 1,000 na kusaidia biashara zaidi ya 40 kukua na kupanuka

Dar es Salaam, Septemba 4, 2026: Vodacom Tanzania Plc leo imetangaza kuingia katika ubia wa miaka mitatu na Bridge for Billions, mtandao wa kimataifa wa ujasiriamali, kwa lengo la kupanua wigo na kuongeza matokeo ya mpango wa Vodacom Digital Accelerator (VDA).

Katika kipindi cha miaka mitatu ya ubia huo, mashirika hayo mawili yatazijengea uwezo na kuziwezesha taasisi zinazosaidia wajasiriamali (ESOs) kote nchini Tanzania na hivyo kuwafikia zaidi ya wajasiriamali 1,000 na kusaidia biashara zaidi ya 40 kukua na kupanuka.

Ushirikiano huu unaashiria mabadiliko katika namna VDA inavyotekeleza na kuongeza matokeo yake. Pamoja na kuendelea na lengo la kusaidia biashara changa moja kwa moja, mpango huu sasa utawekeza pia katika vituo vya kulea na kukuza biashara, vituo vya ujasiriamali, vyuo vikuu na mashirika ya maendeleo ya biashara yanayowasaidia waanzilishi wa biashara kila siku. Hatua hii inalenga kuimarisha mifumo ambayo wajasiriamali nchini Tanzania wanaihitaji hata baada ya kumalizika kwa programu ya kundi fulani la washiriki.

Kupitia makubaliano hayo, Bridge for Billions italeta nchini utaalamu wake katika programu za kulea na kukuza biashara changa (incubation), teknolojia za kidijitali na uzoefu wa kujenga uwezo wa taasisi zinazosaidia wajasiriamali. Taasisi zitakazochaguliwa zitapatiwa mafunzo maalumu, zitawezeshwa kutumia zana na mifumo ya Bridge for Billions, pamoja na kupata msaada katika kubuni programu na kuziendesha.

Aidha, taasisi hizo zitaunganishwa na mtandao wa kimataifa wa washauri na taasisi zinazosaidia wajasiriamali, hivyo kuwawezesha kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujenga mahusiano na taasisi nyingine.

Wajasiriamali watakaopatikana kupitia taasisi hizo watapitia mchakato maalumu wa kulea na kukuza biashara zao, huku biashara zitakazoonesha uwezo mkubwa wa kukua zikiendelea kwenye hatua ya acceleration, ambapo zitapatiwa msaada wa kina zaidi katika kukuza biashara na kujiandaa kwa fursa za uwekezaji.

Tangu kuzinduliwa kwake mwaka 2019, Vodacom Digital Accelerator imekuwa ikiunga mkono biashara changa na zinazokua zinazotumia teknolojia kutengeneza bidhaa na huduma zenye uwezo wa kukua, katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, kilimo, elimu na huduma za kifedha.

Kupitia awamu mbalimbali, programu hiyo imewapatia wajasiriamali mafunzo, ushauri wa kitaalamu, teknolojia, fursa za kuunganishwa na wawekezaji, pamoja na fursa za kufikia mitandao na washirika wa Vodacom.Ubia huu wa miaka mitatu unaendeleza safari ya VDA kutoka kwenye programu zinazotekelezwa kwa awamu moja baada ya nyingine hadi kwenye uwekezaji wa muda mrefu katika kuimarisha mfumo wa ujasiriamali nchini.

Kundi la kwanza la taasisi zitakazoshiriki katika mpango huu linatarajiwa kutangazwa Oktoba 2026, huku maombi kwa wajasiriamali yakitarajiwa kufunguliwa mwishoni mwa Septemba 2026.
Benki ya Exim Tanzania imehitimisha mafunzo kwa wanawake wajasiriamali 50 waliofanikiwa kukamilisha programu ya wiki sita ya Women Empowerment Programme (WEP) 2026 jijini Dar es Salaam.

Utekelezaji wa programu hii kupitia mpango wao wa kurudisha kwa jamii wa Exim Cares unalenga kuwajengea wanawake wajasiriamali maarifa na ujuzi kwa vitendo na kuimarisha biashara zao, ikiwemo usimamizi wa fedha, uandaaji wa bajeti, kuwafahamu wateja wao, kutambua fursa za soko na kupanga mikakati ya ukuaji endelevu wa biashara.
Programu hii haiishii kwenye mafunzo pekee. Wahitimu wanaunganishwa na fursa, mitandao ya masoko pamoja na huduma za kifedha zinazoweza kuwasaidia kuchukua hatua inayofuata katika safari zao za biashara.

Wakati wakiwapongeza wanawake hao 50, Benki ya Exim inaendelea kutarajia kuona biashara zao zikikua, zikitoa fursa kwa wengine na kuleta matokeo chanya katika familia na jamii zinazowazunguka.

Wafanyakazi wa Puma Energy Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja huku wakipeperusha bendera, ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa ziara ya PumaGas katika mikoa mitano nchini. Ziara hiyo imezinduliwa katika kituo cha Puma kilichopo Bunju, Dar es Salaam, tarehe 3 Septemba 2026, na itaendelea kwa wiki nane ikianzia Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Dodoma, kabla ya kuhitimishwa rasmi jijini Mwanza.

Dar es Salaam, 3 Septemba 2026: Puma Energy Tanzania imeanza rasmi ziara ya PumaGas itakayopita katika mikoa mitano nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kampuni hiyo kusogeza huduma za gesi ya kupikia karibu na wananchi na wafanyabiashara.

Ziara hiyo imezinduliwa katika kituo kipya cha Puma Energy kilichopo Bunju, Dar es Salaam, na itaendelea kwa kipindi cha wiki nane katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma na kuhitimishwa rasmi jijini Mwanza.Kupitia ziara hiyo, Puma Energy inalenga kuwafikia watumiaji wa gesi ya kupikia katika maeneo mbalimbali, kuwapa nafasi ya kupata taarifa kuhusu matumizi ya gesi, kujifunza zaidi kuhusu bidhaa na huduma zinazopatikana, pamoja na kuwasiliana na mawakala wa PumaGas katika maeneo yao.

Ziara hiyo inabeba ujumbe wa kampeni yao ya “Hakuna Kuchochea, Tumerahisisha na PumaGas,” unaolenga kuzungumzia namna gesi ya kupikia inavyoweza kutumika katika shughuli za kila siku za kaya na biashara.
“Lengo letu si kuwaambia watu kuhusu gesi ya kupikia pekee, bali kuwapa nafasi ya kuifahamu, kuona namna inavyotumika na kupata taarifa wanazohitaji kabla ya kufanya uamuzi. Kwa kupeleka PumaGas moja kwa moja kwenye jamii, tunataka kuwa karibu zaidi na wateja wetu na kuelewa mahitaji yao katika maeneo mbalimbali,” alisema Bi. Lilian Kanora, Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Puma Energy Tanzania.

Katika maeneo yatakayofikiwa, timu za PumaGas zitakutana na kaya, wafanyabiashara wa chakula, migahawa, hoteli pamoja na mawakala wa gesi. Kutakuwa pia na maonesho ya matumizi ya gesi na fursa kwa wananchi kuuliza maswali kuhusu matumizi, upatikanaji na ujazaji wa gesi kwenye mitungi.

Kwa upande wa wafanyabiashara wanaotumia gesi katika shughuli zao za kila siku, ziara hiyo itatoa nafasi ya kujifunza zaidi kuhusu matumizi ya gesi katika biashara kama vile mama ntilie, watoa chipsi, migahawa na hoteli. Mawakala nao watashirikishwa katika kuimarisha upatikanaji wa bidhaa na huduma kwa wateja katika maeneo yao.

Safari hiyo itafikia kilele chake Mwanza, ambapo Puma Energy itaingia rasmi katika soko la Kanda ya Ziwa. Uzinduzi huo utahusisha hafla ya kutambulisha PumaGas katika soko hilo, kukabidhi mtungi kwa mteja wa kwanza na kumtambua wakala wa kwanza wa PumaGas katika eneo hilo, pamoja na kushirikisha wadau na vyombo vya habari.

Sehemu ya uzinduzi katika Mkoa wa Mwanza pia itahusisha maonesho ya matumizi ya gesi katika shughuli za kawaida za kila siku. Mama ntilie atapika chapati kwa kutumia mtungi wa PumaGas, huku wananchi wakipata nafasi ya kuona moja kwa moja kiasi cha chakula kinachoweza kuandaliwa kwa kutumia gesi hiyo.

Kwa Puma Energy, ziara hii ni sehemu ya mpango mpana wa kuongeza upatikanaji wa gesi ya kupikia na kuifikisha huduma hiyo kwa wananchi katika maeneo mengi zaidi nchini.

Kuanzia Dar es Salaam hadi Mwanza, ziara hiyo itachukua wiki nane kuzunguka jamii mbalimbali, kusikiliza mahitaji ya watumiaji na kuwasogezea huduma za PumaGas karibu zaidi na maeneo wanayoishi na kufanya biashara.PumaGas: Hakuna Kuchochea, Tumerahisisha.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Mtandao wa Vodacom Tanzania Plc Andrew Lupembe (kushoto) na Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa kampuni hiyo Zuweina Farah wakizungumza wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Mazingira, Jamii na Utawala (ESG) ya kampuni hiyo kwa mwaka wa fedha ulioishia Machi 2026, ambayo imeonesha kupungua kwa uzalishaji hewa chafu (carbon emissions) kwa asilimia 24 na uwekezaji mkubwa katika uboreshaji wa mtandao. Tukio hilo lilifanyika jijini Dar es Salaam tarehe 3 Septemba, 2026.

Mkurugenzi wa Miundombinu wa Vodacom Tanzania Plc Andrew Lupembe akizungumza na waandishi wa Habari wakati wa uzinduzi wa ripoti  ya ESG ya mwaka 2026.

Mmoja wa wasikilizaji wakati wa uzinduzi wa ripoti ya ESG akiuliza swali ili apate ufafanuzi zaidi ya namna gani matokeo ya ripoti hiyo yatakavyozidi kuwanufaisha wananchi wa Kawaida.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria uzinduzi wa ripoti hiyo wakisikiliza ufafanuzi wa namna kampuni hiyo inavyochukulia  ESG kwa uzito unaotakiwa, wakati Vodacom ilipozindua ripoti ya ESG ya mwaka ulioishia Machi 31, 2026

Na Mwandishi Wetu.

Dar es Salaam 1 Septemba 2026: Vodacom Tanzania Plc leo imezindua ripoti ya Mazingira, Jamii na Utawala (ESG) kwa mwaka uliomalizika Machi 31, 2026, ikionesha kupungua kwa asilimia 24 ya hewa chafu, sambamba na mpango mkubwa zaidi wa uboreshaji wa mtandao katika historia ya kampuni.

Kampuni pia imewekeza shilingi 3.5 bilioni katika ufanisi wa nishati kwa mwaka huu, na kufikisha uokoaji wa megawati 18,340, ikiwa zaidi ya mara sita ya megawati 2,861 zilizookolewa kwa mwaka wa 2025. 

Uzalishaji wa hewa chafu ulishuka hadi tani 18,445.5, kutoka tani 24,285.6. Pia, matumizi ya mafuta dizeli yalipungua kwa asilimia 24, kutoka lita milioni 8.6 hadi lita milioni 6.6.

Upunguaji  huo ulitokana na kubadilisha vifaa vya zamani vya mawasiliano ya redio katika maeneo 1,808 ndani ya miezi saba, pamoja na uimarishaji wa upatikanaji wa umeme wa gridi uliopunguza muda wa uendeshaji wa jenereta katika vituo vya data vya kampuni.

Mtandao wa Vodacom Tanzania unatumia takriban jigawati (GWh) 169.5 kwa mwaka katika zaidi ya maeneo 3,800, ambapo 2,190 kati yake yapo vijijini. Vituo vya msingi vinachukua asilimia 78.9 ya matumizi yote.

Mwaka huu, maeneo 169 yaliyokuwa nje ya gridi ya taifa yaliunganishwa kwenye gridi ya taifa. Katika kituo cha data cha Kwale, umeme wa gridi ya Taifa uliongezeka kutoka 11kVA hadi 33kVA na kupunguza matumizi ya  jenereta kutoka saa 18 kwa siku hadi saa mbili, sawa na upunguzaji wa asilimia 88 wa matumizi ya dizeli katika kituo hicho.

Asilimia 57 ya nishati yote iliyotumiwa na Vodacom Tanzania ilitokana na vyanzo vya nishati jadidifu. Kampuni iliendelea kuhakikisha kuwa umeme wote wa gridi iliyonunua unaendana na nishati inayotokana na vyanzo jadidifu, hatua iliyosaidia kufikia uzalishaji sifuri wa hewa chafuzi. Aidha, Vodacom Tanzania ilihuisha tena cheti chake cha ISO 50001. Uzalishaji wa hewa chafuzi unaotokana na shughuli zake za biashara na mnyororo wake wa thamani pia ulipungua hadi tani 94,944 kutoka tani 100,455.

"Mafanikio haya ya kimazingira yametokana na kufanya uhandisi wa msingi kwa usahihi, siyo kutoka mradi tofauti wa uendelevu," alisema Mkurugenzi wa Miundombinu ya Mtandao Andrew Lupembe huku akiongeza, "kubadilisha vifaa vya zamani katika maeneo 1,808 kunampa mteja muunganisho wa haraka zaidi huku taifa likifaidika na upunguzaji wa athari za mazingira ambazo zingesababishwa na lita milioni mbili zilizopunguzwa kwenye matumizi.” 

Wigo wa mtandao wa 4G ulifikia asilimia 76.3 ya wakazi, huku wateja milioni 27.7 wakiwa kwenye mtandao baada ya uzinduzi wa huduma ya kwanza ya 5G nchini Tanzania. Umiliki wa simujanja ulifikia asilimia 46.7, huku wateja 325,415 wakipata vifaa kupitia ubia wa mikopo ya rejareja. 

Kwa wateja wasio na simujanja, huduma mpya ya kidijitali inayotumia akili unde inawezesha upatikanaji wa intaneti kupitia jumbefupi (SMS) na simu za sauti, ikisambaza msaada wa kidijitali hadi maeneo ya vijijini.

M-Pesa ilihudumia wateja milioni 14.1 wa ujumuishwaji wa kifedha huku M-Koba, jukwaa la kidijitali la vikundi vya akiba ambao wanachama wake wengi ni wanawake, lilifikia vikundi hai 299,420 huku akiba jumla ikiongezeka kwa asilimia 81.Vodacom Tanzania Foundation ilifikia wanufaika milioni 2.9, kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania, kampuni iliondoa gharama ya data kwenye jukwaa la kitaifa la maendeleo ya walimu, na kuwapa walimu 121,832 fursa ya kupata nyenzo za maendeleo ya kitaaluma bila gharama ya data. Miti 80,000 ya asili iliongezwa katika Msitu wa Kahe 2 katika Mlima Kilimanjaro.

Kampuni ilirekodi mwaka wa kumi na nne mfululizo bila kutokea kifo cha mfanyakazi mahali pa kazi. Mpango wa uboreshaji ulihusisha wafanyakazi 411 waliosafiri zaidi ya kilomita milioni 1.7, na awamu ya kwanza ilikamilika bila kutokea kifo au tukio kubwa. Vodacom Tanzania ina uthibitisho wa ISO 27001 kwa usalama wa data na haikurekodi faini yoyote ya ushindani usio halali au utakatishaji fedha."Nyuma ya kila muunganisho kuna maisha yanayobadilika, mwalimu anayefikia nyenzo za kujifunzia bila gharama ya data, kikundi cha akiba ambacho hakihifadhi tena fedha taslimu katika bati. Tutaendelea kuwajibika kwa wananchi wa Tanzania wanaotuamini kila siku,” aliongeza Philip Besiimire, Afisa Mtendaji mkuu wa kampuni hiyo.


Kutoka kushoto: Tahir Mussa, Kaimu Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade; Juma Burhan, Mkurugenzi Mtendaji wa ZEEA; na Fatma Ahmed, Mkuu wa Huduma za Kibenki kwa Wafanyabiashara, Benki ya Stanbic, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Zanzibar jana kutangaza ushirikiano huo.
Stanbic Bank Tanzania imetangaza udhamini wa TZS milioni 200 kwa maonesho ya Fahari ya Zanzibar 2026, hatua inayoonesha dhamira yake ya kuendelea kuchangia ukuaji wa uchumi wa Zanzibar na kuwawezesha wafanyabiashara, wajasiriamali na jamii kwa ujumla.
 
Maonesho hayo yatafanyika kuanzia tarehe 4 hadi 14 Septemba 2026 katika Viwanja vya Maisara, Zanzibar, yakibeba kaulimbiu “Bidhaa Zetu Ndio Fahari Yetu.” Zaidi ya washiriki 300 na wageni 15,000 wanatarajiwa kushiriki katika tukio hilo, linalolenga kuhamasisha matumizi ya bidhaa zinazozalishwa nchini. Maonesho hayo yameandaliwa na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE).
 
Kama mdhamini mkuu, Stanbic Bank itatumia maonesho hayo kuonesha suluhisho mbalimbali za kifedha zinazolenga kusaidia ukuaji wa biashara, kuwezesha biashara za ndani na za kimataifa, pamoja na kukuza ushiriki wa wafanyabiashara katika fursa za masoko mapya.
 
Akizungumza kuhusu ushiriki wa benki hiyo, Fatma Ahmed, Mkuu wa Huduma za Kibenki kwa Wafanyabiashara, Stanbic Bank Tanzania, alisema ushirikiano huo unaakisi imani ya benki katika nafasi ya Zanzibar kama kitovu muhimu cha biashara na uwekezaji.
 
"Fahari ya Zanzibar ni jukwaa linaloonesha ubunifu, juhudi na uwezo wa wafanyabiashara wa Zanzibar. Sisi tunaendelea kujenga mazingira yatakayowasaidia kukuza biashara zao, kuongeza ushindani na kufikia masoko mapana zaidi. Zanzibar ni nyumbani kwetu, na tutaendelea kuunga mkono safari yake ya maendeleo ya kiuchumi," alisema.
 
Maonesho hayo pia yatahusisha mijadala na shughuli mbalimbali zinazolenga vijana, ubunifu, utalii, sanaa, biashara na ujumuishaji wa kiuchumi.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akizindua Programu ya Mining for a Brighter Tomorrow (MBT) katika eneo la Nyamongo, mkoani Mara, inayolenga kupanua fursa za maeneo ya uchimbaji, taarifa za kijiolojia na leseni kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Helikopta ikifanya utafiti wa madini kwa njia ya anga katika eneo la Nyamongo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya MBT, hatua itakayosaidia kupata taarifa za kijiolojia kwa ajili ya utafiti wa kina na uchorongaji katika maeneo yaliyotengwa kwa wachimbaji wadogo.