Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt Dorothy Gwajima akiangalia mojawapo ya magodoro ambayo yamewekewa kitambaa cha mpira ili yasiharibike kwa haraka.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt Dorothy Gwajima akizungumza na uongozi wa halmashauri ya Kigamboni wakati walipokagua hali ya utoaji huduma katika Hospitali ya Vijibweni ambayo ndiyo inayotoa huduma kama hospitali ya wilaya hiyo.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt Dorothy Gwajima akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi na wafanyakazi wa hospitali ya Vijibweni wilayani Kigamboni.

Mashine mpya ya Xray yenye thamani ya shilingi milioni 153 ambayo imenunuliwa kwa mkopo na Hospitali ya Vijibweni kwa ajili ya kutoa huduma ya kipimo hicho kwa wakazi wa wilaya ya Kigamboni ambao wamekuwa wakilazimika kufuata huduma hiyo katika hospitali za wilaya nyingine za mkoa wa Dar es salaam.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es saaam Dkt Yudas Ndungile akielezea mikakati ya mkoa wake katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za afya zinazoukabili mkoa wa Dar es salaam jana wakati wa ziara ya Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt Dorothy Gwajima katika Hospitali ya Vijibweni

Na Mathew Kwembe, Dar es Salaam

Serikali imewataka Waganga Wakuu wa Mikoa na wa Halmashauri kuhakikisha kuwa ndani ya wiki mbili kuanzia sasa wawe wamekwishanunua vitambaa vigumu vya mpira ambavyo hutumika kuyafunika magodoro yanayotumiwa na wagonjwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili yasiweze kuharibika kwa haraka.

Agizo hilo limetolewa jana na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt Dorothy Gwajima wakati alipofanya ziara kutembelea hospitali ya Vijibweni iliyopo eneo la Kigamboni jijini Dar es salaam.

Amesema anatoa siku 14 kuanzia sasa kwa waganga wakuu wa mikoa na halmashauri kuhakikisha kuwa magodoro yaliyopo kwenye Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati kwenye mikoa yao yanashonwa na kuwekea mifuko maalum ya mpira ili kuyafanya yarudi katika ubora wake.

Ameongeza kuwa kumekuwa na mtindo kwa baadhi ya watendaji wa halmashauri kusingizia uchakavu wa magodoro na vitanda kwa vile tu Bohari kuu ya Dawa ilileta magodoro yenye vitambaa laini vya mpira na ni siku nyingi tangu magodoro hayo yaletwe.

“Watendaji wengine wamekuwa wakidai kuwa MSD wametuuzia magodoro haya siku nyingi na kitambaa chake laini hivyo yameanza kuchoka,”amesema na kuongeza:

“Wakati inawezekana kununua kitambaa cha mpira, kwenye maduka yaliyopo yanayouza vitambaa vya mpira, mafundi wapo na kwa kuwatumia mafundi wenyeji wakashona magodoro haya yakarudi kuwa mapya,” amesema.

Dkt Gwajima ameongeza kuwa hakuna sababu kwa watendaji hao kutumia visingizio vyao kwani bei ya kununulia mita kadhaa za vitambaa vigumu vya mpira na za mashono ni ndogo na ni gharama zilizo ndani ya uwezo wa vituo vyetu vya kutolea huduma za afya.

Wakati huo huo, Dkt Gwajima amesifu hatua ya uongozi wa hospitali ya Vijibweni iliyopo wilayani Kigamboni kwa kuamua kukopa mashine ya Xray kutoka MSD ili waweze kuwahudumia wananchi walio wengi.

Amesema hatua hiyo ni nzuri kwani itawaondolea kero wananchi wengi waliokuwa wanalazimika kufuata huduma hiyo mbali na eneo hilo hivyo Dkt Gwajima amezitaka halmashauri nyingine za wilaya nchini kuiga mfano wa hospitali hiyo kwa kuhakikisha kuwa wanatumia vyanzo vyao vya mapato ya ndani kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

“Tunazo hospitali zetu nyingi ambazo zinasubiri mgao wa serikali, hii haiwezekani, tunachosema ni kwamba kila hospitali itasimama yenyewe kupitia timu yake ya usimamizi huduma za afya ya halmashauri kwa kupanua wigo wa huduma na kuvutia wateja wengi zaidi kutumia huduma hizo badala ya kuzifuata mbali na makazi yao kwa gharama kubwa,” amesisitiza Dkt Gwajima.

Naibu katibu Mkuu ameongeza kuwa kupitia uchangiaji wa huduma hizo kama walivyofanya Vijibweni ni dhahiri kuwa, vituo husika vitaweza kumudu gharama za kununua mahitaji mbalimbali ya kuboresha huduma za afya badala ya kutegemea serikali tu.

Akizungumzia kuhusu kuwepo kwa misongamano ya wagonjwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, Dkt Gwajima amesema pamoja na ukweli kuwa baadhi ya maeneo kumekuwa na upungufu wa watumishi, yapo baadhi ya maeneo ambayo upungufu huo unachangiwa na uzembe wa baadhi ya watoa huduma katika kuwajibika.

“Baadhi ya wataalam huwa wanachelewa kufika kazini na wakifika wanaishia kuona idadi ndogo ya wateja chini ya kiwango cha walau wateja 30 hadi 40 kwa siku kilichopo kwenye miongozo,” amesisitiza Dkt Gwajima

Aidha, amesema kuwa yapo baadhi ya maeneo ambayo yana watoa huduma wengi zaidi kuliko ilivyotakiwa nayo haya yanahitaji kupanguliwa wapelekwe waliko wachache.

Dkt Gwajima ameeleza kuwa ni kweli upungufu upo ila, upungufu huo hauwezi tu kupimwa kwa maneno ya mazoea bali kwa kupima uwingi wa kazi kwa kila mtoa huduma kwa wakati huo.

“Kupitia utaratibu wa kupima uwingi wa kazi kwa wakati wa sasa (workload) inawezekana kuchochea uwajibikaji wa mtumishi mmoja mmoja na kuleta uwiano sawa wa kazi miongoni mwa watumishi wa vituo mbalimbali na siyo baadhi wanasema kuna upungufu wa watumishi akiulizwa amehudumia wateja wangapi unakuta hata kumi hawafiki,” amesema.

Dkt. Gwajima amesema, lazima hoja ipimwe kwa takwimu ndipo tutaweza kujiridhisha kwani maeneo yote hayafanani.

Pamoja na kutembelea hospitali ya Vijibweni, Dkt Gwajima alipata fursa pia ya kutembelea na kushuhudia ujenzi wa hospitali za wilaya za kigamboni na Ilala ambapo kwa upande wa hospitali ya Kigamboni Naibu Katibu Mkuu aliusifu uongozi wa halmashauri hiyo kwa usimamizi thabiti uliopelekea majengo ya hospitali kuwa katika hatua ya kupaua tofauti na wenzao wa Manispaa ya Ilala ambao wao majengo matatu kati ya saba yapo katika hatua za msingi.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Dkt. Yudas Ndungile amesema kuwa wao wameyapokea maagizo ya Naibu Katibu Mkuu na kwamba maagizo hayo yanatekelezeka kwa vile yapo ndani ya uwezo wa mkoa wake.

Naibu Katibu Mkuu yupo katika ziara ya kikazi kutembelea mikoa ya Dar es salaam na Pwani ambapo kabla ya hapo alitembelea mikoa ya Morogoro, Dodoma, Njombe, Ruvuma, Iringa na Manyara.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: