MFANYABIASHARA Khamis Luwonga maarufu kwa jina la Meshack (38), anayedaiwa kumuua mkewe na kisha kumchoma na moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa, amefikishwa katika Mahakama Hakimu Mkazi Kisutu kujibu tuhuma hizo za mauaji ya mke wake, Naomi Marijani.

Akisoma hati ya mashtaka Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon amedai leo mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Salum Ally kuwa mshtakiwa anatuhumiwa kwa kosa moja la mauaji kinyume cha Sheria ya kanuni ya adhabu namba 196 sura 16 kama kilochofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Katika kesi hiyo ya mauaji namba 4 ya mwaka 2019, mshtakiwa Luwonga Mkazi wa Kigamboni, Dar es Salaam anadaiwa Mei 15, mwaka huu wa 2019 akiwa Gezaulole eneo la Kigamboni alimuua mkewe Naomi Marijani.

Hata hivyo, mshtakiwa hakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji ambazo kwa kawaida zinasikilizwa mahakama kuu.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 13, mwaka huu kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika au la.

Mshtakiwa huyo pindi anatolewa mahabusu na kupandishwa mahakamani, alifunika sura yake kwa kutumia kofia ya koti lake kwa lengo la kutokuonekana sura yake. 

Mwanzoni mwa Julai mwaka huu, mshtakiwa Meshack alisambaza tangazo magazetini na kwenye mitandao ya kijamii kuwa anamtafuta mkewe ambaye alitoweka ghafla lakini baadae Jeshi la Polisi kupitia Mkuu wa Upepelezi wa kanda hiyo, Camillius Wambura alitangaza kumshikilia Luwonga akidaiwa kumuua na kisha aliuchoma moto mwili wa mkewe. 
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: