Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF) limepiga marufuku kuingia Mashabiki katika mchezo wa raundi ya nne ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Kundi A kati ya wenyeji Simba SC dhidi ya wageni El Merreikh kutoka Sudan, mchezo utakaopigwa March 16, 2021 kwenye dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Saa 10:00 Jioni.

Sababu kubwa ya kuzuia Mashabiki kuingia Uwanjani katika mchezo huo ni ongezeko la maambukizi ya virusi vya COVID-19 hususani duniani kote.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Dar es Saalam, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Haji Manara amesema tayari wamepata taarifa kutoka Shirikisho la Soka nchini (TFF) zuio la Mashabiki kuingia Uwanjani kupitia Shirikisho la CAF linalosimamia masuala ya mpira wa miguu barani Afrika.

Manara amesema licha ya katazo hilo, Simba SC itacheza mchezo huo bila kuwa na Mashabiki hao pasipo na malalamiko yoyote, amesema hawana hofu yoyote kutokana na kuzoea hali hiyo katika michezo yake dhidi ya AS Vita Club ya DR Congo na kupata ushindi wa bao 1-0 katika dimba la Stade de Martyrs na mchezo dhidi ya El Merreikh nchini Sudan ambapo walipata sare ya 0-0.

Pia amewataka Mashabiki kutoa unyonge kutoka na maamuzi hayo ya CAF, amesema Simba SC na TFF hawana budi kukubali agizo hilo kutoka kwenye Mamlaka hiyo inayosimamia Soka la Afrika, “Tutaangalia uwezekano wa kukusanya Mashabiki wetu sehemu mbalimbali ili kuangalia mechi hiyo pamoja”, amesema Manara.

“Na mchezo huu wa Jumanne, Simba SC tutaingia na kaulimbiu ya ‘Vita ya Kimyakimya’ (Silent Killer) ili kuhakikisha tunapata ushindi na kuendelea kuongoza Kundi A ambapo hadi sasa tuna alama Saba”, ameeleza Manara.

Katika mchezo wao wa mwisho wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba SC walitoka sare ya 0-0 na El Merreikh mjini Khartoum nchini Sudan katika dimba la Al Hilal na kufikisha alama Saba, ikituatiwa na AS vita Club wenye alama Nne sambamba na Al Ahly SC wenye alama Nne wakati El Merreikh wakiburuza mkia na alama Moja.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: