Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Dar es Salaam. Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imemvua uanachama aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Emmanuel Nchimbi, siku moja baada ya kujiuzulu nafasi hiyo na kutangaza kustaafu shughuli za kisiasa.

Uamuzi huo ulifikiwa Jumatano, Agosti 26, 2026, na kutangazwa usiku huo na Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Asha-Rose Migiro, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi Ndogo za CCM, Lumumba, jijini Dar es Salaam.

Dk. Migiro amesema Halmashauri Kuu ilipitia taarifa mbalimbali pamoja na Katiba ya CCM kabla ya kufikia uamuzi wa kumvua Nchimbi uanachama kwa kile kilichoelezwa kuwa ni ukiukwaji wa maadili.

Amesema uamuzi huo umefikiwa kwa kauli moja baada ya chombo hicho cha chama kupitia taarifa zilizowasilishwa na masharti yaliyowekwa kwenye Katiba ya CCM.

“Baada ya kupitia taarifa zote zilizokuwepo, Katiba za CCM, kwa kauli moja Halmashauri Kuu imefikia uamuzi kwamba, kutokana na ukiukwaji wa maadili, afukuzwe uanachama na CCM imefikia uamuzi huo. Si mwanachama wa CCM tena,” amesema Dk. Migiro.
Uamuzi huo umefanyika baada ya Nchimbi, Jumanne Agosti 25, 2026, kumwandikia Rais Samia Suluhu Hassan barua ya kuomba kujiuzulu nafasi ya Makamu wa Rais na wakati huo huo kutangaza kustaafu shughuli za kisiasa.

Katika barua yake, Nchimbi alisema ameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kujiridhisha kuwa Rais Samia anahitaji mabadiliko katika uongozi.

“Nimejiridhisha pasipo shaka kuwa Mhe. Rais anatamani mabadiliko, hivyo nimeamua kutimiza ahadi yangu,” alisema.

Nchimbi pia alieleza kuwa Agosti 27, 2025 alimwahidi Rais Samia kuwa angemsaidia yeye na nchi kwa uwezo wake wote na kwa uaminifu, huku akiahidi kwamba endapo Rais angeona anahitaji Makamu mwingine wa Rais, angeachia nafasi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa yake, Nchimbi aliomba kujiuzulu kuanzia Septemba 4, 2026, akirejea Ibara ya 50(2)(c) ikisomwa pamoja na Ibara ya 149(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika hatua nyingine, Halmashauri Kuu ya CCM imepitisha jina la Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, kuwa mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais, baada ya kujiuzulu kwa Nchimbi.

Hatua hiyo imekuja wakati Serikali ikianza mchakato wa kujaza nafasi hiyo kwa kuzingatia taratibu za kikatiba.

Ndejembi amekuwa akihudumu serikalini akiwa Waziri wa Nishati, na kupitishwa kwa jina lake na Halmashauri Kuu ya CCM kunaweka msingi wa mchakato wa kumpata Makamu mpya wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nchimbi amekuwa kiongozi wa muda mrefu ndani ya CCM, akianza kushika nafasi za uongozi katika chama hicho tangu mwaka 1998 alipokuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).

Baadaye alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), nafasi iliyompa pia uwakilishi katika Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho.

Januari 15, 2024, aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM na Halmashauri Kuu ya Taifa, akichukua nafasi ya Daniel Chongolo aliyejiuzulu.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Nchimbi aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais na kuapishwa Novemba 3, 2025.

Kujiuzulu kwake, kuvuliwa uanachama wa CCM na kupitishwa kwa jina la Ndejembi kunafungua sura mpya katika uongozi wa Serikali na chama, huku hatua za kikatiba zikisubiriwa kukamilisha mchakato wa kumpata Makamu mpya wa Rais.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: