Tunapoelekea kuadhimisha Siku ya Tiba Asili ya Mwafrika tarehe 31 Agosti 2026, Afrika inakabiliwa na swali moja kubwa: Je, tutaendelea kutumia urithi wa tiba asilia kama ulivyo, au tutautafiti, kuuthibitisha, kuuboresha na kuugeuza kuwa sehemu ya suluhisho la afya na uchumi wa kizazi kijacho?

Na Mwandishi Wetu

Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania (TRAMEPRO) limetoa wito kwa Serikali, watafiti, vyuo vikuu, sekta binafsi na wadau wa afya kushirikiana kuifanya tiba asili kuwa nguzo muhimu ya huduma za afya, maendeleo ya sayansi na ukuaji wa uchumi wa Afrika.

Wito huo umetolewa wakati Afrika ikijiandaa kuadhimisha Siku ya Tiba Asili ya Mwafrika itakayoadhimishwa Agosti 31, 2026, yenye kaulimbiu inayosisitiza umuhimu wa utafiti na maendeleo katika tiba asili ili kufikia huduma bora za afya kwa wote.

TRAMEPRO imesema kwa karne nyingi jamii za Afrika zimekuwa zikitumia mimea tiba na maarifa ya jadi katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za afya, lakini maarifa hayo yako hatarini kupotea kutokana na wazee na wataalamu wanaoyamiliki kuzeeka huku mengi yakiwa hayajaandikwa.

Shirika hilo limeeleza kuwa pamoja na kupotea kwa maarifa, uharibifu wa mazingira, ukataji wa misitu, mabadiliko ya tabianchi na uvunaji holela wa mimea tiba vinaendelea kutishia mustakabali wa tiba asili barani Afrika.

Kwa mujibu wa TRAMEPRO, kulinda tiba asili kunamaanisha pia kulinda bioanuwai, mazingira na urithi wa maarifa ya jadi ambayo yamekuwa msingi wa huduma za afya kwa vizazi vingi.

Aidha, shirika hilo limesema sekta ya tiba asili inahitaji takwimu sahihi kuhusu wataalamu, vituo vya huduma, mimea tiba, bidhaa zinazozalishwa na idadi ya wananchi wanaotumia huduma hizo ili kusaidia kupanga sera, uwekezaji na maendeleo ya sekta hiyo.

TRAMEPRO imeeleza kuwa dunia imeanza kutambua nafasi ya tiba asili kufuatia kupitishwa kwa Mkakati wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wa Tiba Asili wa mwaka 2025–2034, unaolenga kuimarisha ushahidi wa kisayansi, usalama, ubora na ujumuishaji wa tiba asili katika mifumo ya afya.

Shirika hilo limesisitiza kuwa Afrika inapaswa kuwa kinara wa utafiti, ubunifu na uzalishaji wa bidhaa za tiba asili badala ya kubaki msambazaji wa malighafi zinazoongezewa thamani nje ya bara.

Aidha, limebainisha kuwa Tanzania ina rasilimali muhimu ikiwemo mimea tiba, wataalamu, vyuo vikuu na taasisi za utafiti, lakini kunahitajika ushirikiano mkubwa zaidi ili kuunganisha utafiti, maabara, uzalishaji wa bidhaa salama na masoko.

TRAMEPRO pia imesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya kuthibitisha usalama, ubora na ufanisi wa dawa za asili, pamoja na kuweka utaratibu wa kufuatilia madhara yanayoweza kujitokeza kwa watumiaji.

Kwa upande wa mazingira, shirika hilo limependekeza kuanzishwa kwa mashamba ya mimea tiba, kuhamasisha kilimo endelevu na kuongeza juhudi za kuhifadhi misitu na bioanuwai ili kuhakikisha rasilimali hizo zinaendelea kuwepo kwa vizazi vijavyo.

Aidha, limeeleza kuwa sekta ya tiba asili ina uwezo mkubwa wa kuchochea uchumi kupitia mnyororo wa thamani unaohusisha kilimo cha mimea tiba, utafiti, uzalishaji wa bidhaa, biashara na ajira kwa vijana.

TRAMEPRO imewataka wataalamu wa tiba asili kukumbatia sayansi, teknolojia na utafiti ili kuongeza ubora wa huduma na kuimarisha imani ya jamii, huku ikisisitiza kuwa matumizi ya teknolojia za kisasa, ikiwemo akili mnemba (AI), yanaweza kusaidia kuhifadhi maarifa na kuharakisha tafiti.

Shirika hilo limependekeza pia kuanzishwa kwa ajenda mpya ya kitaifa ya tiba asili itakayojumuisha utafiti, uhifadhi wa maarifa ya jadi, uwekezaji, matumizi ya teknolojia, usajili wa bidhaa na ulinzi wa haki za jamii zinazomiliki maarifa hayo.

TRAMEPRO imehitimisha kwa kutoa wito kwa Serikali, watafiti, vyuo vikuu, sekta binafsi, mashirika ya kiraia na wananchi kushirikiana kujenga tiba asili yenye ushahidi wa kisayansi, salama, yenye viwango, inayolinda mazingira na kuchangia huduma bora za afya pamoja na maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: