Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza wakati ya kufunga Mkutano wa nne wa Wadau kuhusu Tathmini ya Utekelezaji wa Mkakati wa Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano, Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Sehemu ya Viongozi wa Mahakama na Wadau wengine wakiwa katika Mkutano wa nne wa Wadau kuhusu Tathmini ya Utekelezaji wa Mkakati wa Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara tarehe 16 Septemba, 2026 uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano, Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Wajumbe wa Mkutano wakifuatilia hotuba ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (hayupo katika picha) alipokuwa akifunga Mkutano wa nne wa Wadau kuhusu Tathmini ya Utekelezaji wa Mkakati wa Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara tarehe 16 Septemba, 2026 uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano, Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (kulia) akichangia jambo wakati wa Mkutano wa nne wa Wadau kuhusu Tathmini ya Utekelezaji wa Mkakati wa Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano, Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. (Picha na Mary Gwera, Mahakama).
Na Habiba Mbaruku, Mahakama-Dodoma
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju ametoa rai kwa wadau wanaoshughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara kuchukua tahadhari na hatua madhubuti za kukabiliana na mvua za El nino kufuatia taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) juu ya uwepo wa mvua hizo kuanzia mwezi Oktoba mwaka huu.
Mhe. Masaju ametoa ushauri huo tarehe 16 Septemba, 2026 alipokuwa akifunga Mkutano wa nne wa Wadau kuhusu Tathmini ya Utekelezaji wa Mkakati wa Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano, Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Akizungumza na Wadau hao, Mhe. Masaju amesema kuwa, Serikali inachukua hatua za kujikinga na kukabiliana na janga hilo hivyo, na wao wanapaswa kuchukua tahadhari kila mmoja na kutazama ni kwa namna gani wanaweza kuendeleza shughuli ikiwa mvua hizo zitakuwepo, pia kila mmoja kwa imani yake kumuomba Mwenyezi Mungu bila kusubiri kuambiwa na viongozi wa dini na pasipo kuringia kiburi cha uzima.
“Wadau wa haki mmejiandaa vipi, TLS mmeshaandaa namna gani ya kuendelea kusikiliza mashauri haya, wakati pengine njia barabarani hazifikiki, kwenye ‘Law fame’ zenu mna vyumba vya kutosha, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na wadau wengine humu tumejiandaa namna gani, hayo ndiyo ya kutafakari, sisi wenyewe kwenye sekta hii tuchukue hatua namna gani tutaendeleza shughuli zetu kama hilo janga litakuwepo, lakini pia na kumuomba Mwenyezi Mungu atukinge alitupilie mbali hilo janga, tusiwe na kiburi cha uzima, tuone kama Mungu yupo, maji yana nguvu Ghorofa hazisaidii kitu chochote,” amesema Jaji Mkuu.
Aidha, amesisitiza juu ya maombi huku akirejea Kitabu cha Zaburi 103, kama muongozo katika maombi ambayo itawawezesha wadau kuomba kwa yale ambayo yapo nje ya uwezo wao kuyadhibiti, basi Mwenyezi Mungu kwa rehema na fadhili zake aingilie kati na kuliepusha Taifa na janga hilo kwa sababu hakuna ambaye ana kinga ya uhakika ya kujiweka salama pindi janga hilo litakapotokea.
“Sisi wengine hatuna kinga ya kutofikiwa na hayo majanga ya elnino kama yatakuwepo, yapo mengine yapo nje ya uwezo wetu, na mimi naamini uwepo wa Mwenyezi Mungu, kila mmoja hapa hakuna ambaye anakinga ya kutokufa kwa majanga, kila mmoja achukue tahadhari na kumuomba Mwenyezi Mungu, lazima tuwe tayari kumuomba kwa rehema, neema na fadhili zake kwa mujibu wa Zaburi ya 103 ambayo tunaishi kwayo, anaweza kuingilia kati akatunusuru kwakuwa hata uwezo wetu wa kujikinga na hayo majanga ni mdogo,” ameongeza Mhe. Masaju.
Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu amebainisha changamoto ambazo zinasababisha ucheleweshaji wa usikilizaji wa mashauri ya kiuchumi, ambazo amezitaja kuwa ni changamoto zinazotokana na Mahakama yenyewe, changamoto za kisheria na changamoto zinazotokana na wadau.
Amesema kuwa, changamoto zinazotokana na Mahakama yenyewe ni hasa zile za kisheria, ambazo zinaambatana na mfumo wa kitaasisi na kushauri kuwa wadau waendelee kubaini changamoto hizo na kuzijadili kwa pamoja ili kuzipatia ufumbuzi pale ambapo mhusika amekwama kuzitatua.
Amezitaja changamoto hizo kuwa ni ufunguaji wa mashauri kwa lengo la kuchelewesha ulipaji wa madeni, ambapo watu hufungua mashauri mahakamani ili wasiwajibike kulipa deni na kuongeza kuwa, kukiwa na riba rafiki na upatikanaji wa elimu hususan elimu ya mikopo na masuala ya bima watu watapata uelewa wa kutosha na kufahamu wajibu wao na namna gani wanawajibika.
Kadhalika, ameitaja changamoto nyingine kuwa, ni matumizi ya mbinu za kiufundi ili kuchelewesha usikilizaji na uamuzi wa mashauri, hali ya kuwa Katiba imetoa muongozo wa kutofungwa kupita kiasi na masharti ya kiufundi yanayoweza kukwamisha haki kutendeka akirejelea Ibara ya 107A(2)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, (1977).
“Matumizi ya mbinu za kiufundi ili kuchelewesha usikilizaji na uamuzi wa mashauri hizi (legal technicalities), wakati Katiba imetoa mwongozo kwamba tusifungwe kupita kiasi na masharti ya kiufundi yanayoweza kukwamisha haki kutendeka, hilo sharti limetajwa kwenye Ibara ya 107A(2)(e) haki inapaswa itendeke, tunapojiendekeza kwenye hizi hili tunaahirisha tu mgogoro hatuwezi kutatua mgogoro,” ameongeza Mhe. Masaju.
Pamoja na hayo, Jaji Mkuu amesema kwamba, wadau wanapaswa kuendelea kudhibiti hatua zinazochelewesha usikilizaji wa migogoro kwa kurahisisha matumizi ya notisi ya siku 90, kwa kuangalia wanaohusika kumfanya yule anayepewa notisi kutaka kushtakiwa, awajibike kuchukua hatua ambazo ni za kutatua na ikiwa ni hatua za usuluhishi wajadiliane ili kurahisisha usikilizaji wa migogoro na kuwataka wanaohusika na kuchakata notisi wawajibike ili kumaliza migogoro mapema ipasavyo.
“Wale wanaohusika na kuchakata hizo notisi zinazotolewa na watu wanaotaka kuishtaki Serikali na Taasisi zake, wawajibike kushughulikia hiyo changamoto inayopelekea watake kushtakiwa, kwa namna hiyo migogoro mingi itaisha,” amesema Mhe. Masaju.
Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu ameongeza kuwa, uwajibikaji ni moja ya nyenzo inayotajwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050 pia ni sharti la kikatiba kama Ibara ya 25 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyosisitiza juu ya uwajibikaji, kujituma na kuzingatia nidhamu ili kufikia malengo yaliyowekwa, hivyo ameipongeza Tume ya Taifa ya Mipango kwa mkakati wanaouweka ili kuleta uwajibikaji.
“Uwajibikaji ni sharti la kikatiba, kitu kikishawekwa kwenye sheria tunawajibika kukitekeleza kwa sababu huwa kuna adhabu usipokitekeleza kwa hiyo Ibara ya 25 ya Katiba inatusisitiza juu ya uwajibikaji lakini pia inasisitiza juu ya kujituma na inasisitiza juu ya kuzingatia nidhamu ya kazi ili kufikia malengo tuliyojiwekea,” amesema Mhe. Masaju.
Aidha, katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), amesema Mahakama imepiga hatua kubwa kwa kuweka mifumo mbalimbali ya matumizi ya TEHAMA huku mifumo mingine ikiendelezwa na kuwasisitiza wadau hao kuendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA kama yanavyosisitizwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050. Ametaja manufaa ya kutumia TEHAMA katika utendaji kuwa ni pamoja na kupunguza matumizi ya karatasi ili kuimarisha mwenendo wa mashauri, kupunguza muda na gharama za kiutawala, kuongeza uwazi na uwajibikaji, kuwezesha upatikanaji wa taarifa mapema ipasavyo na kutoa takwimu zinazoweza kusaidia katika kupanga na kupima utendaji wa Mahakama.
Akihitimisha hotuba yake, Jaji Mkuu amemtaka kila mdau wa haki kujitathmini, kubaini changamoto zake za kiuwezo, kiutendaji na kimaadili na kuzifanyia kazi ili kwa pamoja kufikia matarajio ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050.






Toa Maoni Yako:
0 comments: