Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, anayeshughulikia Huduma za Hazina, Bw. Nsubili Joshua, akisalimiana na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Wizara ya Fedha, Bi. Fauzia Nombo, alipowasili katika Ofisi za Hazina Ndogo Morogoro, kwa ajili ya kufungua mafunzo elekezi kwa watumishi wa Ajira Mpya wa Wizara ya Fedha, yanayofanyika katika Ofisi za Hazina Ndogo mkoani Morogoro.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, anayeshughulikia Huduma za Hazina, Bw. Nsubili Joshua, (kushoto), akijadiliana jambo na Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA. Leonard Mkude, katika Ofisi za Mkuu wa Hazina Ndogo - Morogoro kabla ya kufungua mafunzo elekezi kwa watumishi wa Ajira Mpya wa Wizara ya Fedha, yanayofanyika katika Ofisi za Hazina Ndogo mkoani Morogoro.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, anayeshughulikia Huduma za Hazina, Bw. Nsubili Joshua, akizungumza wakati wa kufungua mafunzo elekezi kwa watumishi wa Ajira Mpya wa Wizara ya Fedha, yanayofanyika katika Ofisi za Hazina Ndogo mkoani Morogoro.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Wizara ya Fedha, Bi. Fauzia Nombo, akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa watumishi wa Ajira Mpya wa Wizara ya Fedha, yanayofanyika katika Ofisi za Hazina Ndogo mkoani Morogoro.
Maafisa Utumishi, kutoka Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Wizara ya Fedha, wakimsikiliza Mgeni Rasmi wa mafunzo elekezi kwa watumishi wa Ajira Mpya wa Wizara ya Fedha, ambaye ni Naibu katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, anayeshughulikia Huduma za Hazina Bw. Nsubili Joshua (hayupo pichani), yanayofanyika katika Ofisi za Hazina Ndogo mkoani Morogoro.
Afisa Kumbukumbu na Nyaraka kutoka Chuo Cha Utumishi wa Umma, Bw. Felician Rogatian, akitoa elimu kuhusu masuala ya utunzaji wa Kumbukumbu na nyaraka za Serikali kwa watumishi wa Ajira Mpya wa Wizara ya Fedha, wakati wa mafunzo elekezi kwa watumishi hao yanayofanyika katika Ofisi za Hazina Ndogo mkoani Morogoro.
Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo Cha Utumishi wa Umma nchini, Bw. Georges Ngonyani, akitoa mafunzo kwa watumishi wa Ajira Mpya wa Wizara ya Fedha, yanayofanyika katika Ofisi za Hazina Ndogo mkoani Morogoro.
Baadhi ya watumishi wa Ajira Mpya wa Wizara ya Fedha, wakifuatilia mafunzo elekezi kwa watumishi hao, yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha, yanayotolewa na Wahadhiri kutoka Chuo Cha Utumishi wa Umma, yanayofanyika katika Ofisi za Hazina Ndogo mkoani Morogoro.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, anayeshughulikia Huduma za Hazina, Bw. Nsubili Joshua, (katikati walioketi), Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Wizara ya Fedha, Bi. Fauzia Nombo (kushoto walioketi), Mhadhiri kutoka Chuo Cha Utumishi wa Umma na mwakilishi wa Mkuu wa chuo hicho, Dkt. Mariam Kuhenga (kulia walioketi), wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Ajira Mpya wa Wizara ya Fedha, baada ya kufungua mafunzo hayo yanayofanyika katika Ofisi za Hazina Ndogo mkoani Morogoro. (Picha na Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini, WF - Morogoro).

Na Asia Singano, WF – Morogoro

Watumishi wapya wa Wizara ya Fedha wametakiwa kuzingatia nidhamu, uadilifu na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yao, pamoja na kuimarisha utamaduni wa kufanya kazi kwa kuzingatia matokeo na kuibua mawazo mapya yatakayoboresha utendaji wa Wizara.

Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha anayeshughulikia Huduma za Hazina, Nsubili Joshua, wakati akifungua mafunzo elekezi kwa watumishi wapya wa Wizara hiyo katika Ofisi za Hazina Ndogo mkoani Morogoro.

Joshua aliwataka watumishi hao kutoa huduma kwa wananchi na wadau kwa wakati, kuzingatia taratibu zilizowekwa na kutunza mali za taasisi wanazozitumia ili kusaidia Serikali kufikia malengo yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Alisema kila mtumishi ni mwakilishi wa Wizara na Serikali katika eneo analoishi na kufanyia kazi, hivyo anapaswa kutoa huduma kwa heshima, usawa na weledi, huku akizingatia sheria, miongozo na taratibu zinazomwongoza.

Alieleza kuwa mafanikio ya Wizara ya Fedha na Serikali kwa ujumla yanahitaji ushirikiano wa watumishi na taasisi mbalimbali, hivyo akawataka kutumia mafunzo hayo kupata uelewa utakaoboresha utendaji wao.

Aidha, aliwasisitiza kushirikiana, kuheshimiana na kuwasiliana kwa ufanisi na watumishi wengine ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao.

Aliongeza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kufahamu majukumu na mipaka ya kazi zao, namna ya kushirikiana na watumishi wengine, kutoa huduma bora kwa wadau na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.

Awali, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Wizara ya Fedha, Fauzia Nombo, alisema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea watumishi wapya uwezo wa kiutendaji na kuwapa uelewa wa namna bora ya kutekeleza majukumu yao ndani ya Wizara na Serikali kwa ujumla.

Alisema mafunzo hayo yatawawezesha kutekeleza majukumu ya Wizara kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

Mafunzo hayo yanatolewa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Tawi la Dar es Salaam, yakihusisha watumishi wapya 45 wa Wizara ya Fedha.

Watumishi hao watapatiwa mafunzo kwa siku 10 kuhusu mada 18, zikiwemo muundo wa Serikali na uendeshaji wa shughuli zake, utunzaji wa kumbukumbu, uendeshaji wa ofisi, maadili ya utumishi wa umma na kanuni za utumishi wa umma, pamoja na masuala mengine ya kiutumishi yatakayowaandaa kutekeleza majukumu yao kwa weledi.
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: