Mafinga, Iringa - 25 Novemba 2026: Serikali ya Finland, kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) Tanzania kupitia Programu ya Ubunifu ya FUNGUO, leo imepiga hatua nyingine katika juhudi za kukuza uchumi wa kijani nchini Tanzania kwa kutambulisha rasmi biashara za awamu ya pili ya mradi wa #GreenCatalyst na kuzindua dirisha la tatu la maombi ya ufadhili.
Tukio hilo limefanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Kuchochea Ukuaji, Kuimarisha Biashara na Kupanua Fursa katika Mnyororo wa Thamani wa Misitu,” likisisitiza umuhimu wa uwekezaji katika sekta ya misitu kama nyenzo ya kukuza viwanda, kuongeza ajira na kuboresha maisha ya wananchi, hususan katika maeneo ya vijijini.
Kupitia awamu mbili za kwanza za ufadhili, #GreenCatalyst imetenga takribani shilingi bilioni 1.45 kwa ajili ya kufadhili biashara 19 katika mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma na Lindi. Idadi ya maombi ya ufadhili imeongezeka kutoka 187 katika awamu ya kwanza mpaka 1,178 katika awamu ya pili, hali inayoonesha ukubwa wa fursa za ujasiriamali na ongezeko la mahitaji ya mitaji katika sekta ya misitu.
“Rasilimali za misitu tulizonazo zina fursa kubwa za kukuza viwanda, uwekezaji na ajira. Kwa kuimarisha biashara za ndani na kuongeza thamani ya mazao ya misitu, tunaweza kuhakikisha kuwa sehemu kubwa zaidi ya manufaa ya kiuchumi inabaki katika jamii zetu na kuchangia maendeleo endelevu na ustawi wa wananchi,” amesema Mhe. Atupele Mwakibete, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mufindi.
Uwekezaji huu unalenga kuongeza uwezo wa uzalishaji wa ndani, kuimarisha ubora wa bidhaa, kupunguza upotevu wa rasilimali na kupanua upatikanaji wa masoko. Kupitia ubunifu katika uchakataji wa mbao, matumizi ya mabaki ya mbao, ufugaji nyuki na uzalishaji endelevu wa mazao ya misitu, mradi unalenga kuongeza manufaa ya kiuchumi yanayotokana na rasilimali za misitu, huku ukipanua fursa za ajira na kipato kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
“Ushirikiano wa kimaendeleo kati ya Finland na Tanzania unatambua umuhimu wa sekta endelevu ya misitu katika kuchochea maendeleo ya vijijini. Kupitia #GreenCatalyst, tunaunga mkono uwekezaji unaoleta uwiano kati ya utunzaji wa mazingira na maendeleo ya kiuchumi haswa kwa wajasiriamali wa vijijini wanaojishughulisha na shughuli za mnyororo wa thamani wa misitu ili kuboresha maisha ya wananchi huku tukihakikisha matumizi endelevu ya maliasili,” amesema Sanna-Liisa Taivalmaa, Mkuu wa Ushirikiano wa Kimaendeleo katika Ubalozi wa Finland nchini Tanzania.
Mbali na kutoa ufadhili, mradi unatoa usaidizi wa kitaalamu, unajenga uwezo wa biashara kuvutia uwekezaji na kuziunganisha na masoko ili kuondoa vikwazo vinavyokwamisha ukuaji na ushindani wa biashara za ndani.
“Thamani halisi ya uwekezaji huu haipimwi kwa idadi ya biashara zinazopata ufadhili pekee, bali pia kwa fursa za kiuchumi zinazoweza kutengenezwa kupitia biashara hizo. Kwa kuimarisha biashara, tunaweka msingi wa kuongeza ajira, kukuza uzalishaji wa ndani, kuimarisha minyororo ya thamani na kuvutia uwekezaji zaidi kutoka sekta binafsi,” amesema Joseph Manirakiza, Meneja wa Programu ya FUNGUO.
Uzinduzi wa dirisha la tatu la maombi ya ufadhili unatoa fursa kwa biashara zaidi zenye ubunifu katika mnyororo wa thamani wa misitu kunufaika na ufadhili pamoja na huduma za kuendeleza biashara katika mikoa minne inayolengwa na mradi. Kupata taarifa zaidi kuhusu maombi tembelea www.funguo.org














Toa Maoni Yako:
0 comments: