Articles by "HABARI"
Showing posts with label HABARI. Show all posts


Mafinga, Iringa - 25 Novemba 2026: Serikali ya Finland, kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) Tanzania kupitia Programu ya Ubunifu ya FUNGUO, leo imepiga hatua nyingine katika juhudi za kukuza uchumi wa kijani nchini Tanzania kwa kutambulisha rasmi biashara za awamu ya pili ya mradi wa #GreenCatalyst na kuzindua dirisha la tatu la maombi ya ufadhili.

Tukio hilo limefanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Kuchochea Ukuaji, Kuimarisha Biashara na Kupanua Fursa katika Mnyororo wa Thamani wa Misitu,” likisisitiza umuhimu wa uwekezaji katika sekta ya misitu kama nyenzo ya kukuza viwanda, kuongeza ajira na kuboresha maisha ya wananchi, hususan katika maeneo ya vijijini.

Kupitia awamu mbili za kwanza za ufadhili, #GreenCatalyst imetenga takribani shilingi bilioni 1.45 kwa ajili ya kufadhili biashara 19 katika mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma na Lindi. Idadi ya maombi ya ufadhili imeongezeka kutoka 187 katika awamu ya kwanza mpaka 1,178 katika awamu ya pili, hali inayoonesha ukubwa wa fursa za ujasiriamali na ongezeko la mahitaji ya mitaji katika sekta ya misitu.

“Rasilimali za misitu tulizonazo zina fursa kubwa za kukuza viwanda, uwekezaji na ajira. Kwa kuimarisha biashara za ndani na kuongeza thamani ya mazao ya misitu, tunaweza kuhakikisha kuwa sehemu kubwa zaidi ya manufaa ya kiuchumi inabaki katika jamii zetu na kuchangia maendeleo endelevu na ustawi wa wananchi,” amesema Mhe. Atupele Mwakibete, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mufindi.

Uwekezaji huu unalenga kuongeza uwezo wa uzalishaji wa ndani, kuimarisha ubora wa bidhaa, kupunguza upotevu wa rasilimali na kupanua upatikanaji wa masoko. Kupitia ubunifu katika uchakataji wa mbao, matumizi ya mabaki ya mbao, ufugaji nyuki na uzalishaji endelevu wa mazao ya misitu, mradi unalenga kuongeza manufaa ya kiuchumi yanayotokana na rasilimali za misitu, huku ukipanua fursa za ajira na kipato kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

“Ushirikiano wa kimaendeleo kati ya Finland na Tanzania unatambua umuhimu wa sekta endelevu ya misitu katika kuchochea maendeleo ya vijijini. Kupitia #GreenCatalyst, tunaunga mkono uwekezaji unaoleta uwiano kati ya utunzaji wa mazingira na maendeleo ya kiuchumi haswa kwa wajasiriamali wa vijijini wanaojishughulisha na shughuli za mnyororo wa thamani wa misitu ili kuboresha maisha ya wananchi huku tukihakikisha matumizi endelevu ya maliasili,” amesema Sanna-Liisa Taivalmaa, Mkuu wa Ushirikiano wa Kimaendeleo katika Ubalozi wa Finland nchini Tanzania.
Mbali na kutoa ufadhili, mradi unatoa usaidizi wa kitaalamu, unajenga uwezo wa biashara kuvutia uwekezaji na kuziunganisha na masoko ili kuondoa vikwazo vinavyokwamisha ukuaji na ushindani wa biashara za ndani.

“Thamani halisi ya uwekezaji huu haipimwi kwa idadi ya biashara zinazopata ufadhili pekee, bali pia kwa fursa za kiuchumi zinazoweza kutengenezwa kupitia biashara hizo. Kwa kuimarisha biashara, tunaweka msingi wa kuongeza ajira, kukuza uzalishaji wa ndani, kuimarisha minyororo ya thamani na kuvutia uwekezaji zaidi kutoka sekta binafsi,” amesema Joseph Manirakiza, Meneja wa Programu ya FUNGUO.

Uzinduzi wa dirisha la tatu la maombi ya ufadhili unatoa fursa kwa biashara zaidi zenye ubunifu katika mnyororo wa thamani wa misitu kunufaika na ufadhili pamoja na huduma za kuendeleza biashara katika mikoa minne inayolengwa na mradi. Kupata taarifa zaidi kuhusu maombi tembelea www.funguo.org

Meneja Mwandamizi wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania, Kauthar D’souza, akizungumza na washiriki wa programu ya Women Empowerment Programme (WEP), wakati wa ufunguzi wa awamu mpya ya mafunzo ya wiki sita yanayoendeshwa na Benki ya Exim Tanzania. Katika awamu hii, wanawake 50 wanaomiliki na kusimamia biashara ndogo na za kati wanapatiwa mafunzo ya usimamizi wa biashara na fedha, upangaji wa bajeti na kukuza masoko, pamoja na ushauri elekezi na fursa za kujenga mitandao ya kibiashara. Kupitia programu hii iliyo chini ya mpango wa Exim Cares, Benki inalenga kuwawezesha wanawake kuimarisha biashara zao, kuongeza ushindani na kutumia fursa mpya za ukuaji.

Na Mwandishi Wetu.

Dar es Salaam: Kuanzisha biashara ni hatua muhimu, lakini kuijenga na kuhakikisha inaendelea kwa mafanikio kunahitaji zaidi ya mtaji. Kwa wanawake wengi wajasiriamali, changamoto za kusimamia fedha, kutunza kumbukumbu za biashara, kudhibiti gharama, kupata masoko na kufanya maamuzi ya kimkakati zinaweza kuathiri ukuaji wa biashara zao. Kukabiliana na changamoto hizo kunahitaji elimu ya vitendo kuhusu biashara pamoja na kuwajengea wanawake uwezo wa kutambua na kutumia fursa mbalimbali za kukuza shughuli zao za ujasiriamali.

Kwa kuendeleza juhudi zake za kuwawezesha wanawake kiuchumi, Benki ya Exim Tanzania imezindua awamu nyingine ya mafunzo kupitia programu yake ya Women Empowerment Programme (WEP), itakayowanufaisha wanawake wajasiriamali wengine 50 wanaomiliki au kusimamia biashara ndogo na za kati. 

Tangu kuanzishwa kwake, programu ya WEP imeendelea kupanuka kwa kuwafikia wanawake wengi zaidi na kuongeza wigo wa mafunzo yake. Mwaka 2024, programu hiyo ilipanuliwa hadi mkoani Arusha, huku mwaka 2025 maudhui ya mafunzo yakiboreshwa na kujumuisha masuala ya uongozi, uimara wa kihisia na ujenzi wa mitandao ya kimkakati ya kibiashara. Kufikia mwaka huo, programu ilikuwa imenufaisha zaidi ya wanawake wajasiriamali 300, ikiakisi dhamira ya Benki ya Exim ya kuendeleza fursa za kiuchumi zenye manufaa na endelevu kwa wanawake.

Mwaka 2026, Benki ya Exim Tanzania iliimarisha zaidi programu hiyo kupitia ushirikiano na Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), hatua iliyolenga kuboresha utekelezaji wake na kupanua fursa za washiriki kupata mitandao ya biashara na fursa za ukuaji. Baada ya kundi la kwanza la wanawake 50 kuhitimu mafunzo hayo Septemba mwaka huu, benki imeendeleza fursa hizo kwa kundi jingine la washiriki.
Mafunzo hayo ya wiki sita yameandaliwa kuwapatia washiriki maarifa, nyenzo na ujuzi wa vitendo utakaowawezesha kuimarisha uwezo wao katika usimamizi wa fedha na biashara, kuboresha ufanisi wa shughuli za kibiashara na kufanya maamuzi sahihi yanayochochea ukuaji endelevu wa biashara zao.

Mafunzo hayo yanajumuisha maeneo muhimu ya uendeshaji wa biashara, yakiwemo usimamizi wa mapato na matumizi, utunzaji sahihi wa kumbukumbu za fedha, uandaaji wa bajeti, udhibiti wa gharama za uendeshaji na upangaji wa bei zinazofaa. Washiriki pia wanajifunza namna ya kutambua fursa za masoko na kuweka mikakati ya kuwafikia wateja wengi zaidi. Ujuzi huo unatarajiwa kuwasaidia kusimamia rasilimali zao kwa ufanisi, kufanya maamuzi sahihi ya kibiashara, kuongeza mapato na kutambua fursa zaidi za kukuza biashara zao.

Mbali na mafunzo ya darasani, washiriki watanufaika na ushauri elekezi pamoja na fursa za kujenga mitandao ya kibiashara. Kupitia fursa hizo, wataweza kubadilishana uzoefu, kupata mitazamo mipya na kujifunza mbinu za vitendo za kukabiliana na changamoto za biashara na kuimarisha shughuli zao.
Meneja Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania, Kauthar D’souza, akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa mafunzo hayo, alisema kuwa kuwawezesha wanawake wajasiriamali kunahitaji kuwapatia maarifa na ujuzi wa vitendo utakaowawezesha kusimamia biashara zao kwa ufanisi na kutumia fursa zilizopo kukuza shughuli zao.

Aliongeza kuwa kupitia WEP, benki inalenga kuimarisha uwezo wa wanawake katika ujasiriamali kwa kuwapatia nyenzo na msaada unaohitajika ili kukabiliana na changamoto za usimamizi wa biashara na kujenga biashara zenye ushindani na zinazoweza kudumu.

Julieth Micky Msofe, mmiliki wa Dream Designs, biashara inayojihusisha na ubunifu na utengenezaji wa mavazi ya wanawake, alisema mafunzo hayo yanampa fursa ya kuongeza maarifa yatakayomsaidia kuendesha biashara yake kwa ufanisi zaidi, kuboresha mipango ya biashara na kutambua fursa zaidi za ukuaji. Aliongeza kuwa ujuzi wa kusimamia fedha, kudhibiti gharama za uendeshaji na kupata masoko ni muhimu katika kuimarisha ushindani na kuhakikisha biashara yake inakua na kudumu.

Kwa upande wake, Irene Modesta Kambewe, mmiliki wa MIMII Quality Products, alisema mafunzo hayo yatamsaidia kuongeza uelewa wa masuala mbalimbali ya uendeshaji wa biashara, yakiwemo usimamizi wa fedha, utunzaji wa kumbukumbu na kuandaa mikakati ya kukuza biashara. Aliongeza kuwa maarifa atakayopata yatakuwa muhimu katika kuimarisha shughuli zake za kibiashara na kutumia fursa mpya zitakazojitokeza. 

Kupitia WEP, Benki ya Exim inaendelea kuonesha dhamira yake ya kwenda zaidi ya utoaji wa huduma za kawaida za kibenki kwa kuwekeza katika maarifa na uwezo wa wanawake wajasiriamali. Dhamira hiyo inalenga kuwawezesha kujenga biashara imara zinazoweza kuhimili changamoto, kuzalisha ajira na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Tanzania.


Mshauri wa Rais wa Masuala ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Ummy Mwalimu, ametoa wito kwa vijana na wanawake kushirikishwa kikamilifu katika maamuzi na mipango ya kuboresha huduma za afya badala ya kuishia kuwasikiliza na kuwapa ahadi.

Akizungumza Novemba 22, 2026, katika Mkutano wa Afya na Uzazi kwa Vijana jijini Addis Ababa, Ethiopia, Ummy amesema Serikali na wadau wanapaswa kuelekeza nguvu katika kugharamia na kuhakikisha huduma za afya zinawafikia vijana, wanawake na watoto.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais Mstaafu wa Uganda, Dkt. Speciosa Wandira Kazibwe, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha kinga na kushughulikia sababu za msingi za magonjwa ili kupunguza magonjwa na vifo vinavyoweza kuzuilika.

Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC), Dkt. Ntuli Kapologwe, pamoja na Josephat Rafael na Rahma Suleiman Jumanne, ni miongoni mwa washiriki kutoka Tanzania waliopongeza jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, katika kuendeleza ajenda hiyo barani Afrika.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwasili katika Kituo cha Mikutano cha African International Convention Centre (AICC), Addis Ababa, Ethiopia kwa ajili ya kushiriki kwenye Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026) pamoja na kuzindua Mpango Elekezi wa Kuboresha Afya ya Mama na Mtoto Barani Afrika, tarehe 23 Novemba, 2026.






Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole, Addis Ababa nchini Ethiopia tarehe 22 Novemba, 2026 kwa Ziara ya Kikazi ya siku mbili. akiwa Addis Ababa, Mhe. Rais Dkt. Samia atashiriki Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026), pamoja na kuzindua Mpango Elekezi wa Kuboresha Afya ya Mama na Mtoto Barani Afrika.


Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akizungumza na Waziri wa Ubunifu na Teknolojia wa Ethiopia Mhe.Frehiwot Tamiru baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole, Addis Ababa nchini Ethiopia tarehe 22 Novemba, 2026 kwa Ziara ya Kikazi ya siku mbili. akiwa Addis Ababa, Mhe. Rais Dkt. Samia atashiriki Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026), pamoja na kuzindua Mpango Elekezi wa Kuboresha Afya ya Mama na Mtoto Barani Afrika.




Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwa na Watoto wa Kitanzania wanaoishi nchini Ethiopia waliojitokeza kumlaki baada ya kuwasili nchini humo tarehe 22 Novemba, 2026 kwa Ziara ya Kikazi ya siku mbili. Akiwa Addis Ababa, Mhe. Rais Dkt. Samia atashiriki Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026), pamoja na kuzindua Mpango Elekezi wa Kuboresha Afya ya Mama na Mtoto Barani Afrika.





Dar es Salaam, 14 Novemba 2026: Benki ya Exim Tanzania imetumia tamasha la Twende BBM Festival 2026 kuwasogezea madereva wa bodaboda, bajaji na magari huduma za kifedha zinazolenga kurahisisha shughuli zao za kila siku na kulinda vyanzo vyao vya kipato, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uhusiano na wadau wa sekta ya usafiri nchini. 

Ikiwa mdhamini wa tamasha hilo, Exim Bank ilitumia fursa hiyo kuwafikia madereva wanaohusishwa na jukwaa la Twende. Jukwaa la Twende linahusisha madereva takribani 12,000 na jumuiya pana ya zaidi ya watumiaji 46,000 wa huduma zake. Kupitia tamasha hilo, Benki ya Exim ilipata fursa ya kukutana na kuwafahamisha madereva kuhusu huduma za kifedha zinazoweza kuwasaidia katika shughuli zao za kila siku. 
Katika tamasha hilo, Benki ya Exim iliendeleza ujumbe wa kampeni “Exim Inalinda Hustle Yako” kwa kutambulisha huduma nne zinazolenga mahitaji ya madereva katika shughuli zao za kila siku. Huduma hizo ni Exim Lipa ChapChap, Tumaini Health Insurance, Motor Insurance na Exim Quick Account. Kwa pamoja, huduma hizi zinalenga kurahisisha upatikanaji wa malipo, kuwawezesha madereva kupata ulinzi wa afya na kulinda vyombo vya usafiri wanavyotegemea kujipatia kipato.

Akizungumza wakati wa tamasha hilo, Andrew Lyimo, Mkuu wa Kitengo cha Wateje Binafsi na Wakati wa Benki ya Exim Tanzania alisema benki inatambua mchango wa madereva katika kurahisisha usafiri na shughuli za kiuchumi, hivyo inaendelea kuwasogezea huduma zinazowasaidia kusimamia shughuli zao na kulinda vipato vyao. 
“Kwa madereva wengi, bodaboda, bajaji na magari si vyombo vya usafiri pekee, bali ni nyenzo muhimu za kujipatia kipato na kutunza familia zao. Tunatambua changamoto na mahitaji yanayoambatana na kazi zao za kila siku. Ndiyo maana kupitia huduma zetu, tunalenga kurahisisha upatikanaji wa malipo, kuwapatia fursa ya kupata ulinzi wa afya na vyombo vyao vya usafiri, pamoja na huduma za kibenki zinazowawezesha kusimamia fedha zao kwa urahisi zaidi. Hii ndiyo maana halisi ya ujumbe wetu, Exim Inalinda Hustle Yako,” alisema Lyimo. 

Kupitia Exim Lipa ChapChap, madereva wanaweza kurahisisha upokeaji na ufanyaji wa malipo. Tumaini Health Insurance inawawezesha kupata ulinzi wa bima ya afya, huku Motor Insurance ikitoa ulinzi wa bima kwa vyombo vya usafiri wanavyotumia katika shughuli zao za kila siku. Kw aupande wa Exim Quick Account, inawapa fursa ya kufungua akaunti na kutumia huduma za kibenki za Exim.  
Mmoja wa madereva walioshiriki tamasha hilo, alisema ushiriki wa Exim Bank umewapa madereva fursa ya kufahamu huduma za kifedha zinazoweza kuwasaidia katika kusimamia na kulinda shughuli zao za kila siku. 

“Ni jambo zuri kuona taasisi za kifedha zikija karibu nasi na kutuletea huduma zinazozingatia mahitaji yetu. Kazi yetu ya kila siku inategemea vyombo vyetu vya usafiri na uwezo wetu wa kuendelea kufanya kazi ili kupata kipato. Kwa hiyo, kufahamu huduma za malipo na bima zinazoweza kutusaidia kulinda kazi zetu ni jambo lenye umuhimu mkubwa kwetu,” alisema. 

Kupitia ushiriki wake katika Twende BBM Festival 2026, Exim Bank imelenga kuongeza idadi ya watumiaji wa Exim Lipa ChapChap, kuwafikia wateja wapya wa Tumaini Health Insurance na Motor Insurance, pamoja na kuongeza idadi ya akaunti za Exim Quick Account zinazofunguliwa. Benki pia inalenga kujenga mahusiano ya muda mrefu na madereva, vikundi vyao na wadau wengine wa sekta ya usafiri kwa ajili ya fursa za ushirikiano wa baadaye. 

Benki ya Exim inawaalika madereva, abiria na wadau wengine wa sekta ya usafiri kutembelea matawi yake nchini kote ili kupata maelezo zaidi kuhusu huduma hizo, kujisajili na kufungua akaunti. Kupitia huduma hizo, benki inalenga kuwasaidia wateja kurahisisha miamala yao, kupata ulinzi wa bima ya afya na vyombo vya usafiri, pamoja na kusimamia fedha zao kwa urahisi.

Afisa wa Huduma Mpya za Kifedha wa Vodacom M-Pesa, Sylivester Lukeka(kulia), akielekeza wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati wa hafla ya UDSM Freshers Connect iliyofanyika chuoni hapo, Novemba 20, 2026. Kupitia hafla hiyo, Vodacom Tanzania iliwahamasisha wanafunzi wapya kutumia teknolojia na huduma za kidijitali kama nyenzo muhimu za kujenga ujuzi, kujiongezea kipato na kujiandaa kwa fursa za ajira na ujasiriamali. Aidha, kampuni hiyo iliwatambulisha wanafunzi kwenye mpango wa TECHSTART, unaowawezesha kupata mafunzo mbalimbali ya Microsoft bila malipo ili kuwajengea ujuzi wa kidijitali. Sambamba na hilo, wanafunzi walielimishwa kuhusu huduma ya M-Wekeza ya Vodacom M-Pesa, inayowapa fursa ya kuanza kuwekeza na kujenga utamaduni wa kuweka akiba kwa ajili ya maisha yao ya baadaye. Hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya Vodacom Tanzania ya kuwawezesha vijana kushiriki na kunufaika na fursa zinazotokana na ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.

Afisa wa Huduma Mpya za Kifedha wa Vodacom M-Pesa, Sylivester Lukeka (kushoto), akisikiliza swali kutoka kwa mmoja wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati wa majadiliano yaliyofanyika katika hafla ya UDSM Freshers Connect, Novemba 20, 2026. Kupitia mazungumzo hayo, wanafunzi walipata ufafanuzi kuhusu huduma ya M-Wekeza na fursa za kujenga ujuzi wa kidijitali kupitia mpango wa TECHSTART, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Vodacom Tanzania za kuwaandaa vijana kutumia fursa za ajira, ujasiriamali na uchumi wa kidijitali.

Mkuu wa Idara ya Bei za Bidhaa na Makundi Maalumu ya Wateja wa Vodacom Tanzania, Gemma Vedasto Kamara (kulia), pamoja na Afisa wa Huduma Mpya za Kifedha wa Vodacom M-Pesa, Sylivester Lukeka (kushoto), wakimkabidhi zawadi mmoja wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (katikati), wakati wa hafla ya UDSM Freshers Connect iliyofanyika chuoni hapo Novemba 20, 2026.

Kampuni hiyo pia iliwatambulisha wanafunzi kwenye mpango wa TECHSTART, unaowawezesha kupata mafunzo ya Microsoft bila malipo, pamoja na huduma ya M-Wekeza inayowapa fursa ya kuanza safari ya uwekezaji na kujenga utamaduni wa kuweka akiba kwa ajili ya maisha yao ya baadayea kupata mafunzo ya Microsoft bila malipo, pamoja na huduma ya M-Wekeza inayowapa fursa ya kuanza safari ya uwekezaji na kujenga utamaduni wa kuweka akiba kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.

Mkuu wa Idara ya Bei za Bidhaa na Makundi Maalumu ya Wateja wa Vodacom Tanzania, Gemma Vedasto Kamara akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati wa hafla ya UDSM Freshers Connect iliyofanyika Novemba 20, 2026. Kupitia hafla hiyo, Vodacom Tanzania iliwahamasisha wanafunzi wapya kutumia teknolojia na huduma za kifedha za kidijitali kujenga ujuzi, kujiongezea kipato na kujiandaa kwa fursa za kiuchumi. Kampuni hiyo pia iliwatambulisha wanafunzi kwenye mpango wa TECHSTART, unaowawezesha kupata mafunzo ya Microsoft bila malipo, pamoja na huduma ya M-Wekeza inayowapa fursa ya kuanza safari ya uwekezaji na kujenga utamaduni wa kuweka akiba kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.
kuwekeza kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.

Wafanyakazi wa Vodacom Tanzania wakiwahudumia wanafunzi katika banda la kampuni hiyo wakati wa hafla ya UDSM Freshers Connect iliyofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Novemba 20, 2026. Kupitia hafla hiyo, Vodacom Tanzania ilitoa elimu kuhusu matumizi ya huduma zake za mawasiliano na fedha kwa njia ya kidijitali, ikiwahamasisha vijana kutumia teknolojia kurahisisha shughuli zao za kila siku, kujenga tabia ya kuweka akiba na kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi.

Mkuu wa Idara ya Bei za Bidhaa na Makundi Maalumu ya Wateja wa Vodacom Tanzania, Gemma Vedasto Kamara (wa tano kutoka kushoto), akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waliokamilisha mafunzo ya muda mfupi kupitia mpango wa TECHSTART, wakati wa hafla ya UDSM Freshers Connect iliyofanyika chuoni hapo, Novemba 20, 2026. Wanafunzi hao walionesha vyeti vyao kwa kutumia simu zao kama ishara ya mafanikio baada ya kukamilisha mafunzo hayo, yanayolenga kuwajengea ujuzi wa kidijitali kupitia kozi fupi za Microsoft. Kupitia hafla hiyo, Vodacom Tanzania iliendelea kuonesha dhamira yake ya kuwawezesha vijana kwa kuwapatia fursa za kujifunza, huku pia ikiwahamasisha kutumia huduma ya M-Wekeza kujenga utamaduni wa kuweka akiba na kuwekeza kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.

 


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, akipokea mkoba wenye machapisho na taarifa mbalimbali kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kutoka kwa Afisa Uhusiano Mkuu wa Mfuko huo, Bi. Queen Edward, alipotembelea banda la PSSSF katika Kongamano na Maonesho ya Sekta ya Majengo na Uwekezaji wa Ardhi (Tanzania Real Estate Expo and Forum – TAREX 2026), katika Ukumbi wa Superdome, Masaki, jijini Dar es Salaam, Novemba 20, 2026.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, akipokea mkoba wenye machapisho na taarifa mbalimbali kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kutoka kwa Afisa Uhusiano Mkuu wa Mfuko huo, Bi. Queen Edward, alipotembelea banda la PSSSF katika Kongamano na Maonesho ya Sekta ya Majengo na Uwekezaji wa Ardhi (Tanzania Real Estate Expo and Forum – TAREX 2026), katika Ukumbi wa Superdome, Masaki, jijini Dar es Salaam, Novemba 20, 2026.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, ameipongeza na kuitambua kazi nzuri inayofanywa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), katika kusimamia shughuli zake na kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Pongezi hizo amezitoa leo Novemba 20, 2026, alipotembelea banda la PSSSF katika Kongamano na Maonesho ya Sekta ya Majengo na Uwekezaji wa Ardhi (Tanzania Real Estate Expo and Forum – TAREX 2026), yanayofanyika kwa siku tatu jijini Dar es Salaam, ambapo alikuwa mgeni rasmi.

Akizungumza wakati akiwa katika banda hilo, Mhe. Dkt. Nchemba aliipongeza PSSSF kwa kazi nzuri inayofanya na kuhimiza kuendelea na juhudi hizo.

“Hongereni sana, natambua kazi nzuri mnayofanya. Endeleeni hivyo hivyo,” alisema Mhe. Waziri Mkuu.

Kwa mujibu wa Afisa Mwandamizi toka Idara ya Uwekezaji, Milki na Usimamizi wa Majengo wa PSSSF, Bw. Arnold Kagaruki, ushiriki wa PSSSF katika kongamano na maonesho hayo unatokana na nafasi yake kama mdau muhimu katika sekta ya majengo na uwekezaji wa ardhi, kupitia uwekezaji wake katika miradi mbalimbali ya majengo na ardhi nchini.

“ Kuna uwekezaji unaowagusa moja kwa moja wanachama na wananchi kama vile majengo ya kibiashara, nyumba na viwanja; lakini pia Mfuko umewekeza kimkakati ambapo kwa kushirikiana na Kituo cha Mikutano cha Kimataifa AICC, PSSSF imewekeza katika ujenzi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mount Kilimanjaro International Convention Centre Jijini Arusha ambapo ujenzi umeanza” alisema.

Kongamano na maonesho hayo yanawakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya majengo na uwekezaji wa ardhi, wakiwemo waendelezaji wa miradi ya majengo, wawekezaji, taasisi za kifedha, mamlaka za udhibiti pamoja na watoa huduma za kitaalamu kutoka Tanzania Bara, Zanzibar na Kenya.

Kupitia jukwaa hilo, PSSSF inalenga kuonesha mchango wake katika maendeleo ya sekta ya majengo na uwekezaji wa ardhi, kutangaza fursa zinazotokana na uwekezaji wake, kuimarisha mahusiano na wadau mbalimbali, pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu shughuli na huduma zinazotolewa na Mfuko, Alisema Bw. Kagaruki.