Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah (katikati), akikata utepe kuzindua rasmi mgahawa wa Hungry Lion katika kituo cha Puma Energy Oysterbay, jijini Dar es Salaam, Novemba 13, 2026. Ushirikiano huo unaimarisha nafasi ya Puma Energy kama kampuni inayotoa huduma zaidi ya mafuta, huku ukiboresha uzoefu wa wateja, kuvutia uwekezaji na kuongeza fursa za ajira nchini. Wanaoshuhudia uzinduzi huo ni pamoja na Mkuu wa Hungry Lion Tanzania, Gladstone Okumu (wa pili kulia), Katibu wa Pili wa Masuala ya Siasa katika Ubalozi wa Afrika Kusini, Ndumiso Mngadi (wa kwanza kulia), pamoja na viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo.
●Ushirikiano huo unawawezesha wateja wa kituo cha Puma Energy Oysterbay kupata huduma za chakula kwa haraka na kwa urahisi, huku ukitoa fursa mpya za ajira na kuboresha huduma kwa wateja.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Kampuni ya Puma Energy Tanzania imezindua rasmi mgahawa wa Hungry Lion katika kituo chake cha Oysterbay, jijini Dar es Salaam, hatua inayowezesha kampuni hiyo ya chakula kuingia katika soko la Tanzania na kupanua shughuli zake katika Afrika Mashariki.
Uzinduzi huo uliofanyika Novemba 13, 2026, unaifanya Tanzania kuwa nchi ya nne ambayo Hungry Lion inafanya kazi kwa kushirikiana na Puma Energy, baada ya Namibia, Zambia na Botswana.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah, alisema ushirikiano huo ni sehemu ya mkakati wa kampuni kuboresha vituo vyake kwa kuongeza huduma zinazokidhi mahitaji mbalimbali ya wateja.
Alisema licha ya biashara kuu ya kampuni kuwa usambazaji wa mafuta, inaendelea kuwekeza katika huduma nyingine zinazorahisisha maisha ya wateja, zikiwemo huduma za chakula, maduka, ATM na mawakala wa huduma za kifedha.
“Mkakati wetu ni kuboresha vituo vyetu ili wateja waweze kupata huduma mbalimbali wanazohitaji katika eneo moja. Wanaweza kujaza mafuta, kununua vilainishi vya magari, kufanya manunuzi katika maduka yetu ya Shop Express, kupata huduma za kifedha na sasa pia kupata chakula kupitia Hungry Lion,” alisema.
Fatma alisema kampuni itaendelea kupanua na kuboresha mtandao wake wa vituo vya huduma, ambao kwa sasa una zaidi ya vituo 105 nchini.
Aliongeza kuwa Puma Energy inaendelea kuwekeza katika suluhisho za nishati mbadala, zikiwemo Gesi Asilia Iliyoshindiliwa (CNG) na Gesi ya Petroli Iliyoyeyushwa (LPG), pamoja na huduma za kidijitali kupitia programu ya Puma PRIS inayowazawadia wateja.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hungry Lion, Adrian Basson, alisema upanuzi wa biashara hiyo katika masoko mbalimbali ya Afrika unalenga pia kuongeza ajira, kukuza vipaji vya ndani na kuchangia maendeleo ya jamii.
Alisema kila mgahawa mpya unaofunguliwa unatoa fursa za ajira na kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo husika.
“Tanzania ni soko lenye fursa nzuri kwetu na tunafurahi kuanza safari yetu katika Afrika Mashariki kupitia nchi hii. Ushirikiano wetu na Puma Energy unatupa nafasi nzuri ya kukuza biashara yetu, na tunatarajia kuwa sehemu ya maendeleo ya uchumi wa Tanzania,” alisema.
Basson aliongeza kuwa Hungry Lion inatarajia kupanua shughuli zake katika nchi nyingine za Afrika, zikiwemo Zimbabwe na Eswatini mwaka 2027.
Uzinduzi wa mgahawa huo umefanyika baada ya Puma Energy kufanya maboresho katika kituo chake cha Oysterbay ili kukidhi mahitaji ya uendeshaji wa huduma hizo mpya.
Ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza wigo wa huduma kwa wateja wanaotembelea kituo hicho, huku ukichochea uwekezaji na kutoa fursa zaidi za ajira kupitia shughuli za maandalizi na uendeshaji wa mgahawa.







Toa Maoni Yako:
0 comments: