Articles by "HABARI ZA KIJAMII"
Showing posts with label HABARI ZA KIJAMII. Show all posts
Na Mwandishi Wetu.

Mwandishi wa vitabu na mtaalamu wa rasilimali watu, Damas Raphael Ndalechi, anatarajia kuzindua vitabu vitatu vinavyolenga kuwajengea vijana uelewa kuhusu kujitambua, fursa za ajira, biashara na ujasiriamali.

Uzinduzi wa vitabu hivyo umepangwa kufanyika Ijumaa, Novemba 27, 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kutoa maarifa na mwongozo kwa vijana kuhusu namna ya kujiandaa kukabiliana na changamoto za maisha na kutumia fursa zilizopo kujiletea maendeleo.

Vitabu hivyo vinagusia masuala mbalimbali, yakiwemo maandalizi ya kukua kitaaluma na kupanda vyeo katika maeneo ya kazi, kuanzisha na kukuza biashara, pamoja na matumizi ya mitandao ya kijamii kupata elimu, ajira na fursa za kibiashara.
Akizungumzia maandalizi ya uzinduzi huo, Ndalechi alisema amelenga kuwafikia vijana, wazazi, walezi, walimu na viongozi ili vitabu hivyo viweze kutumika kama nyenzo ya kuongeza maarifa na kuwasaidia vijana kupanga maisha yao ya baadaye.

Alisema vitabu hivyo vinapatikana kwa Sh 10,000 kila kimoja, huku akiwahimiza wazazi na walezi kujipatia nakala kwa ajili yao na vijana wanaowalea.

Malipo yanaweza kufanyika kupitia akaunti ya CRDB namba 0150522731600, yenye jina la Gillian Business Consult Services, au Selcom Pesa kupitia namba 0769651515, kwa jina la Damas Ndalechi.

Kuhusu taaluma yake, Ndalechi alisema ana shahada ya Biashara na Usimamizi (Bachelor of Commerce and Management) pamoja na shahada ya uzamili ya Usimamizi wa Rasilimali Watu (Master of Human Resources Management).

Ameeleza kuwa ana uzoefu wa zaidi ya miaka 15 katika masuala ya kazi, ajira, mafunzo na ushauri, jambo linalompa msingi wa kushughulikia mada zinazohusu maendeleo ya vijana na ukuaji wa taaluma na biashara.

Vitabu hivyo vinatarajiwa kuwa nyenzo ya kuwasaidia vijana kuongeza uelewa, kutambua uwezo wao na kutumia maarifa pamoja na teknolojia zilizopo kutafuta fursa za kujiajiri na kuajiriwa. Kwa Mawasiliano zaidi WhatsApp (only) +255717034423.


Mshauri wa Rais wa Masuala ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Ummy Mwalimu, ametoa wito kwa vijana na wanawake kushirikishwa kikamilifu katika maamuzi na mipango ya kuboresha huduma za afya badala ya kuishia kuwasikiliza na kuwapa ahadi.

Akizungumza Novemba 22, 2026, katika Mkutano wa Afya na Uzazi kwa Vijana jijini Addis Ababa, Ethiopia, Ummy amesema Serikali na wadau wanapaswa kuelekeza nguvu katika kugharamia na kuhakikisha huduma za afya zinawafikia vijana, wanawake na watoto.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais Mstaafu wa Uganda, Dkt. Speciosa Wandira Kazibwe, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha kinga na kushughulikia sababu za msingi za magonjwa ili kupunguza magonjwa na vifo vinavyoweza kuzuilika.

Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC), Dkt. Ntuli Kapologwe, pamoja na Josephat Rafael na Rahma Suleiman Jumanne, ni miongoni mwa washiriki kutoka Tanzania waliopongeza jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, katika kuendeleza ajenda hiyo barani Afrika.


Afisa wa Huduma Mpya za Kifedha wa Vodacom M-Pesa, Sylivester Lukeka(kulia), akielekeza wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati wa hafla ya UDSM Freshers Connect iliyofanyika chuoni hapo, Novemba 20, 2026. Kupitia hafla hiyo, Vodacom Tanzania iliwahamasisha wanafunzi wapya kutumia teknolojia na huduma za kidijitali kama nyenzo muhimu za kujenga ujuzi, kujiongezea kipato na kujiandaa kwa fursa za ajira na ujasiriamali. Aidha, kampuni hiyo iliwatambulisha wanafunzi kwenye mpango wa TECHSTART, unaowawezesha kupata mafunzo mbalimbali ya Microsoft bila malipo ili kuwajengea ujuzi wa kidijitali. Sambamba na hilo, wanafunzi walielimishwa kuhusu huduma ya M-Wekeza ya Vodacom M-Pesa, inayowapa fursa ya kuanza kuwekeza na kujenga utamaduni wa kuweka akiba kwa ajili ya maisha yao ya baadaye. Hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya Vodacom Tanzania ya kuwawezesha vijana kushiriki na kunufaika na fursa zinazotokana na ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.

Afisa wa Huduma Mpya za Kifedha wa Vodacom M-Pesa, Sylivester Lukeka (kushoto), akisikiliza swali kutoka kwa mmoja wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati wa majadiliano yaliyofanyika katika hafla ya UDSM Freshers Connect, Novemba 20, 2026. Kupitia mazungumzo hayo, wanafunzi walipata ufafanuzi kuhusu huduma ya M-Wekeza na fursa za kujenga ujuzi wa kidijitali kupitia mpango wa TECHSTART, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Vodacom Tanzania za kuwaandaa vijana kutumia fursa za ajira, ujasiriamali na uchumi wa kidijitali.

Mkuu wa Idara ya Bei za Bidhaa na Makundi Maalumu ya Wateja wa Vodacom Tanzania, Gemma Vedasto Kamara (kulia), pamoja na Afisa wa Huduma Mpya za Kifedha wa Vodacom M-Pesa, Sylivester Lukeka (kushoto), wakimkabidhi zawadi mmoja wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (katikati), wakati wa hafla ya UDSM Freshers Connect iliyofanyika chuoni hapo Novemba 20, 2026.

Kampuni hiyo pia iliwatambulisha wanafunzi kwenye mpango wa TECHSTART, unaowawezesha kupata mafunzo ya Microsoft bila malipo, pamoja na huduma ya M-Wekeza inayowapa fursa ya kuanza safari ya uwekezaji na kujenga utamaduni wa kuweka akiba kwa ajili ya maisha yao ya baadayea kupata mafunzo ya Microsoft bila malipo, pamoja na huduma ya M-Wekeza inayowapa fursa ya kuanza safari ya uwekezaji na kujenga utamaduni wa kuweka akiba kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.

Mkuu wa Idara ya Bei za Bidhaa na Makundi Maalumu ya Wateja wa Vodacom Tanzania, Gemma Vedasto Kamara akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati wa hafla ya UDSM Freshers Connect iliyofanyika Novemba 20, 2026. Kupitia hafla hiyo, Vodacom Tanzania iliwahamasisha wanafunzi wapya kutumia teknolojia na huduma za kifedha za kidijitali kujenga ujuzi, kujiongezea kipato na kujiandaa kwa fursa za kiuchumi. Kampuni hiyo pia iliwatambulisha wanafunzi kwenye mpango wa TECHSTART, unaowawezesha kupata mafunzo ya Microsoft bila malipo, pamoja na huduma ya M-Wekeza inayowapa fursa ya kuanza safari ya uwekezaji na kujenga utamaduni wa kuweka akiba kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.
kuwekeza kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.

Wafanyakazi wa Vodacom Tanzania wakiwahudumia wanafunzi katika banda la kampuni hiyo wakati wa hafla ya UDSM Freshers Connect iliyofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Novemba 20, 2026. Kupitia hafla hiyo, Vodacom Tanzania ilitoa elimu kuhusu matumizi ya huduma zake za mawasiliano na fedha kwa njia ya kidijitali, ikiwahamasisha vijana kutumia teknolojia kurahisisha shughuli zao za kila siku, kujenga tabia ya kuweka akiba na kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi.

Mkuu wa Idara ya Bei za Bidhaa na Makundi Maalumu ya Wateja wa Vodacom Tanzania, Gemma Vedasto Kamara (wa tano kutoka kushoto), akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waliokamilisha mafunzo ya muda mfupi kupitia mpango wa TECHSTART, wakati wa hafla ya UDSM Freshers Connect iliyofanyika chuoni hapo, Novemba 20, 2026. Wanafunzi hao walionesha vyeti vyao kwa kutumia simu zao kama ishara ya mafanikio baada ya kukamilisha mafunzo hayo, yanayolenga kuwajengea ujuzi wa kidijitali kupitia kozi fupi za Microsoft. Kupitia hafla hiyo, Vodacom Tanzania iliendelea kuonesha dhamira yake ya kuwawezesha vijana kwa kuwapatia fursa za kujifunza, huku pia ikiwahamasisha kutumia huduma ya M-Wekeza kujenga utamaduni wa kuweka akiba na kuwekeza kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.

Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Benki ya Exim Tanzania imezindua kampeni ya miezi mitatu inayolenga kuhamasisha wateja kutumia huduma za kibenki za kidijitali, huku ikitoa fursa ya kujishindia zawadi mbalimbali zikiwemo Sh milioni 15.

Kampeni hiyo inayojulikana kwa jina la *‘Maliza Kirahisi Kidigitali-Kamata Kitita’* itaanza Novemba 2026 hadi Februari 2027, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za kifedha.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mifumo Mbadala ya Kidijitali wa Benki ya Exim Tanzania, Silas Matoi, alisema wateja watapata nafasi ya kujishindia zawadi kupitia droo za kila wiki, kila mwezi na droo kuu ya mwisho wa kampeni.

Alisema katika droo za kila wiki, wateja 30 watajishindia Sh 50,000 kila mmoja, huku washindi 10 wa droo za kila mwezi wakipata Sh 500,000 kila mmoja.

Aidha, katika droo kuu, washindi watatu watajishindia zawadi za Sh milioni tano, milioni 10 na milioni 15 kulingana na nafasi zao.

Matoi alisema kampeni hiyo inalenga kuwahamasisha wateja kufanya miamala yao ya kila siku kupitia njia za kidijitali, ambazo zinawawezesha kupata huduma kwa haraka na urahisi bila kulazimika kutembelea matawi ya benki.

Alitaja njia hizo kuwa ni pamoja na Exim Pay, huduma ya USSD kupitia namba *150*11#, Internet Banking, Exim WhatsApp Banking, Exim Wakala na Exim Mastercard.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo, Kauthar D'souza, alisema kampeni hiyo inalenga kuongeza matumizi ya huduma za kidijitali kwa kuwapa wateja motisha ya kushiriki katika miamala yao ya kawaida na kupata nafasi ya kushinda zawadi.

Aliwahimiza wateja kutumia huduma hizo na kuzingatia vigezo na masharti ya kampeni ili kunufaika na fursa zilizopo.

Naye Afisa Mkaguzi wa Michezo ya Kubahatisha, Pendo Albert Mfuru, alisema droo za kampeni hiyo zitaendeshwa kwa mfumo wa kielektroniki unaochagua washindi kwa nasibu chini ya usimamizi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania.

Alisema usimamizi huo unalenga kuhakikisha mchakato wa kupata washindi unafanyika kwa haki na uwazi, huku washiriki wanaotimiza vigezo na masharti wakipata nafasi sawa ya kuwania zawadi.

 Kampeni hiyo ni sehemu ya juhudi za Benki ya Exim Tanzania kuendelea kuwekeza katika mifumo ya kisasa na kupanua upatikanaji wa huduma za kifedha kupitia teknolojia.

Benki ya Exim Tanzania ilianzishwa mwaka 1997 na inatoa huduma kwa watu binafsi na biashara. Mbali na Tanzania, benki hiyo inaendesha shughuli zake Comoros, Djibouti na Uganda, pamoja na kuwa na ofisi ya uwakilishi nchini Ethiopia.

Neema Temba, Mkurugenzi wa Masuala ya Sheria na Uhusiano TBL (wa pili kulia), na Mkurugenzi wa Maendeleo kutoka Taasisi ya Tanzania Red Cross Society (TRCS), Reginald Mhango (wa pili kushoto), wakizungumza na waandishi wa habari wakati wa kusaini hati ya makubaliano (MoU) ya mpango wa mafunzo ya waendesha pikipiki katika wilaya zote tano za jiji la Dar es salaam yenye lengo la kuepusha ajali za barabarani zinazotokana na uzembe wa waendesha pikipiki. Wengine katika picha ni Afisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka Tanzania Redcross Society Simon Kadogosa(kulia), na Catherine Mabula, Afisa Mawasiliano TBL.Na

 Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Kampuni ya Tanzania Breweries PLC (TBL), kwa kushirikiana na Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania (Tanzania Red Cross Society), imewafundisha waendesha pikipiki 1,624 jijini Dar es Salaam kuhusu usalama barabarani na huduma ya kwanza, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza ajali na kuokoa maisha.

Mafunzo hayo yaliyotolewa kupitia ushirikiano ulioanza mwaka 2024 yamevuka lengo la kuwafikia waendesha pikipiki 1,600, na kufikia asilimia 102 ya lengo lililowekwa.

Mafunzo hayo yalifanyika katika wilaya zote tano za Dar es Salaam, yakilenga kuwajengea washiriki uelewa kuhusu uendeshaji salama, sheria na kanuni za barabarani, matumizi sahihi ya helmeti, hatua za kuchukua wakati wa dharura na kufanya maamuzi sahihi wanapotumia barabara.

Akizungumza kuhusu programu hiyo, Mkurugenzi wa Masuala ya Sheria na Uhusiano wa Kampuni wa TBL, Neema Temba, alisema kampuni inaamini kuwa jamii salama ni msingi wa maendeleo na ustawi wa wananchi.

Alisema usalama barabarani unahusisha kulinda maisha ya watu, familia na vyanzo vyao vya kipato, hivyo elimu kwa waendesha pikipiki ni muhimu katika kuzuia ajali na kuhakikisha wanarejea nyumbani salama.

“Usalama barabarani si tu kuzuia ajali; ni kulinda familia, kulinda vyanzo vya kipato na kuhakikisha watu wanarejea nyumbani salama kila siku,” alisema Temba.
Aliongeza kuwa mwitikio mzuri wa washiriki na kuvuka lengo la mafunzo vinaonesha umuhimu wa kuendeleza programu hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Tanzania Red Cross Society, Lucia Pande, alisema usalama barabarani ni jukumu la kila mmoja na kwamba kuwapatia waendesha pikipiki stadi za huduma ya kwanza kunaongeza uwezo wa jamii kukabiliana na dharura.

Alisema waendesha pikipiki mara nyingi huwa miongoni mwa watu wa kwanza kufika katika maeneo ya ajali, hivyo maarifa ya huduma ya kwanza yanaweza kusaidia kutoa msaada wa haraka kwa waathirika kabla ya kufikishwa hospitalini.

Katika hatua nyingine, TBL imeendelea kuhamasisha matumizi sahihi ya barabara na maamuzi yenye uwajibikaji, ikisisitiza kuwa unywaji wa pombe na uendeshaji wa pikipiki haviendani.

Kampuni hiyo imesema itaendelea kushirikiana na wadau kupanua programu za elimu ya usalama barabarani na huduma ya kwanza ili kuongeza uelewa na kujenga jamii yenye uwezo zaidi wa kuzuia na kukabiliana na ajali.

Matokeo ya Wilaya;

Na Mwandishi Wetu- Morogoro 

Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), kupitia Ofisi yake ya Ushauri wa Kitaalamu (OCB), kinaendesha mafunzo ya uandaaji wa Mpango wa Mwaka wa Ufuatiliaji na Tathmini na Mwongozo Tendaji wa Ufuatiliaji na Tathmini mjini Morogoro.

Mafunzo hayo yanafanyika kwa awamu ya pili yalianza tarehe 10 Novemba 2026 na inatarajiwa kuhitimishwa tarehe 16 Novemba 2026, yameshirikisha washiriki kutoka mamlaka za serikali za mitaa na sekretariati za mikoa ya Simiyu, Iringa na Pwani.

Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo, Mkuu wa chuo Kikuu huria (OUT) Prof. Alex Makulilo amesema,  mafunzo hayo yamejikita katika kazi za vitendo, ambapo washiriki wanaandaa nyaraka za taasisi kwa msaada wa wawezeshaji wa Chuo Kikuu Huria (OUT). 

Aidha, amesema, washiriki wanajifunza kuandaa viashiria vya kupima utendaji, zana za kukusanya taarifa na utaratibu wa kutoa taarifa za utekelezaji wa mipango na miradi ya maendeleo.

"Kila taasisi inayoshiriki inatarajiwa kuondoka na rasimu ya Mpango wa Mwaka wa Ufuatiliaji na Tathmini pamoja na Mwongozo Tendaji kwa ajili ya kukamilishwa na kutumika" amesema Prof. Alex Makulilo.

Ameendelea kusema kwamba, Mwongozo huo utaweka taratibu za kukusanya na kuchambua taarifa, kutoa taarifa za utekelezaji na kutumia matokeo katika maamuzi.

Akizungumza kwa niaba ya  Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini Tanzania Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Bi. Sakina Mwinyimkuu, Afisa Ufuatiliaji na Tathmini Bi. Ashura Selemani, amesema matumizi ya nyaraka hizo zitaboresha ufuatiliaji na tathmini kwa kuweka utaratibu unaoeleweka wa kupima utekelezaji na kubaini mapungufu mapema.

Nae Mratibu wa mafunzo hayo, Dk. Emmanuel Mallya, ameeleza kuwa awamu ya tatu ya mafunzo hayo itafanyika mjini Morogoro kuanzia tarehe 30 Novemba hadi 4 Desemba 2026, ambapo awamu hiyo itahusisha mamlaka za serikali za mitaa na sekretariati za mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Tabora, Shinyanga, Singida, Dodoma, Mara, Kilimanjaro, Arusha na Katavi. Pia itazihusisha halmashauri nyingine ambazo, kwa sababu mbalimbali, hazikuweza kuhudhuria awamu zilizopita.

Hata hivyo Mwisho wa mafunzo hayo, Chuo kitaandaa taarifa rasmi itakayowasilishwa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Na Mwandishi Wetu.

Vyombo vya habari nchini vimetakiwa kuandaa habari za kina zinazoibua changamoto halisi zinazowakabili wananchi katika kuanza na kuendelea kutumia nishati safi ya kupikia, ili kuchochea upatikanaji wa suluhisho na kufanikisha malengo ya kitaifa.

Wito huo umetolewa leo, Novemba 13, 2026, na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Patrick Kipangula, wakati akifungua Mkutano wa Wadau wa Nishati Safi ya Kupikia kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ulioandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Dar es Salaam (DAR-PC), jijini Dar es Salaam.

Wakili Kipangula amependekeza kila chombo cha habari kuandaa angalau habari moja ya kina inayojibu changamoto zinazowakabili wananchi, ikiwemo gharama za kuanza kutumia nishati safi, usalama wa vifaa, upatikanaji wake, changamoto za usambazaji, uzoefu wa watumiaji pamoja na fursa za biashara na uwekezaji.

“Habari tunazotoa zinapaswa kujibu maswali ya wananchi na kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi. Ni muhimu kuwaelimisha kuhusu gharama za matumizi, usalama wa vifaa na upatikanaji wa nishati safi katika maeneo yao,” amesema Wakili Kipangula.

Amesema Waandishi wa Habari wana nafasi muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi, rahisi kueleweka na zinazozingatia mazingira yao kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Ameeleza kuwa habari zinazobeba uzoefu wa wananchi na ushahidi wa kutosha zinaweza kuisaidia Serikali pamoja na wadau wengine kutambua mafanikio yaliyopatikana na maeneo yanayohitaji kuboreshwa.

Aidha, Wakili Kipangula amewataka Waandishi wa Habari kuzingatia ukweli, takwimu sahihi na maadili ya taaluma wanaporipoti masuala ya nishati safi, akisisitiza kuwa kasi ya kutoa taarifa haipaswi kupewa nafasi kuliko usahihi wake.

“Habari ya kwanza si bora kama si sahihi. Mwandishi wa Habari mwenye weledi si yule anayewahi kutoa taarifa pekee, bali ni yule anayehakikisha taarifa anayotoa ni ya kweli, imehakikiwa na ina manufaa kwa jamii,” amesema.

Ameongeza kuwa Serikali imeandaa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024 hadi 2034, unaolenga kufikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa asilimia 80 ya Watanzania ifikapo mwaka 2034.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa DAR-PC, Bw. Bakari Kimwanga, ameeleza mafanikio ya klabu hiyo, yakiwemo kuongezeka kwa idadi ya wanachama, Waandishi wa Habari kuendelea kujiendeleza kielimu na kuimarika kwa ushirikiano na maafisa pamoja na wadau mbalimbali katika upatikanaji wa taarifa.

Mkutano huo umefanyika chini ya kaulimbiu isemayo, “Nishati Safi ya Kupikia kwa Maendeleo Endelevu kuelekea Dira ya Taifa 2050,” ukiwakutanisha Waandishi wa Habari, wataalamu, taasisi za Serikali, sekta binafsi na wadau wa sekta ya nishati.
Tume ya Taifa ya UNESCO (NATCOM) imesisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi shirikishi wa Hifadhi ya Biosphere ya Rufiji-Mafia-Kilwa-Kibiti (RUMAKI), kwa kuzingatia uwiano kati ya uhifadhi wa bioanuwai, maendeleo endelevu ya jamii na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari na pwani.

Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mtendaji wa Programu wa Tume ya Taifa ya UNESCO, Dkt. Khamis Khalid Said, wakati wa kufungua rasmi Kikao cha Kitaalamu cha Kuhakiki Rasimu ya Mpango Mkuu wa Usimamizi (GMP) wa Hifadhi ya Biosphere ya RUMAKI kilichofanyika katika Ukumbi wa TUJIWAKI, Kilwa Masoko, Wilaya ya Kilwa, Mkoa wa Lindi.
Kikao hiki kinalenga kupitia na kuboresha rasimu ya mpango huo ili kuhakikisha unazingatia changamoto zinazokabili mifumo ikolojia ya bahari na pwani, zikiwemo athari za mabadiliko ya tabianchi, uvuvi uliokithiri na uharibifu wa makazi ya viumbe vya baharini.

Mpango huo unalenga kulinda mifumo muhimu ya ikolojia, ikiwemo misitu ya mikoko, miamba ya matumbawe na maeneo ya kutagia mayai ya kasa, sambamba na kuimarisha maisha ya jamii za pwani kupitia uvuvi endelevu, utalii wa kiikolojia na ufugaji endelevu wa viumbe vya majini.
Kupitia Mpango wa UNESCO wa Binadamu na Hifadhi Hai (MAB), NATCOM inaendelea kuratibu na kusimamia juhudi za kuunganisha uhifadhi wa bioanuwai, utafiti wa kisayansi na maendeleo endelevu, kwa kuhakikisha kuwa uhifadhi wa mazingira unaenda sambamba na ustawi wa jamii na vizazi vijavyo.

Uhifadhi wa mazingira ni uwekezaji katika maisha ya sasa na mustakabali wa vizazi vijavyo.
#UNESCOTanzania #RUMAKI #MABProgramme #Biodiversity #SustainableDevelopment
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman (wapili kulia), akipokea mkoba wenye machapisho yanayohusu utekelezaji wa majukumu ya Mfuko wa PSSSF, kutoka kwa Meneja wa Mfuko huo Ofisi ya Zanzibar, Bi. Mariam Saleh, alipotembelea Banda la PSSSF kwenye Maonesho yanayofanyika sambamba na Mkutano wa 11 wa Mtandao wa Wasimamizi wa Rasilimaliwatu katika Taasisi za Umma Barani Afrika ( APS-HRMnet) mjini Unguja, Zanzibar Novemba 10, 2026.

Meneja Rasilimali Watu Bi. Gloria Mboya kulia, akiwa na Meneja wa Ofisi ya PSSSF Zanzibar, Bi. Mariam Saleh, wakitoa huduma kwa mwanachama katika banda la Maonesho ya Mkutano wa 11 wa APS-HRMnet (11th APS-HRMnet Annual Conference Delegates) unaoendelea Verde Hoteli, Zanzibar.

Meneja wa Utawala Bi. Fatma Chondo wa kwanza kulia akiwa na Afisa utekelezaji Bi. Zakia Mohamed, wakitoa huduma kwa wanachama wakati wa Maonesho ya Mkutano wa 11wa Mwaka wa APS-HRMnet (11th APS-HRMnet Annual Conference Delegates) Verde Hotel, Zanzibar. Novemba 10,2026.

Makamu wa Kwanza wa Rais, Mhe.Othman Masoud Othman, akimsikiliza Meneja wa Ofisi ya Zanzibar ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Bi. Mariam Saleh alipotembelea banda la mfuko huo kwenye Maonesho ya Mkutano wa 11 wa Mwaka wa APS-HRMnet (11th APS-HRMnet Annual Conference Delegates) Hotel Verde, Zanzibar. Novemba 10, 2026.

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, ameipongeza PSSSF kwa matumizi ya kidijitali katika kutoa huduma, amesema kwamba imechangia kwa kiasi kikubwa kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wanachama na kuwaondolea usumbufu wa kufika mara kwa mara katika ofisi za Mfuko kufuata huduma.

Mhe. Othman ameyasema hayo leo, Novemba 10, 2026, alipotembelea banda la PSSSF katika Maonesho ya Mkutano wa 11 wa Mwaka wa APS-HRMnet (11th APS-HRMnet Annual Conference Delegates) yaliyofanyika Zanzibar.

Akizungumza baada ya kupata maelezo kuhusu huduma zinazotolewa na Mfuko, Mhe. Othman alisema kuwa matumizi ya mifumo ya kidijitali yameleta urahisi mkubwa kwa wanachama.

Mhe. Othman, alimuwakilisha Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kufungua mkutano huo, katika Banda la PSSSF alipokelewa na Meneja wa PSSSF Ofisi ya Zanzibar, Bi. Mariam Saleh aliyemueleza namna Mfuko ulivyoendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa kutumia ambapo sasa huduma zote zinapatikana kidijitali ili kuongeza ufanisi na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wanachama.

Aidha, alielezwa kaulimbiu mpya ya Mfuko isemayo 'Tunalipa Jana', inayosisitiza dhamira ya PSSSF ya kuhakikisha wanachama wanapata mafao yao kwa wakati na kwa ufanisi zaidi ikiwemo kuimarisha mifumo ya usimamizi na ufuatiliaji wa michango ili kuwezesha ulipaji wa mafao kwa wakati.