Na Fatma Salum- MAELEZO.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema kuwa Serikali kupitia Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) itaendelea na zoezi la ukaguzi wa vyuo vya elimu ya juu kila mwaka na taarifa za vyuo husika zitakuwa zikitolewa kabla ya udahili kuanza.

Ndalichako aliyasema hayo mapema wiki hii wakati akizungumza kuhusu utekelezaji wa wizara hiyo katika kipindi cha ‘Tunatekeleza’ kilichorushwa na kituo cha Televisheni cha TBC.

Alibainisha kuwa Serikali imedhamiria kuboresha elimu ya juu kwa kuhakikisha vyuo vyote vimekidhi vigezo na kutoa elimu yenye viwango vinavyotakiwa na vyuo vitakavyokosa sifa vitafungiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.

“Zoezi hili la ukaguzi wa vyuo vya elimu ya juu ni endelevu na wanafunzi wanaohamishwa kutoka katika vyuo vilivyofungiwa wataendelea kupata mikopo yao kama kawaida katika vyuo watakavyohamishiwa,” alisisitiza Ndalichako.

Pia alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imepanga kufanya tathmini kwa programu 100 za masomo mbalimbali katika vyuo vikuu nchini na kuzisajili zitakazokidhi vigezo.

Aidha katika mwaka huu wa fedha Serikali itafanya tathmini na kutambua tuzo 2,500 za ngazi ya shahada zilizotolewa katika vyuo vya elimu ya juu vilivyopo nje ya nchi.

“Katika mwaka huu wa fedha tutaendelea kusimamia ubora wa elimu ya juu kwa kupitia mifumo na miongozo mbalimbali inayotumika kusimamia udhibiti na ithibati ya elimu ya juu hapa nchini,” alibainisha Ndalichako.

Pia alieleza kuwa Serikali itaendelea kuhakiki wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaodahiliwa katika vyuo vya elimu ya juu ili kujiridhisha kama wamekidhi vigezo vya kudahiliwa katika programu husika.

Akizungumzia kuhusu mikopo ya elimu ya juu, Ndalichako alisema kuwa urejeshaji wa mikopo umeongezeka kutoka shilingi bilioni 28 mwaka 2015/2016 hadi bilioni 181 mwaka 2017/2018 kutokana na hatua madhubuti zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano.

Mwaka 2016 Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) ilifanya ukaguzi maalum wa kuhakiki ubora wa vyuo na kubaini changamoto zinazoathiri utoaji wa elimu bora katika baadhi ya vyuo hapa nchini na kuweza kuvichukulia hatua mara moja.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: