Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi (kushoto), Katibu Tawala Msaidizi mkoa wa Arusha Miundombinu Mahmoud Mansour (kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa TANFOAM Riaz Lemtula (katikati) na Mshauri wa TANFOAM Victor Njau wakijadiliana na namna ya kumega eneo kwa ajili ya wafugaji wa kimasai wa kijiji cha Lengiroliti wilaya ya Monduli mkoa wa Arusha wakati Waziri wa Ardhi alipokwenda kutatua mgogoro wa ardhi baina ya kijiji hicho na Mwekezaji.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuviu akijadiliana na wafugaji wa kimasai wa kijiji cha Lengiroliti wakati alipokwenda kutatua mgogoro wa ardhi kati ya kijiji hicho na mwekezaji wa Shamba TANFOAM. Kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo na wa tatu kushoto ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Lengiroliti Baraka Lemai.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na wananchi wa vijiji vya Lengiroliti na Naaralami wilaya ya Monduli mkoa wa Arusha alipokwenda kutatua mgogoro wa ardhi baina ya vijiji hivyo na wawekezaji wa mashamba TANFOAM NA na SLUIS. Kulia ni Mkurugenzi wa TANFOAM Riaz Lemtula (PICHA NA WIZARA YA ARDHI).

Na Munir Shemweta, WANNM MONDULI.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amemaliza mgogoro uliodumukwa muda mrefu baina ya wananchi wa vijiji vya Lengiloriti na Naalarami vilivyopo wilayani Monduli mkoani Arusha na wawekezaji wa mashamba yanayomilikiwa na TANFOAM na SLUIS kwa kuamua kumega sehemu za mashamba na kuwapatia wananchi wa vijiji hivyo.

Lukuvi alifikia umauzi huo baada ya kukutana na pande zote mbili jana tarehe 23 Aprili 2019 wilayani humo na kujadiliana kwa kina kwa takriban saa tano kwa lengo la kupata suluhu ya mgogoro huo ambao umeleta sintofahamu kati ya wananchi wa vijiji hivyo na wawekezaji wa mashamba.

Katika makubaliano hayo iliamuliwa ekari kati ya 850 hadi 900 zimegwe kutoka kwa muwekezaji TANFOAM na kugawiwa kwa kijiji cha Lengiloriti wilayani Monduli kutoka shamba namba 44 lenye ukubwa wa ekari 3098. Aidha, upande wa muwekezaji SLUIS jumla ya ekari 2000 za muwekezaji zimetolewa kwa kijiji cha Naaralami, NAFCO, Lokisari na Tukusi ambapo sasa muwekezaji atabaki na aekari 2217 badala ya 4,217 alizokuwa nazo awali.

Kwa mujibu wa Lukuvi, ardhi iliyomegwa na kurudishwa katika vijiji hivyo itakuwa chini ya mamlaka ya kijiji ambacho ndicho kitakuwa na jukumu la kuigawa upya kwa wananchi wa vijiji husika na baadaye kupangwa matumizi bora ya ardhi.

Akizungumzia kijiji cha Lengiloriti, Waziri wa Ardhi aliwataka wananchi wenye Maboma yaliyokuwa ndani ya eneo la shamba la muwekezaji TANFOAM kuhamia eneo jipya walilotengewa katika kipindi cha miezi mitatu ili kupisha muwekezaji kuendelea na shughuli za kilimo na kutotekelezwa kwa aina yoyote agizo hilo kutaifanya serikali kuchukua hatua.

Maboma yaliyohamishwa ni pamoja na linaloongozwa na mwenyekiti wa kijiji cha Lengiloriti Baraka Lemai. Maboma mengine ni la Kaay Rao, Remi Paraleti, Kelemo Kipara, Yamat Miriliali, Bete Kabulua, Barik Simon, Rais Ramadhani, Ramadhani Hamis na Lakalai Olodo ambapo Waziri wa Ardhi alisisitiza wamiliki wa Maboma hayo kupewa kipaumbele wakati wa kugawiwa ekari zilizotolewa na kiasi kitakachobaki wapatiwe wananchi wengine.

Aidha, ameagiza kuanzia wiki hii timu ya upimaji ardhi mkoani Arusha iende ktika eneo hilo kwa ajili ya kuweka mipaka/alama za kudumu ili kuepuka uvamizi mwingine unaoweza kutokea na kuagiza wawekezaji na wananchi wa vijiji vilivyopatiwa ekari hizo kuchangia fedha kwa ajili ya upimaji ambapo muwekezaji na wananchi walikubali kutoa milioni tano kwa ajili ya upimaji.

Kuhusu mgogoro wa muwekezaji SLUIS, Lukuvi alisema muwekezaji huyo amekubali kutoa ekari 520 kwa kijiji cha Naaralami pamoja na ekari 300 kwa ajili ya kupitishia mifugo ya wananchi wa kijiji hicho huku ekari 513 zikitolewa kwa NAFCO, 366 kwa Lokisari na ekari 301 kwa kijiji cha Tukusi.

Lukuvi alisema serikali inawaeshimu sana wawekezaji wa sekta ya ardhi kwa kuwa wanalipa kodi inayosadia utoaji wa huduma za jamii huku wananchi nao wakipata ajira na kusisisitiza kuwa wawekezaji wanaomiliki mashamba kisheria serikali itawalinda na kuonya baadhi ya viongozi wa vijiji kujigawia maeneo bila ya kushirikisha wananchi wa vijiji husika.

‘’Nimekuja kusuluhisha mgogoro siyo kunyanganya wawekezaji mashamba, wawekezaji wamekubali kupunguza mashamba yao na hayo mashamba siyo mali ya wananchi wanaoishi katika maboma yaliyohamishwa bali ni mali ya kijiji ambacho kitakuwa na jukumu la kugawa maeneo hayo’’ alisema Lukuvi

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo alisema kuwa, baada ya makubaliano ya pande zote mbili anategemea kila upande utaheshimu maamuzi yaliyotolewa na mtu yoyote atakayekiuka basi serikali ya mkoa itachukua hatua kali dhidi yake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanfoam Riaz Lemtula amepongeza jitihada iliyofanywa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi mpaka kufikia muafaka wa suala hilo na kuahidi kutekeleza makubaliano waliyoafikiana kwa lengo la kuleta maendeleo.

Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Lengiroliti Baraka Lemai alimshukuru Waziri wa Ardhi kwa niaba ya Kijiji chake kwa kazi anayoifanya ya kutatua migogoro ya ardhi na kuahidi kushirikiana na wawekezaji waiokubali kumega maeneo yao kwa ajili ya kijiji.

Wawekezaji wanaomili mashamba katika vijiji hivyo wamekuwa wakiendesha mashamba yao katika shughuli za kilimo ambapo hulima mazoa ya Maharage, Mtama, Ngwara na mahindi na kusafirisha mazo hao katika nchi za Sweden, Canada na Uholanzi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: