Charles James, Michuzi TV

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo amewataka Walimu kujiunga na benki ya walimu ili waweze kuongeza mtaji kutokana na miamala itakayofanyika mara kwa mara.

Jafo ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akizindua benki ya mwalimu visa card ambayo itawarahisishia walimu kufanya miamala kwa njia ya kidigitali mahali popote walipo.

“Kuna kazi kubwa ya kujenga uelewa kwa walimu na kuwashawishi kuhusu faida za kujiunga na benki yao na walimu wakiwa wengi benki yenu itakuwa kubwa na kupata faida kubwa,” Amesema Waziri Jafo.

Waziri Jafo pia amesema kupitia benki hiyo walimu wanapaswa kuweka mazingira wezeshi yatakayosaidia walimu kuchukua mikopo kwa riba nafuu kwani hiyo itakuwa njia rahisi ya kuwavuta walimu wengi kujiunga na benki hiyo.

" Walimu wamekuwa watumwa huko mitani wanachukua mikopo umiza tena kwa riba kubwa ambayo inapelekea wengine kufukuzwa kazi kutokana na mawazo yanayosababishwa na mikopo hiyo.

Walimu wanapigwa sana kwenye suala la mikopo, wengi wamewekeza kadi zao za benki wanakatwa hela nyingi, naomba benki hii ikawe chachu ya mabadiliko na kuwafuta machozi walimu baada ya kilio cha muda mrefu,”alieleza

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Walimu, Francis Ramadhan amesema Mwalimu Commercial Benki iliandaa mkakati wa muda mrefu ukiwa na malengo ya kuboresha huduma zenye ubunifu na ufanisi katika kuwafikia wateja.

Amesema katika mikakati hiyo ni pamoja na utoaji huduma za kisasa kwa njia ya kidijitali na kuwafikia wateja zaidi ya 41000 pamoja na wateja tarajiwa ambao ni walimu na wanahisa zaidi ya 200000.

“ Mwalimu Commercial Benki ni benki iliyojikita kutoa huduma za kifedha kwenye ikolojia ya elimu ikiwa ni pamoja na walimu mashuleni, Taasisi za za elimu,TAMISEMI, na wadau wote wa elimu,”Amesema Ramadhani.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu (CWT) Deus Seif amewataka walimu wote nchini kujiunga na benki yao ambayo itawawezesha kuchukua mikopo yenye riba nafuu.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: