Meneja Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania, Kauthar D’souza (kushoto), akisalimiana na Mwanzilishi Mwenza wa Taasisi ya Wanasayansi Chipukizi Tanzania (YST), Dkt. Gozibert Kamugisha (kulia), muda mfupi baada ya Benki ya Exim Tanzania na YST kuzindua ushirikiano wa mwaka 2026 kupitia Programu ya YST 2026 jijini Dar es Salaam. Ushirikiano huo unaofikisha mwaka wa sita unaendelea kuwawezesha vijana wa Kitanzania kutumia sayansi, utafiti na ubunifu kubuni suluhisho za changamoto za jamii. Kwa mwaka huu, miradi 1,330 kutoka shule 287 za sekondari imewasilishwa, huku miradi 45 bora ikitarajiwa kushiriki Maonesho ya Kitaifa ya Sayansi na Teknolojia ya YST yatakayofanyika tarehe 17 Septemba 2026 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo kupitia wataalamu wake, Benki ya Exim Tanzania imeshiriki kutoa ulezi na ushauri wa kitaalamu kwa wanafunzi na walimu ili kuboresha tafiti na ubunifu wao. Uzinduzi wa ushirikiano huo umefanyika tarehe 31 Julai 2026 katika Makao Makuu ya Benki ya Exim Tanzania.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Benki ya Exim Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Wanasayansi Chipukizi Tanzania (YST) wamezindua rasmi Programu ya YST 2026, wakiahidi kuendelea kuwawezesha vijana wabunifu kupitia sayansi, teknolojia, utafiti na ubunifu.
Uzinduzi huo uliofanyika Julai 31, 2026 katika Makao Makuu ya Benki ya Exim (Exim Tower), Dar es Salaam, umeadhimisha miaka sita ya ushirikiano kati ya taasisi hizo katika kukuza vipaji vya wanafunzi wa shule za sekondari nchini.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Meneja Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania, Kauthar D'Souza, alisema benki hiyo inaamini kuwa uwekezaji kwa vijana ni msingi wa kujenga taifa lenye ushindani na maendeleo endelevu.
Alisema kupitia falsafa ya benki hiyo ya *"Ubunifu ni Maisha"*, Exim imeendelea kuwaunga mkono wanafunzi wenye vipaji vya ubunifu na kuwapa fursa ya kutumia sayansi na utafiti kutatua changamoto zinazozikabili jamii.
Kwa mujibu wa D'Souza, programu ya mwaka huu imeweka rekodi mpya baada ya kupokea miradi 1,330 kutoka shule 287 za sekondari katika mikoa yote ya Tanzania. Baada ya tathmini ya kitaalamu, miradi 162 imechaguliwa kuingia hatua inayofuata, huku miradi 45 bora ikitarajiwa kushiriki Maonesho ya Kitaifa ya Sayansi na Teknolojia yatakayofanyika Septemba 17, 2026 katika Ukumbi wa Maktaba Mpya wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Alieleza kuwa wataalamu wa benki hiyo wamekuwa wakishiriki moja kwa moja katika kutembelea shule, kutoa ushauri wa kitaalamu kwa walimu na wanafunzi pamoja na kusaidia kuboresha tafiti na miradi ya ubunifu.
Hata hivyo, Dkt. Kamugisha alisema YST bado inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa rasilimali fedha na uelewa mdogo wa jamii kuhusu umuhimu wa kuwekeza katika maendeleo ya vijana wabunifu.
Alisisitiza kuwa maendeleo ya taifa hayawezi kufikiwa bila uwekezaji wa kutosha katika sayansi, teknolojia na ubunifu wa vijana, akibainisha kuwa mataifa yaliyopiga hatua yamefanikiwa kutokana na kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika tafiti na ugunduzi.
Kwa zaidi ya miaka 16, YST imekuwa ikiwajengea uwezo wanafunzi wa shule za sekondari katika utafiti wa kisayansi na ubunifu, huku ushirikiano wake na Benki ya Exim ukiendelea kusaidia vijana kubuni suluhisho katika maeneo mbalimbali ikiwemo akili unde (AI), kilimo, afya, uhifadhi wa mazingira, usalama wa chakula na teknolojia za mawasiliano.




Toa Maoni Yako:
0 comments: