
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Tamasha la Kizimkazi limekuwa kichocheo muhimu cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii, huku eneo hilo likizidi kufunguka kwa fursa za biashara, uwekezaji na utalii kwa wananchi wa Kusini, Zanzibar na maeneo jirani.
Akizungumza leo, Ijumaa, Agosti 14, 2026, katika kilele cha Tamasha la Kizimkazi, Rais Samia amesema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2016, tamasha hilo limeendelea kukua na kuacha alama katika maendeleo ya eneo hilo kupitia kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi pamoja na uboreshaji wa miundombinu na huduma mbalimbali.
Rais Samia amesema mabadiliko yanayoendelea Kizimkazi yameifanya eneo hilo kuwa sehemu yenye mazingira yanayofaa zaidi kwa wafanyabiashara na wawekezaji, akiwataka kutumia fursa zilizopo kuanzisha na kuendeleza shughuli zitakazoongeza ajira na kuchochea uchumi wa eneo hilo.
“Tunawakaribisha kuja kuwekeza, mazingira mazuri ya uwekezaji yamekwishawekwa,” amesema Rais Samia, akisisitiza umuhimu wa sekta binafsi kutumia fursa zinazotokana na maendeleo yanayoendelea kufanyika Kizimkazi.
Amesema pia Serikali inaendelea na ujenzi wa uwanja wa michezo ambao ukikamilika utakuwa miongoni mwa miundombinu itakayotumika katika michuano ya AFCON 2027. Kwa kuzingatia idadi ya wageni, wanamichezo na washiriki watakaotarajiwa kufika, Rais Samia amewataka wawekezaji kuona fursa katika sekta za malazi, chakula, usafiri, burudani na huduma nyingine zitakazohitajika.


Toa Maoni Yako:
0 comments: