Na Mwandishi Wetu.

DAR ES SALAAM: Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, amewapongeza walimu wa Kata ya Ukonga kwa mchango wao katika jamii, akisema wamekuwa msingi muhimu wa uzalishaji wa wataalamu na viongozi mbalimbali nchini.

Mhe. Mpogolo ameyasema hayo wakati wa sherehe ya walimu wa Kata ya Ukonga, inayojulikana kama UKONGA DAY, iliyofanyika Ukonga jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Mpogolo amesema walimu wana nafasi kubwa katika maendeleo ya Taifa kwa kuwa ndio wanaowaandaa wanafunzi kuwa wataalamu na viongozi wanaokuja kuliongoza na kulitumikia Taifa.
Amesema mchango wa walimu hauishii darasani pekee, bali unaendelea kuonekana kupitia mafanikio ya wanafunzi wao katika nyanja mbalimbali za maisha.

Mhe. Mpogolo ametoa pongezi hizo kufuatia hotuba ya utangulizi iliyotolewa na mgeni maalum wa hafla hiyo, Mhe. Jerry Silaa, ambaye pia ni mlezi wa walimu wa Kata ya Ukonga.

Mhe. Silaa ana historia ya kipekee na eneo hilo, kwani amezaliwa katika Kata ya Ukonga na kusoma katika Shule ya Msingi Ukonga.
Katika safari yake ya maisha, amekuwa akirejea katika eneo hilo na kutoa shukrani kwa walimu wa Kata ya Ukonga, akiwatambua kuwa miongoni mwa watu waliochangia kwa kiasi kikubwa mafanikio yake.

Aidha, Mhe. Mpogolo amesema walimu ni miongoni mwa watu wanaofurahia mafanikio ya wale waliowafundisha, akieleza kuwa mafanikio ya mwanafunzi ni sehemu ya mafanikio ya mwalimu.

Amesema tofauti na baadhi ya watu ambao wanaweza kuwa na wivu wanapowaona wenzao wakifanikiwa, walimu hufurahia kuona wanafunzi wao wakipiga hatua na kufikia mafanikio makubwa.

Kwa mujibu wa Mhe. Mpogolo, hali hiyo inaonesha umuhimu wa kutambua na kuthamini mchango wa walimu katika kujenga jamii na Taifa kwa ujumla.
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: