Articles by "HABARI PICHA"
Showing posts with label HABARI PICHA. Show all posts

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameagwa rasmi na Menejimenti ya Wizara ya Nishati pamoja na Taasisi zilizo chini yake katika hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Kambarage Treasury Square, Dodoma. Jumatano Septemba 09, 2026.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughukia Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Felchesmi Mramba, Menejimenti ya Wizara na Wakurugenzi wa Taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu wa Rais amewaasa Viongozi na Watendaji hao kuendelea kumwombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Wasaidizi wake ili waendelee kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia Watanzania.

Aidha, Makamu wa Rais amewataka Viongozi na Watendaji hao kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi, uaminifu na uzalendo ili kutimiza matarajio ya wananchi kwa Serikali.












Na Mwandishi Wetu.

DAR ES SALAAM: Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, amewapongeza walimu wa Kata ya Ukonga kwa mchango wao katika jamii, akisema wamekuwa msingi muhimu wa uzalishaji wa wataalamu na viongozi mbalimbali nchini.

Mhe. Mpogolo ameyasema hayo wakati wa sherehe ya walimu wa Kata ya Ukonga, inayojulikana kama UKONGA DAY, iliyofanyika Ukonga jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Mpogolo amesema walimu wana nafasi kubwa katika maendeleo ya Taifa kwa kuwa ndio wanaowaandaa wanafunzi kuwa wataalamu na viongozi wanaokuja kuliongoza na kulitumikia Taifa.
Amesema mchango wa walimu hauishii darasani pekee, bali unaendelea kuonekana kupitia mafanikio ya wanafunzi wao katika nyanja mbalimbali za maisha.

Mhe. Mpogolo ametoa pongezi hizo kufuatia hotuba ya utangulizi iliyotolewa na mgeni maalum wa hafla hiyo, Mhe. Jerry Silaa, ambaye pia ni mlezi wa walimu wa Kata ya Ukonga.

Mhe. Silaa ana historia ya kipekee na eneo hilo, kwani amezaliwa katika Kata ya Ukonga na kusoma katika Shule ya Msingi Ukonga.
Katika safari yake ya maisha, amekuwa akirejea katika eneo hilo na kutoa shukrani kwa walimu wa Kata ya Ukonga, akiwatambua kuwa miongoni mwa watu waliochangia kwa kiasi kikubwa mafanikio yake.

Aidha, Mhe. Mpogolo amesema walimu ni miongoni mwa watu wanaofurahia mafanikio ya wale waliowafundisha, akieleza kuwa mafanikio ya mwanafunzi ni sehemu ya mafanikio ya mwalimu.

Amesema tofauti na baadhi ya watu ambao wanaweza kuwa na wivu wanapowaona wenzao wakifanikiwa, walimu hufurahia kuona wanafunzi wao wakipiga hatua na kufikia mafanikio makubwa.

Kwa mujibu wa Mhe. Mpogolo, hali hiyo inaonesha umuhimu wa kutambua na kuthamini mchango wa walimu katika kujenga jamii na Taifa kwa ujumla.
Washindi wa Vodacom Corporate Masters 2026 Golf Tournament katika makundi mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kupokea zawadi zao, Tukio hilo lilifanyika Lugalo Golf Club, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando (kushoto), akikabidhi zawadi ya tiketi ya kwenda na kurudi Mauritius kwa mshindi wa jumla kwa wanaume Khalid Shemndolwa (wa tatu kushoto) katika mashindano ya Vodacom Corporate Masters 2026 Golf Tournament yaliyofanyika Lugalo Golf Club, Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki. Shemndolwa alikusanya point 42 katika mashindano yaliyoshirikisha wachezaji gofu 150 kutoka Tanzania na nje ya nchi.
Mshindi wa jumla kwa upande wa wanawake, Yvonne Ondari (wa tatu kushoto), akipokea zawadi baada ya kutwaa taji katika Vodacom Corporate Masters 2026 Golf Tournament yaliyofanyika Lugalo Golf Club mwishoni mwa wiki. Ondari alikusanya pointi 42 (CB) katika mashindano yaliyoshirikisha wachezaji golf 150 kutoka Tanzania na nje ya nchi.

Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando, akishiriki mashindano ya Vodacom Corporate Masters 2026 Golf Cup yaliyofanyika Lugalo Golf Club, Dar es Salaam, Septemba 5, 2026. Mashindano hayo yalishirikisha wachezaji gofu 150 kutoka Tanzania na nje ya nchi.

Mkuu wa Idara ya Masoko na Uwezeshaji wa Vodacom Business Joseph Sayi, akishiriki mashindano ya Vodacom Corporate Masters 2026 Golf Cup yaliyofanyika Lugalo Golf Club, Dar es Salaam, Septemba 5, 2026. Mashindano hayo yalishirikisha wachezaji gofu 150 kutoka Tanzania na nje ya nchi.

Na Mwandishi Wetu.

Dar es salaam, Septemba 5, 2026:  Vodacom Tanzania PLC, kwa kushirikiana na Oakwood Holdings Limited, imehitimisha mashindano ya Vodacom Corporate Masters 2026 yaliyofanyika katika Uwanja wa TPDF Lugalo Golf Club, yakiwakutanisha wachezaji wapatao 150 kutoka Tanzania na nchi jirani, wakiwemo viongozi wa biashara, wakurugenzi na wakuu wa makampuni pamoja na wapenzi wa mchezo wa golf.

Wachezaji gofu Khalid Shemndolwa na Yvonne Ondari wameibuka washinda kwa jumla shindano la Vodacom Corporate Masters kwa upande wa wanaume na wanawake. Katika shindano hilo lililofanyika kwenye uwanja wa Lugalo, Shemndolwa alikusanya pointi 42 huku Ondari akikusanya pointi kama hizo katika mashindano hayo ya siku moja. 

Mbali ya Shemndolwa na Ondari, Godfrey Abel aliibuka mhsindi katika daraja A, kwa kupata pointi 42, akifuatiwa na Likuli Juma aliyepata pointi 41 ambapo Sigfrid Urassa alitwaa ubingwa wa daraja B kwa pointi 40, akimzidi Godfrey Kilenga aliyemaliza na pointi hizo hizo, lakini Urassa akashinda kwa kanuni ya countback.

Boniface Japhet alitwaa ubingwa wa daraha C  baada ya kupata pointi 39, huku Abdallah Singano akimaliza nafasi ya pili kwa pointi 37. Kwa upande wa wanawake, Neema Job alimaliza na pointi 42 na kutwaa ubingwa, akifuatiwa na Leticia Kapalia aliyepata pointi 40. Mashindano ya timu za kampuni nayo yalikuwa kivutio kikubwa, huku timu ya KQ ikiibuka mshindi baada ya kushindana na timu nyingine tisa za kampuni.

Zawadi maalum za mtu mmoja mmoja zilienda kwa Michael Norbert aliyeshinda Longest Drive kwa wanaume, huku Kapalia akitwaa tuzo hiyo kwa wanawake. Harshid Barmeda alishinda Nearest to the Pin kwa wanaume, wakati Vaileth James akitwaa tuzo hiyo kwa wanawake.

Mbali na ushindani, washiriki pamoja na familia zao walifurahia shughuli mbalimbali katika eneo la Corporate Village, lililokuwa na burudani, maonesho ya biashara, magari ya zamani pamoja na eneo maalum la watoto.

Mkurugenzi wa Vodacom Business wa Vodacom Tanzania PLC, Nguvu Kamando, alisema mashindano hayo yameendelea kuonyesha nafasi ya michezo katika kujenga mahusiano yenye tija katika biashara.

“Vodacom Corporate Masters 2026 Golf Cup imethibitisha tena kwamba michezo ni jukwaa lenye nguvu katika kujenga mahusiano ya muda mrefu ya kibiashara. Tunafurahishwa na ushiriki mkubwa wa kampuni na kasi ya mahusiano mapya yaliyojengwa wiki hii,” alisema Kamando.

Mwenyekiti wa Kamati ya Corporate Masters, Ken Kariuki, alizipongeza kampuni zilizoshiriki na kusema mashindano hayo yanaendelea kuchangia katika kujenga mtandao wa kibiashara na kukuza mchezo wa gofu.“Mwaka huu tulishuhudia ushindani wa kiwango cha juu uwanjani na ushiriki wenye maana katika biashara nje ya uwanja. Hilo ndilo lengo kuu la Corporate Masters, kuzikutanisha kampuni katika mazingira rafiki yanayozalisha fursa halisi za ushirikiano,” alisema Kariuki.

Alisema ushirikiano kati ya Vodacom na Corporate Masters unaonyesha namna kampuni zinavyoweza kufanya kazi pamoja katika kutengeneza thamani kwa wateja na wadau, huku zikiunga mkono maendeleo ya mchezo wa gofu nchini Tanzania.

Kufanikiwa kwa mashindano ya Vodacom Corporate Masters 2026 kunaendelea kuthibitisha mkakati wa Vodacom Tanzania wa kutumia michezo kama jukwaa la kuimarisha mahusiano ya kibiashara, kuhamasisha ubunifu na kuwasogeza karibu viongozi wa biashara na suluhisho za kidijitali zinazochochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN), Beda Msimbe (Kushoto) akizungumza mara baada ya kupokea timu ya maofisa wa PSSSF ilipotembelea Makao Makuu ya Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) yaliyopo Kijitonyama, Dar es Salaam. Kulia ni Mkuu wa Msafara wa PSSSF, Abdul Njaidi.

Na Mwandishi Wetu TBN, DAR ES SALAAM.

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umeeleza dhamira ya kutumia nguvu ya majukwaa ya kidijitali kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa elimu kuhusu hifadhi ya jamii, pensheni na uwekezaji, kupitia ushirikiano na Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN).

Ushirikiano huo umejadiliwa wakati timu ya maofisa wa PSSSF ilipotembelea Makao Makuu ya Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) yaliyopo Kijitonyama, Dar es Salaam, ambapo pande hizo zilikubaliana kuimarisha ushirikiano katika utoaji wa taarifa sahihi na uelimishaji wa umma.

Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, alisema mtandao huo wenye zaidi ya wanachama 200 nchini na Diaspora una nafasi kubwa ya kusaidia taasisi mbalimbali kuwafikia wananchi kupitia majukwaa ya kidijitali.

Msimbe alisema TBN iko tayari kutumia mtandao wake katika kuelimisha jamii kuhusu huduma na shughuli za PSSSF, huku akisisitiza umuhimu wa wanablogu kupata mafunzo ya kina kuhusu masuala ya hifadhi ya jamii ili taarifa wanazozifikisha kwa umma ziwe sahihi na zenye uelewa mpana.

Kwa upande wake, Mkuu wa Msafara wa PSSSF, Abdul Njaidi, alisema ushirikiano huo ni sehemu ya jitihada za mfuko kuimarisha uhusiano na wadau wa habari ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa elimu kwa jamii.

Njaidi alisema mapendekezo na hoja zilizowasilishwa na TBN zitafanyiwa kazi, akisisitiza kuwa PSSSF inalenga kuhakikisha wananchi wanaelewa kwa usahihi masuala ya pensheni, hifadhi ya jamii na uwekezaji unaofanywa na mfuko huo.
Naye Mdhamini wa TBN, Issa Michuzi, alisema mtandao huo una uzoefu mkubwa katika uandishi na usambazaji wa habari za kidijitali na uko tayari kushirikiana na PSSSF katika kuhakikisha elimu ya hifadhi ya jamii inawafikia wananchi kwa lugha rahisi na inayoeleweka.

Alisema TBN imejengwa kwa dhamira ya kukuza mazingira bora ya habari za kidijitali nchini, hivyo ushirikiano huo unaweza kuwa chachu ya kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala yanayogusa maisha na ustawi wao wa baadaye.
Katibu wa TBN, Rahel Pallangyo, alisema majukwaa ya wanachama wa mtandao huo yanaweza kuwa kiungo muhimu kati ya PSSSF na wananchi, hasa katika kipindi ambacho mitandao ya kidijitali imekuwa chanzo muhimu cha habari na maarifa.

Ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu hifadhi ya jamii, pensheni na fursa za uwekezaji, huku ukilenga kuwafikia wananchi wengi zaidi ndani na nje ya Tanzania.

Ujumbe wa PSSSF uliongozwa na Abdul Njaidi na kuwajumuisha Regina Kumba, Grayson Mgunda na Doreen Lyimo, huku upande wa TBN ukihudhuriwa na Mwenyekiti Beda Msimbe, Katibu Rahel Pallangyo, Mtaalamu wa Mawasiliano Cathbert Kajuna na Mdhamini Issa Michuzi.

Mkurugenzi wa Vodacom Business Nguvu Kamando (kushoto), akisalimiana na Mkurugenzi wa Programu za Afrika wa Bridge for Billions, Liliosa Mbirimi (kulia), muda mfupi baada ya kutangazwa kwa ushirikiano wa miaka mitatu kati ya Vodacom Digital Accelerator (VDA) na Bridge for Billions. Ushirikiano huo unalenga kuimarisha mfumo wa ujasiriamali nchini kwa kuwafikia zaidi ya wajasiriamali na wabunifu 1,000 na kusaidia zaidi ya biashara 40 kukua na kupanuka, ushirikiano huu ulitangazwa wakati wa Wiki ya Ubunifu Tanzania (IWTz) 2026, Septemba 3 jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Programu za Afrika wa Bridge for Billions, Liliosa Mbirimi (kulia), akizungumza wakati wa kutangazwa kwa ushirikiano wa miaka mitatu kati ya Vodacom Digital Accelerator (VDA) na kampuni hiyo unaolenga kuimarisha mfumo wa ujasiriamali nchini kwa kuwafikia zaidi ya wajasiriamali na wabunifu 1,000 na kusaidia zaidi ya biashara 40 kukua na kupanuka. Ushirikiano huo ulitangazwa wakati wa Wiki ya Ubunifu Tanzania (IWTz) 2026, Septemba 3 jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa Vodacom Business Nguvu Kamando.

Mkurugenzi wa Programu za Afrika wa Bridge for Billions, Liliosa Mbirimi (kulia) akifafanua kuhusu ushirikiano mpya wa miaka mitatu kati ya Vodacom Digital Accelerator (VDA) na kampuni hiyo unaolenga kuimarisha mfumo wa ujasiriamali nchini kwa kuwafikia zaidi ya wajasiriamali na wabunifu 1,000 na kusaidia zaidi ya biashara 40 kukua na kupanuka. Ushirikiano huo ulitangazwa wakati wa Wiki ya Ubunifu Tanzania (IWTz) 2026, Septemba 3 jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa Vodacom Business Nguvu Kamando.

Baadhi ya washiriki na wabunifu wakifuatilia uzinduzi wa ushirikiano wa miaka mitatu kati ya Vodacom Digital Accelerator (VDA) na Bridge for Billions unaolenga kuimarisha mfumo wa ujasiriamali nchini uliotangazwa wakati wa Wiki ya Ubunifu Tanzania (IWTz) 2026, Septemba 3 jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Vodacom Business Biashara Nguvu Kamando, akizungumza wakati wa kutangazwa kwa ushirikiano mpya wa miaka mitatu kati ya Vodacom Digital Accelerator (VDA) na Bridge for Billions, unaolenga kuimarisha mfumo wa ujasiriamali nchini na kuwawezesha wajasiriamali na wabunifu kukua. Ushirikiano huo ulitangazwa wakati wa Wiki ya Ubunifu Tanzania (IWTz) 2026, Septemba 3 jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa Programu za Afrika wa Bridge for Billions, Liliosa Mbirimi.

Na Mwandishi Wetu.

● Ushirikiano huu kupitia taasisi zinazosaidia wajasiriamali vyuoni unalenga kuwafikia zaidi ya wajasiriamali 1,000 na kusaidia biashara zaidi ya 40 kukua na kupanuka

Dar es Salaam, Septemba 4, 2026: Vodacom Tanzania Plc leo imetangaza kuingia katika ubia wa miaka mitatu na Bridge for Billions, mtandao wa kimataifa wa ujasiriamali, kwa lengo la kupanua wigo na kuongeza matokeo ya mpango wa Vodacom Digital Accelerator (VDA).

Katika kipindi cha miaka mitatu ya ubia huo, mashirika hayo mawili yatazijengea uwezo na kuziwezesha taasisi zinazosaidia wajasiriamali (ESOs) kote nchini Tanzania na hivyo kuwafikia zaidi ya wajasiriamali 1,000 na kusaidia biashara zaidi ya 40 kukua na kupanuka.

Ushirikiano huu unaashiria mabadiliko katika namna VDA inavyotekeleza na kuongeza matokeo yake. Pamoja na kuendelea na lengo la kusaidia biashara changa moja kwa moja, mpango huu sasa utawekeza pia katika vituo vya kulea na kukuza biashara, vituo vya ujasiriamali, vyuo vikuu na mashirika ya maendeleo ya biashara yanayowasaidia waanzilishi wa biashara kila siku. Hatua hii inalenga kuimarisha mifumo ambayo wajasiriamali nchini Tanzania wanaihitaji hata baada ya kumalizika kwa programu ya kundi fulani la washiriki.

Kupitia makubaliano hayo, Bridge for Billions italeta nchini utaalamu wake katika programu za kulea na kukuza biashara changa (incubation), teknolojia za kidijitali na uzoefu wa kujenga uwezo wa taasisi zinazosaidia wajasiriamali. Taasisi zitakazochaguliwa zitapatiwa mafunzo maalumu, zitawezeshwa kutumia zana na mifumo ya Bridge for Billions, pamoja na kupata msaada katika kubuni programu na kuziendesha.

Aidha, taasisi hizo zitaunganishwa na mtandao wa kimataifa wa washauri na taasisi zinazosaidia wajasiriamali, hivyo kuwawezesha kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujenga mahusiano na taasisi nyingine.

Wajasiriamali watakaopatikana kupitia taasisi hizo watapitia mchakato maalumu wa kulea na kukuza biashara zao, huku biashara zitakazoonesha uwezo mkubwa wa kukua zikiendelea kwenye hatua ya acceleration, ambapo zitapatiwa msaada wa kina zaidi katika kukuza biashara na kujiandaa kwa fursa za uwekezaji.

Tangu kuzinduliwa kwake mwaka 2019, Vodacom Digital Accelerator imekuwa ikiunga mkono biashara changa na zinazokua zinazotumia teknolojia kutengeneza bidhaa na huduma zenye uwezo wa kukua, katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, kilimo, elimu na huduma za kifedha.

Kupitia awamu mbalimbali, programu hiyo imewapatia wajasiriamali mafunzo, ushauri wa kitaalamu, teknolojia, fursa za kuunganishwa na wawekezaji, pamoja na fursa za kufikia mitandao na washirika wa Vodacom.Ubia huu wa miaka mitatu unaendeleza safari ya VDA kutoka kwenye programu zinazotekelezwa kwa awamu moja baada ya nyingine hadi kwenye uwekezaji wa muda mrefu katika kuimarisha mfumo wa ujasiriamali nchini.

Kundi la kwanza la taasisi zitakazoshiriki katika mpango huu linatarajiwa kutangazwa Oktoba 2026, huku maombi kwa wajasiriamali yakitarajiwa kufunguliwa mwishoni mwa Septemba 2026.
Benki ya Exim Tanzania imehitimisha mafunzo kwa wanawake wajasiriamali 50 waliofanikiwa kukamilisha programu ya wiki sita ya Women Empowerment Programme (WEP) 2026 jijini Dar es Salaam.

Utekelezaji wa programu hii kupitia mpango wao wa kurudisha kwa jamii wa Exim Cares unalenga kuwajengea wanawake wajasiriamali maarifa na ujuzi kwa vitendo na kuimarisha biashara zao, ikiwemo usimamizi wa fedha, uandaaji wa bajeti, kuwafahamu wateja wao, kutambua fursa za soko na kupanga mikakati ya ukuaji endelevu wa biashara.
Programu hii haiishii kwenye mafunzo pekee. Wahitimu wanaunganishwa na fursa, mitandao ya masoko pamoja na huduma za kifedha zinazoweza kuwasaidia kuchukua hatua inayofuata katika safari zao za biashara.

Wakati wakiwapongeza wanawake hao 50, Benki ya Exim inaendelea kutarajia kuona biashara zao zikikua, zikitoa fursa kwa wengine na kuleta matokeo chanya katika familia na jamii zinazowazunguka.

 Na Mwandishi Wetu.

 Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imekutana na kufanya mazungumzo na watangazaji na waandaaji wa kipindi cha Good Morning kinachorushwa na Wasafi FM, ambapo imewakumbusha umuhimu wa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya uandishi wa habari katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Kikao hicho kimefanyika leo, Septemba 2, 2026, katika Makao Makuu ya JAB, Mtaa wa Jamhuri, jijini Dar es Salaam, kikilenga kuimarisha uelewa wa watangazaji hao kuhusu misingi ya weledi, uwajibikaji na matumizi sahihi ya majukwaa ya habari.

Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, amefafanua matakwa ya Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229; Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta, Sura ya 306; pamoja na kanuni zake zinazopaswa kuzingatiwa katika utayarishaji na utangazaji wa maudhui.

Wakili Kipangula ameeleza kuwa kuzingatia sheria na maadili ni msingi wa kulinda heshima ya taaluma, haki za watu wanaohusika katika maudhui na imani ya jamii kwa Waandishi wa Habari.
Baada ya mazungumzo hayo, watangazaji wakongwe Gelard Hando na Hilary Mtuta, maarufu kama Zembwela, walikabidhiwa vitambulisho vyao vya ithibati ya uandishi wa habari baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari.

Makabidhiano hayo yamekamilisha hatua ya kuwatambulisha rasmi kama Waandishi wa Habari wenye ithibati, wenye wajibu wa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, maadili na uwajibikaji.