
Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini makubaliano hayo, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi na wa kati wa Benki ya Exim Tanzania Bw. Andrew Lyimo, alisema ushirikiano huo unaakisi dhamira ya Benki hiyo ya kutoa huduma za kifedha zinazokwenda sambamba na mahitaji halisi ya wafanyabiashara.
“Kwa biashara nyingi, gari la biashara ni zaidi ya chombo cha usafiri; ni mali inayosaidia shughuli za kila siku na kuweka mazingira ya biashara kukua. Kupitia ushirikiano huu, biashara zinazokidhi vigezo zinaweza kupata magari mapya bila kutumia mtaji wao wote kwa wakati mmoja. Hii inawawezesha kubaki na fedha kwa ajili ya mahitaji mengine ya biashara huku wakirejesha ufadhili huo kwa muda waliokubaliana.”
“Kwa hiyo, tunawakaribisha wafanyabiashara wanaotaka kuongeza idadi ya magari yao, kuimarisha shughuli zao au kutumia fursa mpya za ukuaji wa biashara kuwasiliana nasi na kupata maelezo zaidi kuhusu huduma za ufadhili zinazopatikana,” aliongeza.
Ushirikiano huo pia unatarajiwa kuimarisha huduma za Benki ya Exim kwa wafanyabiashara, hasa biashara ndogo na za kati pamoja na kampuni, kwa kuongeza fursa za kupata huduma nyingine za kifedha zinazohusiana na uendeshaji wa biashara, ikiwemo huduma za miamala, bima na ukusanyaji wa fedha.

Akizungumzia ushirikiano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Group la Six Continental Trading Company Limited, Benson Mahinya, alisema ushirikiano huo utasaidia wafanyabiashara kupata magari pamoja na ufadhili wanaohitaji ili kuimarisha shughuli zao.
“Magari ya kuaminika ni muhimu kwa biashara zinazojihusisha na usafirishaji, usambazaji na uhamishaji wa bidhaa. Kupitia ushirikiano wetu na Benki ya Exim, tunaunganisha huduma zetu za magari ya biashara na ufadhili unaoweza kuwasaidia wafanyabiashara kupata magari mapya na kuongeza uwezo unaohitajika ili biashara zao zikue.”
Kifurushi hicho cha ufadhili pia kinajumuisha bima ya gari pamoja na bima ya maisha kwa mkopo, hatua inayowapa wateja ulinzi wa ziada katika kipindi cha marejesho.
Kupitia ushirikiano huo, Benki ya Exim na Six Continental zinalenga kuwawezesha wafanyabiashara kupata magari mapya ya biashara, kuongeza idadi ya magari yao na kuimarisha uwezo wa kusafirisha bidhaa na kuwahudumia wateja katika masoko yanayokua nchini Tanzania na katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.





Toa Maoni Yako:
0 comments: