Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akishiriki Mkutano wa 17 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Hifadhi ya Bioanuai unaoendelea jijini Yerevan, Armenia, Oktoba 27, 2026.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (kulia) akielezea jambo wakati wa Mkutano wa 17 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Hifadhi ya Bioanuai unaoendelea jijini Yerevan, Armenia, Oktoba 27, 2026. Wengine katika picha ni Naibu Katibu Mkuu (Mazingira), Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Maduhu Kazi, Mkurugenzi Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Bi. Farhat Mbarouk na Mkurugenzi Msaidizi (Sehemu ya Hifadhi ya Bioanuai) Ofisi ya Makamu wa Rais wa Dkt. Paul Deogratius.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (kushoto) akimsikiliza Naibu Katibu Mkuu (Mazingira), Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Maduhu Kazi, wakati wa Mkutano wa 17 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Hifadhi ya Bioanuai unaoendelea jijini Yerevan, Armenia, Oktoba 27, 2026. Aliyesimama kulia ni Mkurugenzi Msaidizi (Sehemu ya Hifadhi ya Bioanuai) Ofisi ya Makamu wa Rais wa Dkt. Paul Deogratius.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (kushoto) akimsikiliza Naibu Katibu Mkuu (Mazingira), Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Maduhu Kazi, wakati wa Mkutano wa 17 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Hifadhi ya Bioanuai unaoendelea jijini Yerevan, Armenia, Oktoba 27, 2026. Wengine waliosimama kulia ni Mkurugenzi Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Bi. Farhat Mbarouk na Mkurugenzi Msaidizi (Sehemu ya Hifadhi ya Bioanuai) Ofisi ya Makamu wa Rais wa Dkt. Paul Deogratius.

Na Mwandishi Wetu.

Tanzania imesisitiza umuhimu wa kuimarisha utekelezaji wa vitendo wa ajenda ya dunia ya hifadhi ya bioanuai, ikieleza kuwa upatikanaji wa fedha za uhakika, kuimarishwa kwa uwezo wa kitaasisi na ushirikiano wa kimataifa ni nguzo muhimu katika kufikia malengo ya uhifadhi na maendeleo endelevu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamadi Yussuf Masauni amesema hayo wakati wa Mkutano wa 17 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Bioanuai (COP17), unaofanyika Yerevan, Armenia, Oktoba 27, 2026.

Amesema Tanzania inashiriki mkutano huo ikiwa na dhamira ya kuhakikisha Mfumo wa Dunia katika kuhifadhi Bioanuai unatekelezwa kwa vitendo, kwa kuzingatia matokeo yanayopimika na manufaa ya muda mrefu kwa wananchi na dunia kwa ujumla.

Aidha, Tanzania imesisitiza umuhimu wa kuoanisha utekelezaji wa Mkakati na Mpango wa Kazi wa Taifa wa Bioanuai wa mwaka 2025–2030 (NBAP 2025–2030) na Programu ya Mageuzi ya Utunzaji wa Mazingira, ili kuchangia kufikiwa kwa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, hususan katika kuimarisha ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuboresha utunzaji wa mazingira.

Katika mkutano huo, Tanzania imeainisha maeneo kadhaa ya kipaumbele, ikiwemo suala la upatikanaji wa fedha za bioanuai. Nchi imesisitiza umuhimu wa kuongeza rasilimali za kifedha zilizo za uhakika, zinazotabirika na zinazofikika kwa urahisi, hasa kwa nchi zinazoendelea, ili kuwezesha utekelezaji wa mipango ya uhifadhi.

Tanzania pia imeeleza kuwa mageuzi ya sera na mifumo ya vivutio vinavyoweza kuchochea uharibifu wa bioanuai yanapaswa kuzingatia haki, ushahidi wa kisayansi na mazingira halisi ya wananchi. Hatua hizo zinapaswa kulinda usalama wa chakula, maisha ya wakulima na vipaumbele vya maendeleo ya jamii.

Katika eneo la utekelezaji na ufuatiliaji, Tanzania imehimiza kuimarishwa kwa uwezo wa kitaasisi, upatikanaji wa teknolojia sahihi, takwimu za bioanuai na rasilimali za kiufundi na kifedha. Hatua hizo zitasaidia nchi kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na kuhakikisha ahadi zilizowekwa katika ngazi ya kitaifa zinatafsiriwa kuwa matokeo yanayoweza kupimwa na kuthibitishwa.

Vilevile, Tanzania imesisitiza umuhimu wa kuchukua hatua shirikishi katika kulinda mifumo muhimu ya ikolojia, hususan vyanzo vya maji, pamoja na kuimarisha uratibu kati ya ajenda ya hifadhi ya bioanuai, mabadiliko ya tabianchi na mapambano dhidi ya ujangwa.

Nchi imetambua pia nafasi muhimu ya wanawake, vijana, jamii na sekta binafsi katika kusimamia rasilimali za asili na kuendeleza juhudi za uhifadhi. Kwa msingi huo, ushirikishwaji wa wadau hao unapaswa kupewa kipaumbele ili kuhakikisha hatua za uhifadhi zinakuwa jumuishi na zenye manufaa kwa wananchi.

Tanzania imeeleza utayari wake wa kuendelea kushirikiana na nchi wanachama wa Mkataba wa Bioanuai pamoja na wadau wa maendeleo katika kuhamasisha rasilimali na kuharakisha utekelezaji wa Mfumo wa Dunia wa Bioanuai.

Tanzania imetoa wito katika mkutano huo kuwa hatua muhimu ya kuimarisha utekelezaji wa ahadi za kimataifa kwa vitendo, kuoanisha dhamira za kisera na uwekezaji wa fedha na rasilimali, na kuhakikisha malengo ya kimataifa yanazaa matokeo halisi katika ngazi ya taifa.

Naye, Naibu Katibu Mkuu (Mazingira), Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Maduhu Kazi, amesema Tanzania inaamini kuwa mafanikio ya juhudi za kimataifa za hifadhi ya bioanuai yatategemea uwezo wa nchi kubadilisha ahadi kuwa hatua madhubuti, kuhakikisha rasilimali zinazohitajika zinapatikana na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kwa ajili ya kulinda mifumo ya ikolojia na ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Immaculate Semesi amesema Uhifadhi wa bioanuwai unahitaji ushirikiano wa wadau wote, uwekezaji wa kutosha na mifumo imara ya usimamizi na ufuatiliaji wa mazingira. Ni muhimu kuhakikisha kuwa rasilimali za kifedha zinazopatikana zinasaidia utekelezaji wa hatua halisi za uhifadhi, urejeshaji wa mazingira na kuboresha maisha ya wananchi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: