Michelle Kilpin, Mkurugenzi Mkuu wa TBL (wa pili kulia), na CPA Anthony Kasore, Mkurugenzi Mkuu wa VETA (wa pili kushoto), wakionyesha Hati ya Makubaliano (MoU) ya mpango wa ufadhili wa masomo wa TBL Ujuzi Kwanza, unaolenga kuwawezesha vijana kupata ujuzi kupitia mafunzo ya vitendo katika mnyororo wa thamani wa kilimo. Wengine katika picha ni Neema Temba, Mkurugenzi wa Masuala ya Kampuni na Udhibiti wa TBL (kulia), na Dkt. Abdallah Ngodu, Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi wa VETA.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
TANZANIA Breweries Public Limited Company (TBL) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), imeanzisha mpango wa ufadhili wa mafunzo ya kilimo utakaowanufaisha vijana 300 wa Kitanzania kutoka familia zenye kipato cha chini.
Mpango huo unaojulikana kama Ujuzi-Kwanza, unalenga kuwapatia vijana ujuzi wa vitendo katika uzalishaji wa mazao, matengenezo ya vifaa, ufundi wa mitambo ya kilimo na shughuli nyingine za kiufundi zinazohusiana na sekta hiyo.
Kupitia mpango huo wa miaka mitatu, TBL italipia gharama za mafunzo, huku VETA ikitoa mafunzo yanayotambulika kitaifa. Vijana watakaoshiriki pia watapata uzoefu wa vitendo katika shughuli za kilimo, ikiwemo mashamba ya wakulima wa shayiri na mtama wanaoshirikiana na TBL.
Makubaliano ya kuanzisha mpango huo yalisainiwa jijini Dar es Salaam Oktoba 28, 2026, na Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Michelle Kilpin, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Kasore alisema ushirikiano huo utasaidia kuwaandaa vijana wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya sekta ya kilimo, ambayo inaendelea kutumia teknolojia na mbinu za kisasa.
Alisema mafunzo hayo yatawapa vijana fursa ya kupata ajira, kujiajiri na kuanzisha biashara zinazohusiana na kilimo, ikiwemo huduma za matengenezo ya vifaa na mitambo ya kilimo.
“Ushirikiano huu unafungua fursa kwa vijana wenye vipaji ambao huenda wasiwe na uwezo wa kugharamia mafunzo, huku ukihakikisha kwamba ujuzi wanaoupata unakidhi mahitaji halisi ya sekta,” alisema Kasore.
Kwa upande wake, Kilpin alisema biashara ya TBL inategemea kwa kiasi kikubwa mazao yanayozalishwa na wakulima wa Tanzania, hivyo kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa kilimo kutachangia kuimarisha uzalishaji na kuongeza fursa za kiuchumi.
Alisema kampuni hiyo inalenga kuona vijana wakitumia ujuzi watakaopata kujenga taaluma, kuanzisha biashara na kujipatia kipato endelevu, huku wakichangia maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.
Kilpin aliongeza kuwa TBL imekuwa ikishirikiana na wakulima wadogo zaidi ya 2,500 wanaozalisha shayiri na mtama katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Dodoma, kwa kuwapatia mbegu, mafunzo ya kilimo na masoko ya uhakika.
Alisema kampuni hiyo pia imewekeza katika uchakataji wa shayiri nchini kupitia kiwanda cha Kilimanjaro Malting kilichopo Moshi, ambacho kilikamilisha mwaka wake wa kwanza wa uzalishaji kamili mwaka 2025 kikitumia shayiri iliyolimwa nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kuhusu mpango huo, kilimo kilichangia asilimia 26.3 ya pato la taifa mwaka 2024 na kinaajiri zaidi ya nusu ya watu wote wanaofanya kazi nchini, hali inayoonesha umuhimu wa kuongeza ujuzi na tija katika sekta hiyo.
Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa zaidi ya vijana 800,000 huingia katika soko la ajira nchini kila mwaka, hivyo mafunzo ya ufundi stadi yanayolenga mahitaji ya soko yanaweza kuongeza fursa za ajira na kujiajiri.
Kasore alisema idadi ya wanafunzi waliojiunga na mafunzo ya VETA imeongezeka kutoka 69,347 mwaka wa masomo 2022/23 hadi 116,468 mwaka 2025/26, huku vyuo vipya 65 vikitarajiwa kufunguliwa Januari 2027.
Alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya taasisi za mafunzo na sekta binafsi ni muhimu katika kuhakikisha vijana wanapata ujuzi unaoweza kutumika moja kwa moja katika shughuli za uzalishaji.
Mpango wa Ujuzi-Kwanza unaendana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050, inayolenga kukuza nguvu kazi yenye ujuzi, kuimarisha kilimo na kujenga uchumi jumuishi. Pia unaunga mkono ajenda ya kukuza sekta ya kilimo na programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora inayohamasisha vijana kushiriki katika biashara za kilimo.









Toa Maoni Yako:
0 comments: