Afisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom Tanzania PLC, Philip Besiimire (kushoto), akikabidhi tuzo ya pongezi kwa mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo, ikiwa ni sehemu ya kutambua na kuthamini mchango wake katika utoaji wa huduma kwa wateja. Hafla hiyo ilifanyika wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026, yaliyolenga kuhamasisha utamaduni wa kuweka wateja mbele na kuthamini juhudi za wafanyakazi wanaotekeleza dhamira hiyo kila siku. Pembeni ni Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Vodacom Tanzania, Herriet Lwakatare.
Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Vodacom Tanzania, Herriet Lwakatare, akizungumza na waandishi wa habari wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026 iliyowakutanisha wafanyakazi wa kampuni hiyo. Katika maadhimisho hayo, Vodacom iliangazia dhamira yake ya kuwaweka wateja mbele kwa kuhakikisha wanapata huduma bora, huku usalama wa fedha na taarifa zao binafsi ukipewa kipaumbele. Kampuni hio imesisitiza umuhimu wa kuendeleza mwingiliano wa kibinadamu katika huduma kwa wateja licha ya kuongezeka kwa matumizi ya Akili Unde (AI), mifumo ya kiotomatiki na roboti kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuboresha shughuli za biashara.
Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Vodacom Tanzania, Herriet Lwakatare, akizungumza na wafanyakazi wa kampuni hiyo wakati wa hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026. Katika hotuba yake, alisisitiza umuhimu wa kuweka mahitaji ya wateja mbele kwa kuwasikiliza, kuwapatia majibu kwa wakati na kuhakikisha wanapata huduma salama na zenye ubora. Maadhimisho hayo yalitoa nafasi kwa wafanyakazi kutafakari mchango wao katika kujenga imani ya wateja na kuhakikisha kila mawasiliano na mteja yanaacha uzoefu mzuri.
Baadhi ya wafanyakazi wa Vodacom Tanzania ikiongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Philip Besiimire (katikati), ikiwa katika picha ya pamoja wakati wa hafla ya kuhitimisha maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026. Hafla hiyo iliwaunganisha wafanyakazi katika kusherehekea mafanikio, kutambua juhudi za waliotoa huduma bora na kuimarisha dhamira ya kampuni ya kuwaweka wateja mbele. Kupitia maadhimisho hayo, Vodacom ilisisitiza kuwa huduma bora si kutoa majibu ya haraka pekee, bali pia ni kujenga imani ya wateja, kulinda taarifa zao na kuhakikisha wanapata msaada wanaouhitaji kila wanapowasiliana na kampuni.Na Mwandishi Wetu
Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania imesisitiza umuhimu wa kudumisha mwingiliano wa kibinadamu katika huduma kwa wateja licha ya kuongezeka kwa matumizi ya akili Unde (AI), mifumo ya kiotomatiki na roboti kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuboresha shughuli za biashara.
Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Vodacom Tanzania, Herriet lwakatare, alisema hayo wakati wa hafla ya utoaji tuzo kwa wafanyakazi wa huduma kwa wateja iliyofanyika kuhitimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja.
Hali hii inajiri wakati ambapo kampuni mbalimbali zinazidi kutumia akili mnemba na mifumo ya kiotomatiki kurahisisha shughuli, kupunguza kazi zinazojirudia na kukidhi mabadiliko ya matarajio ya wateja. Hali hiyo inaziweka kampuni za mawasiliano katika changamoto ya kusawazisha ufanisi unaotokana na teknolojia na utoaji wa huduma zinazozingatia mahitaji binafsi ya wateja.Bi. Harriet Lwakatare, alisema maendeleo ya teknolojia yanabadilisha namna kampuni zinavyowahudumia wateja, lakini watu bado wana nafasi ya msingi katika utoaji wa huduma.
“Sekta yetu inabadilika. Akili Unde na mifumo ya kiotomatiki inazidi kuwa sehemu ya shughuli zetu za kila siku, lakini jambo moja linabaki kuwa muhimu, nalo ni uhusiano wa kibinadamu,” alisema Bi. Lwakatare wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo za wiki ya huduma kwa wateja ya kampuni hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki.
Kauli yake inatolewa wakati ambapo kampuni katika sekta mbalimbali zinazidi kuwekeza katika zana za kidijitali, mifumo ya kiotomatiki na mifumo inayotumia takwimu ili kuboresha uzoefu wa wateja, kupunguza gharama za uendeshaji na kujibu mahitaji ya watumiaji kwa haraka zaidi.
Kadri uchumi wa kidijitali nchini Tanzania unavyoendelea kukua, kampuni zinatarajiwa kuongeza uwekezaji katika akili mnemba na mifumo ya kiotomatiki. Hata hivyo, wataalamu wanaeleza kuwa teknolojia inatarajiwa kusaidia na kukamilisha ujuzi wa binadamu badala ya kuuchukua nafasi yake, hasa katika sekta zinazohitaji uaminifu, uelewa wa hisia za wateja na huduma zinazozingatia mahitaji yao binafsi.
Kwa kampuni za mawasiliano, kusawazisha ubunifu wa kidijitali na kudumisha uhusiano imara na wateja kunazidi kuwa jambo muhimu katika kuwabakiza wateja na kukuza biashara kwa muda mrefu.
Meneja wa Uendeshaji wa Rejareja wa Vodacom Tanzania, Bi. Vanessa Mlawi, aliunga mkono msimamo huo akisema matumizi ya akili Unde yanaweza kuongeza ufanisi mahali pa kazi huku yakienda sambamba na kudumisha uhusiano wa kibinadamu.
Alisema kampuni zinapaswa kuendelea kutumia akili Unde kutokana na uwezo wake wa kuboresha shughuli za biashara, lakini akasisitiza kuwa teknolojia haiwezi kuchukua nafasi ya mguso wa kibinadamu katika huduma.
Kwa upande wake, Bw. Padili James, mtaalamu wa mikakati ya maudhui, alisema huduma za intaneti za kuaminika zimekuwa muhimu zaidi katika kazi zake kama mtayarishaji wa maudhui na mjasiriamali. Alisema huduma hizo zinamwezesha kupata taarifa, kujifunza ujuzi mpya na kupanua wigo wa shughuli zake.
Wakati huo huo, katika hotuba iliyotolewa kwa wafanyakazi, uongozi wa huduma kwa wateja ulisisitiza kuwa mafanikio ya huduma bora yanategemea pia namna wateja wanavyopokelewa, kusikilizwa na kuhudumiwa.
Uongozi huo ulisema matumizi ya teknolojia yanapaswa kuwawezesha wafanyakazi kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kuwapa nafasi ya kuzingatia mahitaji ya wateja, badala ya kuchukua nafasi yao.





Toa Maoni Yako:
0 comments: