Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Vodacom Tanzania PLC, Harriet Lwakatare (kulia), akizungumza na wateja wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja katika Duka la Vodacom jijini Dar es Salaam. Maadhimisho hayo yalilenga kuwathamini wateja na kuhamasisha matumizi salama ya huduma za simu, ikiwemo kutumia njia rasmi za Vodacom na kuripoti vitendo vya kutiliwa shaka kupitia Huduma kwa Wateja kwa namba 100. Kushoto ni Mkurugenzi wa Biashara wa Vodacom Tanzania. Tukio hilo lilifanyika Oktoba 5, 2026.
Mkurugenzi wa TEHAMA wa Vodacom Tanzania PLC, Athumani Mlinga (kulia), akizungumza na kumkabidhi zawadi mteja wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja katika Duka la Vodacom jijini Dar es Salaam. Maadhimisho hayo yalilenga kuwathamini wateja na kuwakumbusha umuhimu wa usalama wanapotumia huduma za simu, ikiwemo kutumia njia rasmi za Vodacom na kuripoti vitendo vya kutiliwa shaka kupitia Huduma kwa Wateja kwa namba 100. Tukio hilo lilifanyika Oktoba 5, 2026.
Brigita Shirima (kushoto), Mkurugenzi wa Biashara na Masoko wa Vodacom Tanzania PLC, akimkabidhi zawadi mteja wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja katika kituo cha huduma cha Vodacom. Maadhimisho hayo yalilenga kuwathamini wateja na kuimarisha uzoefu wao wa huduma. Tukio hilo lilifanyika tarehe 5 Oktoba jijini Dar es Salaam.

Harriet Lwakatare (katikati), Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Vodacom Tanzania PLC, akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Vodacom wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja. Maadhimisho hayo yalilenga kuimarisha huduma kwa wateja na kuhamasisha wafanyakazi kuendelea kutoa huduma bora. Tukio hilo lilifanyika tarehe 5 Oktoba jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu.

Dar es Salaam – Tanzania, 5 Oktoba 2026: Mteja anapokabidhi fedha zake, anaposhirikisha taarifa zake binafsi na hata anapopiga simu kuomba msaada, matarajio yake ni zaidi ya kupata jibu la haraka. Anatarajia pia kuwa salama.

Hili ndilo jambo ambalo Vodacom Tanzania imelipa kipaumbele katika Wiki ya Huduma kwa Wateja ya mwaka 2026, inayoanza Oktoba 5 hadi 9, kwa kuwapa wateja nafasi ya kufahamu kwa karibu zaidi hatua zinazochukuliwa kuwalinda wao, fedha zao na taarifa zao binafsi, pamoja na mambo wanayoweza kufanya ili kujilinda.

Takwimu zinaonesha kwa nini suala hili ni muhimu. Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hadi Juni 2026 kulikuwa na akaunti milioni 87 za huduma za fedha kwa njia ya simu nchini. Katika kipindi hichohicho, TCRA ilirekodi jumla ya majaribio 7,334 ya udanganyifu. Ingawa idadi hiyo ilipungua kwa asilimia 25.29 ikilinganishwa na robo iliyotangulia, bado inaonesha kuwa udanganyifu ni changamoto ambayo watumiaji wa huduma za simu wanahitaji kuwa makini nayo.

Kwa Vodacom Tanzania ambayo inatawala soko huduma simu nchini, usalama wa mteja unaanzia kwenye kuhakikisha kuwa mtu sahihi ndiye anayepata huduma kwenye akaunti husika. Usajili wa laini za simu unahusisha uthibitishaji wa alama za vidole dhidi ya taarifa za NIDA, na utaratibu huohuo hutumika wakati wa kubadilisha laini za simu. Mabadiliko ya laini za simu hayawezi kufanyika kwa niaba ya mtu mwingine.

“Wateja wetu wanatuamini na kutukabidhi sehemu muhimu za maisha yao ya kila siku, ikiwemo fedha zao na taarifa zao binafsi. Imani hiyo inakuja na wajibu wa kuhakikisha wateja wetu wako salama. Wiki ya Huduma kwa Wateja inatupa nafasi ya kuwaonesha hatua tunazochukua kuwalinda, lakini pia kuwakumbusha kuwa nao wana nafasi kubwa katika kujilinda,” alisema Mkurugenzi wa Kitengo cha Shughuli za Huduma kwa Wateja kutoka Vodacom Tanzania PLC, Harriet Lwakatare. Utaratibu huo unaendelea pia pale mteja anapowasiliana na Huduma kwa Wateja. Kabla ya kusaidiwa, mteja huthibitishwa kuwa ndiye mmiliki wa akaunti. Wakati huohuo, Vodacom inaendelea kuwakumbusha wateja jambo moja muhimu kuhusu usalama wa fedha zao: usiwahi kumpa mtu yeyote namba yako ya siri ya M-PESA, hata kama anajitambulisha kuwa ni mfanyakazi wa Vodacom.

Na pale mteja anapohisi kuwa kuna kitu hakiko sawa, kutoa taarifa mapema kunaweza kusaidia.

Timu ya Vodacom Tanzania inayoshughulikia masuala ya udanganyifu hushirikiana na wateja kufuatilia namba za simu au barua pepe zinazohusishwa na tukio lililoripotiwa. Pale inapohitajika, timu hiyo pia hushirikiana na Jeshi la Polisi katika uchunguzi na hatua za kisheria. Kwa sababu hiyo, wateja wanahimizwa kutoa taarifa haraka wanapohisi wamekutana na tukio la udanganyifu, badala ya kusubiri.

Hatua za kupata msaada zimerahisishwa. Wateja wanaweza kuwasiliana na Huduma kwa Wateja ya Vodacom kwa kupiga 100 au 101, kutuma ujumbe WhatsApp kupitia +255 754 100 100, kutuma barua pepe customercare@vodacom.co.tz, au kufika katika duka la Vodacom au dawati la Huduma kwa Wateja.

Kwa wateja wanaopendelea kujihudumia wenyewe, App ya My Vodacom inawawezesha kupata huduma mbalimbali bila kutumia data. Wateja pia wanaweza kutumia huduma ya kufungua PIN ya M-PESA kila siku.

Vodacom Tanzania inawahimiza wateja kufanya usalama kuwa sehemu ya matumizi yao ya kila siku ya simu: kutumia njia rasmi za Vodacom, kuhakikisha wanajua wanayewasiliana naye kabla ya kutoa taarifa au kutuma fedha, na kuripoti mara moja jambo lolote la kutiliwa shaka kupitia Huduma kwa Wateja kwa namba 100.

Wateja pia wanaweza kuangalia namba za simu zilizosajiliwa kwa kutumia kitambulisho chao cha NIDA, hatua inayowasaidia kufahamu namba zote zinazohusishwa na utambulisho wao.

Wiki ya Huduma kwa Wateja huadhimishwa duniani kote katika wiki ya kwanza kamili ya mwezi Oktoba. Katika maadhimisho ya mwaka huu, Vodacom Tanzania itaendelea kutumia vyombo vya habari na mitandao yake ya kijamii kuwafikishia wateja taarifa muhimu kuhusu usalama, namna ya kupata msaada na hatua wanazoweza kuchukua kujilinda.

Kwa sababu huduma nzuri kwa mteja si kuwa tu tayari kusaidia pale tatizo linapotokea. Ni pia kumsaidia mteja kujua namna ya kujilinda kabla tatizo halijatokea.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: