Na Mwandishi We
tu.
 
Dar es Salaam, Novemba 19, 2026: Jitihada za Tanzania kuongeza manufaa ya kiuchumi yatokanayo na rasilimali za madini zinafungua fursa mbalimbali katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta hiyo, kuanzia uchimbaji na uchakataji hadi uzalishaji viwandani na huduma saidizi. Hata hivyo, ili kutumia fursa hizo kikamilifu, kunahitajika uwekezaji, upatikanaji wa mitaji na ushirikiano imara utakaowezesha rasilimali za madini kuchochea maendeleo ya viwanda na ukuaji endelevu wa uchumi.

Katika kuunga mkono juhudi hizo, Benki ya Exim Tanzania imeshiriki katika Mkutano wa Saba wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania (Tanzania Mining and Investment Conference – TMIC 2026), ikiwa miongoni mwa wadhamini wa mkutano huo. Kupitia ushiriki wake, Benki inaendeleza ushirikiano na wadau mbalimbali katika kukuza uwekezaji na kuongeza thamani ya madini nchini.

Mkutano huo wa siku tatu, ulifanyika kuanzia Novemba 19 hadi 21 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, unawakutanisha viongozi wa Serikali, wawekezaji, kampuni za uchimbaji madini na taasisi za fedha kujadili fursa za uwekezaji, mahitaji ya kifedha, teknolojia na ushirikiano unaoweza kuharakisha maendeleo ya sekta ya madini nchini.

Kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu, ‘Madini Yaliyoongezwa Thamani: Chachu ya Ukuaji wa Viwanda na Uchumi,’ Kauli mbiu hii inaakisi azma ya Tanzania ya kupanua shughuli za uchakataji wa madini nchini, kuimarisha viwanda vinavyotumia madini kama malighafi na kuongeza manufaa ya kiuchumi yatokanayo na rasilimali hizo. Ajenda ya mkutano pia inasisitiza umuhimu wa upatikanaji wa mitaji na ubia wa kimkakati katika kufanikisha azma hiyo. 

 


Ushiriki wa Benki ya Exim Tanzania katika mkutano huo unaakisi dhamira yake pana ya kusaidia biashara na uwekezaji katika mnyororo mzima wa thamani wa madini. Benki inatambua kuwa ukuaji wa sekta hiyo hauishii kwenye uchimbaji pekee, bali unahusisha pia uchakataji wa madini, usambazaji wa vifaa na mitambo, ukandarasi, usafirishaji na biashara nyingine zinazotoa huduma kwa sekta hiyo.

Dhamira hiyo inadhihirishwa pia na hatua za Benki kuimarisha uwepo wake mkoani Geita, mojawapo ya maeneo muhimu ya uchimbaji madini nchini. Mwezi Mei 2026, Exim Bank ilifungua tawi jipya mkoani humo ili kusogeza huduma zake za kifedha karibu na wachimbaji madini, wafanyabiashara, wajasiriamali na wadau wengine wa shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.

Kupitia huduma ya Ufadhili wa Miradi (Project Finance), Benki ya Exim Tanzania hutoa ufadhili kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa katika sekta mbalimbali. Uwezo wake katika eneo hili unatokana na uelewa wa kina wa mazingira ya biashara nchini na mifumo ya udhibiti, pamoja na uhusiano imara ambao Benki imejenga na taasisi za fedha za maendeleo.

Mbali na ufadhili wa miradi, Benki ya Exim hutoa huduma mbalimbali za kibenki kwa biashara, zikiwemo mikopo ya mtaji wa uendeshaji, mikopo ya muda mfupi na mikopo ya muda maalumu, ufadhili wa pamoja wa mikopo, huduma ya punguzo la ankara, huduma za fedha za biashara, huduma za kibenki za kidijitali na usimamizi wa fedha. Huduma hizi zimekusudiwa kusaidia biashara zinazohusika katika mnyororo wa thamani wa madini kusimamia mtiririko wa fedha, kugharamia shughuli za uendeshaji na kutekeleza mipango ya kukuza na kupanua biashara zao.

Katika siku ya ufunguzi wa mkutano huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim Tanzania, Jaffari Matundu, aliongoza ujumbe wa viongozi waandamizi na wataalamu kutoka vitengo mbalimbali vya Benki, ushriki wao ni kielelezo cha dhamira ya Benki ya kuimarisha ushirikiano na wadau wa sekta hiyo, kujadiliana nao na kubaini fursa zinazoweza kuchochea uwekezaji katika sekta ya madini.

Akizungumzia ushiriki wa benki ya Exim Tanzania katika mkutano huo, Matundu alisema: “Fursa katika sekta ya madini nchini haziishii kwenye shughuli za uchimbaji pekee, bali zinajumuisha pia biashara zinazohusika katika mnyororo mzima wa thamani, kuanzia uchakataji na usambazaji wa vifaa hadi usafirishaji na huduma nyingine za ndani. Benki yetu inalenga kujenga ushirikiano imara na kutoa suluhisho za kifedha zinazokidhi mahitaji ya biashara. Kwa kufanya hivyo, tunaziwezesha biashara kukua, tunachochea maendeleo ya viwanda na kusaidia Tanzania kupata manufaa makubwa zaidi ya kiuchumi kutokana na rasilimali zake za madini”.

Kupitia udhamini na ushiriki wake katika mkutano wa TMIC 2026, Exim Bank imeonyesha kuendelea kuunga mkono azma ya Tanzania ya kukuza uwekezaji na kuongeza manufaa yatokanayo na rasilimali zake, huku ikichangia ukuaji wa muda mrefu na endelevu wa sekta ya madini nchini.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: