Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetoa maelekezo kwa wapiga kura watakaoshiriki Uchaguzi Mdogo wa Ubunge Jimbo la Chamwino na Udiwani katika kata 11 za Tanzania Bara, ikiwataka kuzingatia taratibu za uchaguzi ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa amani na utulivu.
Miongoni mwa maelekezo yaliyotolewa ni kuruhusu baadhi ya wapiga kura kupiga kura hata kama hawana kadi zao, kadi zimeharibika au kuna tofauti ya namba ya mpiga kura, mradi taarifa zao zinathibitishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufaa Jacobs C. M. Mwambegele, amesema mpiga kura aliyepoteza kadi au kadi yake kuharibika anaweza kutumia kitambulisho cha Taifa (NIDA), leseni ya udereva au hati ya kusafiria, iwapo majina yake yanafanana na yale yaliyopo katika daftari la wapiga kura.
Aidha, amesema mpiga kura ambaye hana picha katika daftari lakini ana kadi yenye taarifa binafsi zinazolingana na zilizopo kwenye daftari, anaruhusiwa kupiga kura. Hali kadhalika, mpiga kura ambaye namba ya kadi yake inatofautiana na ile iliyopo kwenye daftari, lakini taarifa nyingine zikiwemo picha na majina zinafanana, ataruhusiwa kushiriki uchaguzi.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa mtu ambaye ana kadi ya mpiga kura lakini taarifa zake hazipo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura hataruhusiwa kupiga kura.
Jaji Mwambegele ametoa maelekezo hayo wakati akizungumza kuhusu maandalizi ya uchaguzi mdogo unaofanyika leo Novemba 4, 2026, ambapo jumla ya wapiga kura 213,024 wanatarajiwa kushiriki.
Amesema kati ya hao, wapiga kura 133,864 wameandikishwa katika Jimbo la Chamwino, huku 79,160 wakiwa katika kata 11 zinazofanya uchaguzi wa udiwani.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, uchaguzi huo utasimamiwa katika vituo 665, vikiwemo 441 vya Jimbo la Chamwino na 224 katika kata 11.
Katika uchaguzi huo, jumla ya wagombea 67 kutoka vyama 17 vya siasa wanawania nafasi za ubunge na udiwani. Jimbo la Chamwino lina wagombea 16 wa ubunge, wakiwemo wanaume wanane na wanawake wanane.
Kwa upande wa udiwani, wagombea 51 wanawania nafasi hizo katika kata 11, ambapo wanaume ni 43 sawa na asilimia 84.31, huku wanawake wakiwa wanane sawa na asilimia 15.69.
Jaji Mwambegele amevikumbusha vyama vya siasa kuhakikisha vinaweka mawakala katika vituo vya kupigia, kuhesabia na kujumlishia kura ili kulinda maslahi ya wagombea wao na kufuatilia mchakato mzima wa uchaguzi kwa mujibu wa sheria na kanuni.
Amesema vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni. Hata hivyo, wapiga kura watakaokuwa kwenye foleni wakati wa kufungwa kwa vituo wataruhusiwa kuendelea kupiga kura hadi wote watakapomaliza.
Aidha, amewataka wapiga kura kwenda katika vituo walivyojiandikisha wakiwa na kadi zao, huku akisisitiza umuhimu wa kutoa kipaumbele kwa wazee, wagonjwa, watu wenye ulemavu, wajawazito na wanawake wenye watoto wachanga.
Amesema watu wenye mahitaji maalumu wanaruhusiwa kwenda vituoni wakiwa na wasaidizi wao, huku wapiga kura wakitakiwa kuondoka katika eneo la kituo mara baada ya kukamilisha zoezi la kupiga kura.
Mwenyekiti huyo ametoa wito kwa wananchi wote katika maeneo yanayofanya uchaguzi kujitokeza kwa wingi na kutumia haki yao ya kidemokrasia kuwachagua viongozi wanaowataka.



Toa Maoni Yako:
0 comments: