Mahakama Kuu ya Tanzania imemhukumu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, kifungo cha miaka minne jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la uchochezi.
Hukumu hiyo imetolewa leo, Novemba 6, 2026, na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru. Mahakama pia imemweleza kuwa ana haki ya kukata rufaa.
Awali, akizungumza kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Lissu alisisitiza kuwa haombi msamaha kwa sababu anaamini hana hatia. Alipinga kutiwa hatiani kwa uchochezi, akisema shtaka alilokuwa akikabiliwa nalo lilikuwa la uhaini.
Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025, baada ya kuhutubia mkutano wa hadhara wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma. Baadaye alisafirishwa kwenda Dar es Salaam na kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Aprili 10, 2025, ambako alisomewa shtaka la uhaini.
Hadi leo, amekuwa kizuizini kwa takribani mwaka mmoja na miezi saba akisubiri kukamilika kwa kesi yake. Akizungumza mahakamani kabla ya kupewa adhabu, Lissu amesema leo ni siku yake ya 577 akiwa mahabusu.
MAHAKAMA YAMTIA HATIANI LISSU KWA KOSA LA UCHOCHEZI, JAMHURI YAOMBA ADHABU KALI
Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
Jaji Dustan Ndunguru, akisoma uamuzi wa Mahakama leo Novemba 6, 2026, kwa niaba ya jopo la majaji, amesema Mahakama imeridhika kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, alitenda kosa la uchochezi kwa mujibu wa Kifungu cha 390 cha Kanuni ya Adhabu, hivyo kumtia hatiani kwa kosa hilo.
Jaji Ndunguru amesema Mahakama inaamini kuwa Lissu alikuwa na taarifa ya kosa dogo la uchochezi na alikuwa na nafasi ya kujitetea, huku ushahidi wote uliotolewa ukijikita katika suala la uchochezi na kauli za kumchochea umma kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, upande wa mashtaka ulisimama kuwasilisha hoja kuhusu adhabu inayopaswa kutolewa dhidi ya mshtakiwa.
Akizungumza kwa niaba ya Jamhuri, Katuga amesema kwa mujibu wa Kifungu cha 339 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), Mahakama inaweza kupokea ushahidi hadi kufikia hatua ya kutoa adhabu inayofaa.
Amesema moja ya malengo ya adhabu ni kutoa onyo kwa mtu aliyepatikana na hatia ili asirudie kosa hilo au kutenda makosa mengine, pamoja na kuwa onyo kwa watu wengine wenye nia ya kutenda makosa kama hayo.
Katuga amesema licha ya kutokuwepo kwa kumbukumbu za makosa ya awali dhidi ya mshtakiwa, taarifa zilizopo polisi zinaonyesha ongezeko kubwa la watu wanaotenda makosa ya kuchochea umma kwa maslahi yao binafsi ya kisiasa au kiuchumi.



Toa Maoni Yako:
0 comments: