Na Mwandishi Wetu, Arusha.

MKUU wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, ameingilia kati mgogoro wa ardhi uliodumu kwa takribani miaka 20 katika Kijiji cha Makuyuni, Wilaya ya Monduli, kwa kupendekeza ekari 100 za eneo la mwekezaji kutengwa kwa ajili ya wananchi wa Kitongoji cha Zaburi.

Hatua hiyo inalenga kupata suluhisho la kudumu la mgogoro huo uliohusisha wananchi kuvamia eneo la ekari 200 linalomilikiwa na kampuni ya Rhino Equipment & Transportation na kuanzisha makazi pamoja na shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Zaburi, Novemba 6, 2026, Makalla alisema kampuni hiyo ndiyo mmiliki halali wa eneo hilo, lakini Serikali imependekeza sehemu ya ardhi hiyo kutengwa kwa wananchi kutokana na uwepo wa kitongoji kilichosajiliwa na kuendelezwa kwa miundombinu ya kijamii.

Alisema kitongoji hicho tayari kina huduma muhimu zikiwemo msikiti, kanisa, shule ya awali, maji na umeme, hali inayohitaji suluhisho linalozingatia maslahi ya wananchi na haki za mwekezaji.

Aidha, Makalla aliuagiza uongozi wa kampuni hiyo kukutana na wananchi walioingia katika eneo lake jingine lenye ukubwa wa ekari 100 ili kujadiliana na kufikia makubaliano yatakayowezesha matumizi sahihi ya ardhi hiyo na kumaliza mgogoro huo.

Aliwataka wananchi kuwa watulivu na kusitisha uvamizi pamoja na shughuli za kuendeleza maeneo hayo hadi mazungumzo na makubaliano yatakapokamilika.

Pia, aliiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Monduli kusimamia utekelezaji wa maelekezo hayo na kuhakikisha eneo litakalotengwa kwa ajili ya wananchi linakuwa na mpango mzuri wa matumizi ya ardhi.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mzee Leng’ida alisema hatua iliyochukuliwa na Mkuu wa Mkoa pamoja na timu yake imerejesha matumaini kwa wakazi wa Kitongoji cha Zaburi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na sintofahamu kuhusu hatma ya makazi yao.

Alisema busara na hekima zilizotumika katika kutafuta suluhisho la mgogoro huo zitasaidia kuleta matumaini mapya na kuwarejeshea wananchi amani.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Makuyuni, Ngayoki, alisema atahakikisha maelekezo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa yanatekelezwa katika ngazi ya kijiji na kata kwa kushirikiana na wananchi.

Naye mkazi wa Kitongoji cha Zaburi, Naserian Saitabau, alisema mgogoro huo umewafanya wananchi kuishi kwa taharuki kwa miaka mingi kutokana na kutokuwa na uhakika wa hatma ya makazi yao.

Alisema hatua ya Mkuu wa Mkoa kuingilia kati imewapa matumaini mapya ya kupata suluhisho la kudumu litakalowawezesha kuishi kwa amani na kuendelea na shughuli zao za maendeleo.
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: