
Na Dk Reubeni Lumbagala
Mkoa wa Tanga ni maarufu kwa uzalishaji wa matunda nchini. Machungwa ni miongoni mwa matunda yanayozalishwa kwa wingi katika wilaya za Muheza, Korogwe na Handeni mkoani humo.
Wakulima wa zao hili hufanya jitihada kubwa za uzalishaji, lakini bado hawajafaidi vya kutosha jasho lao. Wakulima hutegemea baada ya kuvuna, wauze machungwa kwa bei nzuri ambayo itarejesha gharama za uendeshaji.
Aidha, wakulima hao hutegemea kupata faida kwani kwao kilimo hicho ni ajira kwa ajili ya kuendesha maisha yao na kufanya mambo mengine ya maendeleo kama kusomesha watoto, kujenga nyumba, kufungua biashara, kununua vyombo vya moto za usafiri, kutaja kwa uchache.
Miongoni mwa changamoto katika kilimo cha machungwa ni bei ndogo na kukosa soko la uhakika. Hili limesababisha wakulima kuuza machungwa yao mashambani kwa madalali.
Kwa kufanya hivyo, wakulima wamejikuta wakiuza machungwa yao kwa bei ndogo huku madalali wakinufaika pasi na kumwaga jasho kama walivyomwaga wakulima.
Kutokana na changamoto hizi, serikali ya mkoa wa Tanga chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa, Balozi Dk. Batilda Buriani, umejizatiti kuinua zao hili ili libadili hali za maisha ya wakulima na kuchangia katika maendeleo.
Novemba 1, 2026, katika kikao cha viongozi wa mkoa na wilaya, Dk. Buriani alisema, mkoa wa Tanga huzalisha asilimia 60 ya machungwa yote nchini, hivyo ni muhimu kuweka mazingira mazuri ya biashara hiyo ili iwanufaishe wakulima.
"Tumepiga marufuku madalali kununua machungwa mashambani, machungwa yatauzwa katika vituo maalum, hii itasaidia machungwa kuuzwa kwa bei nzuri," amesema Dk. Buriani.
Katika hatua nyingine, Dk. Buriani amesema, serikali mkoani humo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), watajenga vituo vinne ambapo wanunuzi wa machungwa watakwenda kununua moja kwa moja katika vituo hivyo kwa bei elekezi.
Kimsingi, ujenzi wa vituo hivi na kuwa na bei elekezi ya machungwa ni mkakati mzuri wa kuinua zao hili. Ni wakati muafaka sasa kwa wakulima kufaidi jasho lao na kuona fahari kulima machungwa kwani sasa kilimo hicho kitalipa na chenchi itabaki.


Toa Maoni Yako:
0 comments: