
Na Mwandishi Wetu, Arusha
WAFANYABIASHARA 20 wa Kitanzania wanaoendesha biashara zinazolenga kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi wamechaguliwa kujiunga na awamu ya tatu ya programu ya AfroGreen, inayolenga kuwawezesha kukuza biashara zao, kuvutia uwekezaji na kuongeza fursa za ajira.,,
Programu hiyo ya miezi tisa inaendeshwa na Westerwelle Startup Haus Arusha (WSHA), kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania na Westerwelle Foundation ya Ujerumani, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ujasiriamali na kukuza biashara zinazozingatia uhifadhi wa mazingira.
Kati ya biashara 20 zilizochaguliwa, nane sawa na asilimia 40 zinaongozwa na w³³¾anawake, huku 15 zikitoka Arusha na tano kutoka Dar es Salaam na Iringa.
Biashara hizo zinajihusisha na maeneo mbalimbali yakiwemo nishati jadidifu, uchumi mzunguko, kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi, kukabiliana na athari za tabianchi na minyororo endelevu ya thamani.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa awamu hiyo sambamba na maadhimisho ya miaka minne ya WSHA, Mkurugenzi wa Westerwelle Foundation Tanzania, Isaack Shayo, alisema programu hiyo ni sehemu ya mkakati wa taasisi hiyo wa kuwawezesha wajasiriamali kuvuka hatua za ukuaji na kuingia katika soko la uwekezaji.
Alisema tangu kuanzishwa kwa WSHA, mwaka 2022, taasisi hiyo imeendelea kuwaunganisha wajasiriamali wa Kitanzania na mitandao ya kimataifa, huku mahitaji ya biashara zinazokua yakichochea kuanzishwa kwa programu zinazolenga kuwaandaa kupata mitaji na fursa za kibiashara.
Shayo alisema mpango wa WSHA hadi mwaka 2030 umeweka msisitizo katika kuwaunganisha wajasiriamali na wawekezaji, kuwapatia fursa za kimataifa na kuimarisha ushirikiano na wafanyabiashara wa Arusha ili kupata ushauri na mitaji.
Aliongeza kuwa kupitia AfroGreen, washiriki watapata msaada wa kuimarisha mifumo ya biashara zao, kujiandaa kuvutia uwekezaji na kupima mchango wa shughuli zao katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa hḥupande wake, Mkuu wa Kitengo cha Ajira na Kipato katika Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania, Andrea Inglin, alisema Serikali ya Uswisi imeendelea kuunga mkono programu hiyo kwa kutambua umuhimu wa mitaji, utaalamu wa kiufundi na mitandao ya kibiashara katika kukuza biashara zinazotoa suluhisho za changamoto za tabianchi.
Alisema mabadiliko ya tabianchi ni changamoto inayogusa maeneo mbalimbali ya maisha na uchumi, hivyo ni muhimu kuwawezesha wajasiriamali kupata rasilimali na maarifa yatakayowawezesha kuanzisha na kuendeleza suluhisho endelevu.
Takwimu zinaonesha kuwa awamu mbili zilizopita za AfroGreen zilisaidia biashara changa 30, kuchangia upatikanaji wa ajira 42 na kuvutia uwekezaji uliovuka Euro 132,000.
Katika awamu ya tatu, programu hiyo inalenga kusaidia biashara zote 20 kujiandaa kupata mitaji na kuongeza ajira zisizopungua 40, sambamba na kuvutia uwekezaji mpya.
Akizungumzia mchango wa programu hiyo, Afisa Vijana wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Evodius Cleophace, aliipongeza WSHA kwa kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwawezesha vijana kiuchumi.
waliofikiwa.
Alisema programu kama AfroGreen zinasaidia kuwafikia wajasiriamali ambao huenda wasipate fursa za aina hiyo kupitia mifumo mingine ya uwezeshaji.Aidha, alibainisha kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/27, Halmashauri ya Jiji la Arusha imetoa mikopo ya Sh bilioni mbili kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, ambapo vijana wamepatiwa Sh 578,702,420.
Alitaja kampuni ya Himan Investment, iliyoshiriki katika awamu iliyopita ya AfroGreen, kuwa miongoni mwa wanufaika wa fursa hizo baada ya kupata mkopo wa zaidi ya Sh milioni 130 kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (YDF).
Naye mjumbe wa Bodi ya WSHA na mwanzilishi mwenza wa Obuntu Hub, Collins Kimaro, aliwahimiza washiriki wapya kutumia fursa hiyo kwa kujenga biashara imara na kuamini uwezo wao wa kufikia malengo makubwa.
Kwa upande wake, Mwanzilishi wa Innolif Aquaculture Group, Fortunatus Fungatwende, alisema ushiriki wao katika programu hiyo utawasaidia kuimarisha mifumo ya biashara na kuongeza uwezo wa kuvutia wawekezaji.
Alisema wanatarajia kupata maarifa, ujuzi na mahusiano ya kibiashara yatakayowawezesha kupata mitaji ya kupanua shughuli zao.
Washiriki wa AfroGreen 3.0 watanufaika na mafunzo ya biashara, ushauri wa kitaalamu na mwongozo wa kuandaa biashara zao kwa ajili ya uwekezaji, pamoja na kuunganishwa na mtandao wa wawekezaji binafsi.
Programu hiyo inatarajiwa kuhitimishwa Mei 28, 2027, kwa siku maalumu ya kuwasilisha mipango ya biashara kwa wawekezaji (Demo Day), ambapo washiriki watapata fursa ya kueleza biashara zao na kutafuta mitaji ya kuziendeleza.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2022, WSHA imewafikia wajasiriamali 809, wakiwemo waanzilishi wa biashara changa 309, huku wanawake wakichangia asilimia 55 ya wote waliofikiwa.



Toa Maoni Yako:
0 comments: