Articles by "ELIMU."
Showing posts with label ELIMU.. Show all posts
Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza matokeo ya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (Darasa la Saba) uliofanyika nchini kote kuanzia Septemba 9, 2026.

Matokeo hayo yametangazwa leo, Jumanne, Novemba 3, 2026, na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Profesa Said Ally Mohamed.

Na Mary Gwera, Mahakama-Mwanza

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju amewataka Wahitimu wa Kidato cha Nne wa Shule ya Sekondari Lake kutumia vema maarifa waliyopata kutoka katika shule hiyo kama mwanzo wa safari na si kikomo cha ndoto.

Mhe. Masaju alieleza hayo tarehe 02 Novemba, 2026 jijini Mwanza alipokuwa akitoa hotuba yake akiwa Mgeni Rasmi katika Mahafali ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Lake iliyopo jijini Mwanza shule ambayo naye alisoma katika safari yake ya kitaaluma.

“Leo nimesimama kama mmoja wa watu ambao safari yao ilipita katika shule hii. Sitaki mnaponisikia mseme tu kwamba mwanafunzi wa zamani wa Lake amefika katika nafasi hii. Nataka mjifunze jambo pana zaidi: safari ya maisha hujengwa kwa hatua, kwa watu wanaotusaidia, kwa maamuzi tunayofanya na kwa juhudi tunazoweka kila siku. Msifikiri kwamba lazima muanze mkiwa na kila kitu. Anzeni kwa kutumia vizuri kile mlicho nacho, muda wenu, nafasi ya kujifunza, ushauri mnaopewa na vipaji mlivyonavyo,” alisema Jaji Mkuu.

Mhe. Masaju amewataka Wahitimu hao kuendelea kujifunza, kuwa waadilifu, kutobadili misingi yao kwa faida ya muda mfupi, kuheshimu watu, kutumia teknolojia kwa busara, kuipenda Tanzania kwa vitendo kwa kufanya kazi kwa bidii, kuheshimu sheria, kulinda mali za umma na kutatua matatizo ya jamii.

“Msisubiri mazingira yawe kamili ndipo mfanye bidii. Jengeni uwezo wenu katika mazingira mliyopo, huku mkiboresha mazingira hayo kwa manufaa ya wengine,” amesisitiza Jaji Mkuu na kusema kwamba, angependa siku zijazo, asikie simulizi za wahitimu wa leo: walioboresha huduma za afya, waliobuni teknolojia, walioanzisha biashara na ajira, waliotetea haki, waliofundisha vizazi vipya na walioleta mabadiliko chanya katika jamii zao. Hizo ndizo simulizi zinazojenga heshima ya taasisi.

Ameongeza kuwa, Kidato cha Nne ni hatua muhimu, lakini si mwisho wa elimu wala mwisho wa kujijenga. Ni mlango unaofunguka kuelekea hatua nyingine. Amesema, “baadhi yenu mtaendelea na Kidato cha Tano na Sita; wengine mtachagua mafunzo ya ufundi na stadi; wengine mtajiandaa kwa njia nyingine za kujifunza na kujenga taaluma. Njia zinaweza kutofautiana, lakini wajibu ni mmoja: kuendelea kujifunza na kujitengeneza.”

Aidha, amewakumbusha wahitimu hao kutokimbilia kutafuta mafanikio yanayoonekana kabla hawajajenga msingi wa mafanikio ya kweli kwakuwa Dunia ya sasa inaweza kumfanya kijana aamini kwamba mafanikio ni kuonekana, kuwa maarufu au kupata fedha haraka. Amesema, huo si msingi salama wa maisha kwani mafanikio ya kudumu yanahitaji maarifa, ujuzi, nidhamu, uvumilivu, uaminifu na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi hata pale ambapo hakuna mtu anayewaangalia.

Kadhalika, Jaji Mkuu amewaasa Wahitimu hao wa Kidato cha Nne kumcha Mungu na wawe na dhamira inayowaongoza kutenda yaliyo mema huku akinukuu Biblia Takatifu, katika Mithali 4:13, inayohimiza kuishika elimu na Qur’ani Tukufu, katika Suratul Al-Alaq (96:1–5), inatukumbusha umuhimu wa kusoma na kujifunza ambapo mafundisho hayo yanatuelekeza kuona elimu kama wajibu na neema inayopaswa kutumiwa kwa busara. Vilevile, amewataka kuwaheshimu wazazi, walezi na walimu wao na kusisitiza kuwa heshima si udhaifu; ni alama ya ukomavu.

Katika hatua nyingine, Mhe. Masaju amewataka Wahitimu hao kutosubiri Taifa liwaite viongozi ndipo waanze kuonesha uongozi hivyo, amewasisitiza kuanza kuongoza maisha yao kwa nidhamu, kwa kuwa waaminifu, kwa kuwaheshimu wengine na kwa kutimiza wajibu wao kwakuwa Uongozi huanza kabla ya cheo.

Akiizungumzia Shule ya Sekondari Lake, Jaji Mkuu amesema anaiheshimu na kusisitiza Lake isiwe shule inayojivunia tu watu waliopita hapo bale iwe shule inayowaandaa watu ambao Taifa litajivunia kesho. “Kila mhitimu anayekuwa muadilifu, kila mtaalamu anayefanya kazi kwa ubora, kila kiongozi anayewajibika na kila kijana anayebuni suluhisho jipya, anaongeza ukurasa katika historia ya Lake,” amesisitiza.

Kadhalika, Mhe. Masaju amewakumbusha watu mbalimbali waliomaliza katika shule hiyo na katika shule nyingine nchini kuwa na utaratibu wa kuzitembelea shule walizosoma. Amesisitiza kwa kusema, “Tunaporejea mashuleni tulikosoma, tunapata fursa ya kutoa shukrani na kukutana na wale waliochangia kutujenga.”

Jaji Mkuu amesema, amerudi shuleni hapo akiwa na dhamira ya kutoa shukrani, kutambua mchango wa shule hiyo na, muhimu zaidi, kuwaambia wanafunzi wa leo kwamba ndoto zao zinaweza kuwapeleka mbali zaidi ya mipaka wanayoiona sasa.

Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu ameushukuru Uongozi wa Shule hiyo kwa kumualika na kumpa nafasi ya kurejea katika Shule ya Sekondari Lake mahali pa kumbukumbu, malezi na sehemu ya safari ya maisha yake na wengine wengi waliopita katika shule hiyo. Ameomba shule hiyo iendelee kung’aa, si kwa historia yake tu, bali kwa ubora wa watu inaowaandaa kwa ajili ya Tanzania.

“Nimepokea mwaliko huu kwa heshima kubwa. Lakini niseme wazi: kwangu mimi, leo si siku ya kutembelea shule nyingine tu; ni siku ya kurejea mahali ambapo sehemu ya safari yangu ya maisha ilianzia. Kabla ya vyeo vyetu, kabla ya ofisi zetu, kabla ya majukumu yetu kitaifa na kabla ya heshima tuliyokuwa nayo, tulikuwa wanafunzi. Nasi pamoja na Madaraka yetu tulikuwa vijana wenye safari mbele yetu, wenye mambo ya kujifunza, wenye ndoto na wenye wajibu wa kufanya bidii,” amesema Mhe. Masaju.

“Ningependa niwaambie jambo moja mapema: msinitazame leo kwa kuona tu cheo nilichonacho. Nitajeni pia kama mmoja wa wanafunzi waliowahi kukaa madarasani hapa, kusoma, kufundishwa na kuandaliwa kwa maisha. Cheo ni dhamana ya leo; lakini historia ya mtu hujengwa hatua kwa hatua, na mara nyingi hatua hizo huanzia katika madarasa kama haya,” ameeleza.

Kadhalika, Jaji Mkuu amekiri kupokea kwa furaha taarifa ya wazo la kuanzisha Chuo Kikuu cha Lake (Lake University) ambapo amewapongeza viongozi na wadau wa shule kwa kuwa na ndoto hiyo. Amesema, Taasisi inayothubutu kufikiria hatua inayofuata inaonesha kuwa haitaki kuishi kwa kutegemea historia pekee; inataka kushiriki katika kuandika historia mpya.

“Nimeelezwa pia kuhusu changamoto ya eneo lililokuwa limetengwa kwa ajili ya mradi huo. Changamoto hiyo isitumike kuzima ndoto, bali iwe nafasi ya kutathmini upya mpango. Hata hivyo, ndoto ya chuo kikuu inahitaji maandalizi ya kitaalamu na ya muda mrefu: upembuzi yakinifu, mahitaji ya jamii na soko la ajira, maeneo ya kitaaluma yatakayopewa kipaumbele, uwezo wa kifedha, miundombinu, rasilimali watu, usimamizi na utii wa taratibu za mamlaka husika,” amesisitiza.

Ameushari uongozi wa shule hiyo uandae mpango kabambe wa hatua kwa hatua, ukiangalia mahitaji ya sasa na ukuaji wa taasisi kwa miaka mingi ijayo. Eneo la chuo lisitazamwe kwa mahitaji ya leo pekee; litazamwe kwa uwezo wa kupanuka, usafiri, huduma, mazingira na mahitaji ya wanafunzi na wafanyakazi. Ndoto kubwa inahitaji maandalizi makubwa, lakini utekelezaji wake uanze kwa hatua zinazopimika.

Kadhalika, ametoa wito kwa wadau wote kuendelea kuwekeza katika walimu, maabara, maktaba, teknolojia, michezo, ushauri nasaha na mazingira salama ya kujifunzia na si kuwekeza katika majengo pekee bali wawekeze pia kwa watu, mifumo na maadili yanayofanya majengo hayo yawe na maana.

Awali akizungumza katika mahafali hayo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Lake, Mwalimu Lucas Bunuma amesema jumla ya Wanafunzi 76 wamehitimu kidato cha nne, 30 Wanawake na 46 Wanaume.

Mwalimu Bunuma amemshukuru Jaji Mkuu, Mhe. Masaju kwa heshima na fadhila kubwa ambayo amefanya kwa uongozi wa shule hiyo kwa kukubali kuwa mgeni rasmi wa siku hiyo muhimu.

“Tunajua una majukumu mengi na katika shughuli zako ikiwa ni pamoja na familia, bado umetupa kipaumbele siku hii ya leo, na umetupa hadhi kubwa ya kitaifa, wewe ambaye ulikuwa mwanafunzi wa shule hii, ikiwa ni pamoja na wanafunzi wengine waliosoma hapa na wamehudhuria mahafali ya leo,” amesema Mkuu wa Shule huyo.

Akizungumzia kuhusu maendeleo ya Taaluma, Mwalimu Bunuma ameishukuru Bodi ya Wamiliki ya Shule hiyo kwa kuboresha mazingira mazuri yanayohamasisha wanafunzi kujifunza na kufundisha. “Tumepata ushindi wa daraja la kwanza, la pili, la tatu pekee kwa mwaka 2025. Kidato cha nne na cha sita ufaulu wetu ni asilimia 100. Kwa mfano mwaka 2025, kidato cha nne daraja la kwanza tulikuwa na wanafunzi 44, daraja la pili wanafunzi 33, daraja la tatu wanafunzi 4. Kidato cha sita daraja la kwanza walikuwa ni wanafunzi 20, daraja la pili walikuwa ni wanafunzi 36, na daraja la tatu walikuwa ni wanafunzi 10,” amesema.

Katika Mahafali hayo Kadhalika Jaji Mkuu alipata wasaa wa kutembezwa katika maeneo mbalimbali ya shule hiyo ikiwemo Maabara, Maktaba na sehemu nyingine kadhaa ambapo alijionea maboresho mbalimbali yaliyofanyika katika shule hiyo. Kadhalika, Mhe. Masaju amekutana na Mwalimu aliyemfundisha Somo la Kemia (Chemistry), Mwalimu Kiran Mody ambapo ameonesha furaha baada ya kukutana na Mwalimu huyo.

Miongoni mwa Viongozi waliosoma katika shule hiyo ni pamoja na Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, Mhe. Dkt. Stegomena Tax, aliyekuwa waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga taifa, lakini pia alikuwa katibu mtendaji wa jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika (SADC), Dkt. Angelina Mabula na wengine kadhaa.

Mahafali hayo yalipambwa na burudani mbalimbali kutoka kwa Wahitimu, Wanafunzi na Kikundi cha Ngoma za Asili cha Bujora igizo la uendeshaji wa Mahakama ya Mazoezi (Moot Court).

Matukio katika picha ya Mahafali ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Lake ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju leo tarehe 02 Novemba, 2026 jijini Mwanza.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (aliyesimama katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wahitimu wa Kidato cha Nne wa Shule ya Sekondari Lake iliyopo jijini Mwanza. Mhe. Masaju alikuwa Mgeni Rasmi wa Mahafali hayo yaliyofanyika tarehe 02 Novemba, 2026.
Wahitimu wa Kidato cha Nne wa Shule ya Sekondari Lake iliyopo jijini Mwanza wakiwa katika Mahafali yaliyofanyika tarehe 02 Novemba, 2026.


Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akitoa hotuba yake wakati wa Mahafali ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Lake yaliyofanyika tarehe 02 Novemba, 2026 jijini Mwanza.
Sehemu ya Wazazi, Walezi pamoja na Wageni Waalikwa wakisikiliza hotuba ya Mgeni Rasmi, Jaji Mkuu, Mhe. George Masaju (hayupo katika picha) wakati wa Mahafali ya Shule ya Sekondari Lake yaliyofanyika tarehe 02 Novemba, 2026.
Wahitimu wa Kidato cha Nne wa Shule ya Sekondari Lake.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Mwanza, Mhe. Ephery Kisanya akizungumza jambo wakati wa Mahafali hayo.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akisalimiana na aliyekuwa Mwalimu wake wa Somo la Kemia, Mwalimu Mstaafu wa Shule ya Sekondari Lake, Kiran Mody.


Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akipokea zawadi kama ishara ya upendo kutoka Uongozi wa Shule ya Sekondari Lake iliyopo jijini Mwanza.
Sehemu ya Viongozi wa Shule ya Sekondari Lake wakifuatilia hotuba ya Jaji Mkuu wakati wa Mahafali ya Kidato cha Nne yaliyofanyika tarehe 02 Novemba, 2026. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Lucas Bunuma.


Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stagomena Tax akizungumza jambo wakati wa Mahafali hayo.


Mkuu wa Shule ya Sekondari Lake, Mwalimu Lucas Bunuma akitoa neno wakati wa Mahafali ya Shule ya Sekondari Lake jijini Mwanza.


Katibu wa Baraza la Uongozi wa Shule akitoa neno.


Igizo la Uendeshaji Mahakama ya Mazoezi (Moot Court) likifanywa na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Lake wakati wa Mahafali ya Kidato cha Nne ya Shule hiyo.


Burudani kutoka kwa Wanafunzi wakati wa Mahafali ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Lake.



Burudani kutoka katika Kikundi cha Ngoma za Asili cha Bujora.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akiangalia moja ya vitabu vilivyopo katika Maktaba ya Shule ya Sekondari Lake.


Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi waliosoma (Alumni) katika Shule ya Sekondari Lake ambao ni pamoja na Mhe. Dkt. Stergomena Tax (wa tatu kushoto), Mwalimu Lucas Bunuma (wa kwanza kushoto). Aliyesimama wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, CP Salum Hamduni.


Jaji Mkuu akipata maelezo alipotembelea Maabara ya Shule ya Sekondari Lake tarehe 02 Novemba, 2026 alipoalikwa kuwa Mgeni Rasmi wa Mahafali ya Kidato cha Nne ya Shule hiyo.


Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akisaini kitabu cha wageni alipowasili ofisini kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Lake kuhudhuria Mafahali ya Kidato cha Nne ya Shule hiyo tarehe 02 Novemba, 2026.




Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akiwa katika picha za pamoja na Wahitimu wa Kidato cha Nne pamoja na baadhi ya Viongozi wengine walioshiriki katika Mahafali hayo.


Sehemu ya picha za Makundi wakati wa Mahafali ya Shule ya Sekondari Lake. (Picha na MARY GWERA, Mahakama)

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira (katikati) na Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation, Zuweina Farah (wa pili kutoka kulia) wakikata utepe wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kituo cha kwanza kati ya 50, vinavyojengwa kwa ajili ya Rasilimali za Walimu katika Shule ya Msingi Naurei, wilayani Arusha, wakiwa pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya, Selemani Msumi (wa kwanza kushoto), Mkuu wa Shule, Getrude Tarimo (wa tatu kutoka kushoto) na wanafunzi tukio hilo limefanyika mwishoni mwa wiki jijini Arusha. Kituo hicho kimejengwa kupitia ushirikiano wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) na Vodacom Tanzania Foundation kwa lengo la kuimarisha mafunzo ya kidijitali kwa walimu na kuboresha ubora wa elimu nchini.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira (wa tatu kutoka kulia) na Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation, Zuweina Farah (wa tatu kutoka kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine wa Serikali na uongozi wa Shule ya Msingi Naurei katika Kituo cha Rasilimali za Walimu kilichozinduliwa rasmi shuleni hapo, Kituo hicho kimeanzishwa kupitia ushirikiano wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) na Vodacom Tanzania Foundation kwa lengo la kuimarisha mafunzo ya kidijitali kwa walimu na kuboresha ubora wa elimu nchini.
Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation, Zuweina Farah, akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Rasilimali za Walimu katika Shule ya Msingi Naurei, wilayani Arusha. Kituo hicho kimeanzishwa kupitia ushirikiano wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) na Vodacom Tanzania Foundation kwa lengo la kuwekeza katika maendeleo ya walimu kwa kutumia teknolojia na miundombinu ya kidijitali, ili kuwawezesha waalimu walio kazini kujiendeleza kitaaluma, kuboresha mbinu za ufundishaji na hatimaye kuongeza ubora wa elimu kwa wanafunzi nchini.
Baadhi ya vifaa vya TEHAMA vilivyowekwa katika Kituo cha Rasilimali za Walimu katika Shule ya Msingi Naurei, wilayani Arusha, kituo hiki kimejengwa kupitia ushirikiano wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) na Vodacom Tanzania Foundation kwa lengo la kuwawezesha walimu walio kazini kupata mafunzo ya kidijitali na kuimarisha uwezo wao wa kutumia teknolojia katika ufundishaji.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Neema Lugangira, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa Kituo cha Rasilimali za Walimu katika Shule ya Msingi Naurei, wilayani Arusha. Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kuimarisha miundombinu na matumizi ya teknolojia ili kuwawezesha walimu kujiendeleza kitaaluma, kuboresha mbinu za ufundishaji na kuongeza ubora wa elimu nchini.
Muonekano wa jengo la Kituo cha Rasilimali za Walimu (TRC) katika Shule ya Msingi Naurei, wilayani Arusha. Kituo hicho ni cha kwanza kati ya vituo 50 vinavyotarajiwa kujengwa nchini kupitia ushirikiano wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) na Vodacom Tanzania Foundation, kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa mafunzo ya kidijitali na TEHAMA kwa walimu, kuimarisha mbinu za ufundishaji na kuboresha ubora wa elimu nchini.


●Ni kituo cha kwanza kati ya 50 vinavyotarajiwa kujengwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini

●Kupitia ushirikiano wa TIE na Vodacom Tanzania Foundation, maelfu ya Walimu watanufaika na mafunzo ya kidijitali yatakayoboresha uwezo wa ufundishaji na matumizi ya TEHAMA

Arusha, Tanzania – 9 Oktoba 2026; Maelfu ya walimu nchini sasa watanufaika na upatikanaji wa mafunzo ya maendeleo ya kitaaluma kupitia matumizi ya teknolojia, hatua inayolenga kuongeza umahiri wa ufundishaji, kuongeza ufaulu wa wanafunzi na kuchochea maendeleo ya taifa kupitia elimu.

Mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano kati ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) na Vodacom Tanzania Foundation katika utekelezaji wa Programu ya Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (TCPD/MEWAKA), ambayo imeimarisha matumizi ya Mfumo wa Usimamizi wa Kujifunza (LMS) pamoja na Vituo vya Rasilimali za Walimu (TRC) nchini.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi na kuzindua kituo cha Rasilimali za Walimu kilichojengwa shule ya Msingi Naurei, wilayani Arusha, kikiwa ni cha kwanza kati ya 50 vinavyotarajiwa kujengwa hapa nchini, Mkuu wa wilaya ya Arumeru Neema Lugangira alisema uwekezaji kwa walimu ni uwekezaji wa moja kwa moja katika kuongeza uwezo wa kufundisha kwa kutumia TEHAMA, na kwa ujumla mustakabali wa elimu nchini.

“Leo nimekuja kuzindua kituo hiki, hili sio jambo dogo maana kituo hiki kitaongeza ubora wa elimu hapa nchini, na pia ni uthibitisho kwamba serikali na sekta binafsi zikishirikiana kuimarisha miundombinu, teknolojia na mifumo inayomwezesha mwalimu kujifunza na kujiendeleza wakati wote matokeo yake ni kuboresha elimu kwa ujumla wake. Mwalimu anayepata maarifa mapya, anayeongeza kiwango cha elimu alichonacho na kutumia teknolojia kwa ufanisi, huongeza nafasi ya wanafunzi kufaulu na kufikia ndoto zao,” alisema Mh Lugangira.

Alisema tathmini ya mahitaji ya TCPD/MEWAKA iliyohusisha Vituo vya Rasilimali za Walimu 178, walimu 350 na wadau mbalimbali imebaini kuwa walimu wengi wana hamasa ya kujifunza na kutumia teknolojia, huku asilimia 99 wakifahamu LMS na asilimia 71 wakiwa na uelewa wa msingi wa TEHAMA.

Hata hivyo, tathmini hiyo imeonesha kuwa changamoto za upatikanaji wa vifaa vya TEHAMA, kompyuta, intaneti na usaidizi wa kiufundi bado zinaendelea kuathiri matumizi kamili ya mfumo huo, hasa katika maeneo ya vijijini.

“Mafanikio ya TCPD/MEWAKA hayategemei motisha ya mwalimu pekee. Yanahitaji uwekezaji katika vifaa, uwepo wa intaneti, mafunzo ya vitendo na mifumo imara. Ndio maana ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi una umuhimu mkubwa katika kuhakikisha walimu wanapata mazingira bora ya kujifunza,” alisisitiza.

Mkuu wa Wilaya pia aliipongeza Vodacom Tanzania Foundation kwa mchango wake katika kuendeleza elimu nchini na kuzihamasisha taasisi nyingine za sekta binafsi kuunga mkono juhudi hizo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation, Zuweina Farah alisema uwekezaji katika walimu ni moja ya njia zinazoleta matokeo makubwa katika kuboresha mfumo wa elimu na kukuza uchumi wa kidijitali wa taifa.

“Tunafahamu kuwa walimu ndiyo nguzo ya maendeleo ya elimu. Wanapopewa fursa za kujifunza na kutumia teknolojia kwa ufanisi, matokeo chanya huonekana moja kwa moja kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla. Hii ndiyo sababu Vodacom Tanzania Foundation imeamua kuwekeza katika mifumo na miundombinu inayowezesha maendeleo ya walimu kwa njia endelevu,” alisema Farah.

Aliongeza kuwa kupitia ushirikiano na TIE, matumizi ya LMS yameondolewa gharama za data kwa watumiaji wa mtandao wa Vodacom, hatua iliyolenga kupunguza vikwazo vya upatikanaji wa maudhui ya maendeleo ya kitaaluma kwa walimu.

“Kupitia ushirikiano wetu na TIE, walimu wanaotumia mtandao wa Vodacom wanaweza kuifikia LMS bila gharama yeyote. Tunaamini teknolojia ina uwezo mkubwa wa kuondoa vikwazo vya upatikanaji wa elimu na kuhakikisha walimu wengi zaidi wanapata fursa ya kuendeleza taaluma zao bila kujali mahali walipo,” alisema.

Farah aliongeza kuwa sekta binafsi inaweza kuharakisha utekelezaji wa mipango ya elimu kwa kuwekeza katika teknolojia, muunganisho wa intaneti, vifaa vya TEHAMA, ubunifu na utaalamu wa kidijitali unaohitajika ili kujenga mfumo wa elimu unaoendana na mahitaji ya karne ya 21.
Na Mwandishi Wetu, Pwani.

MBUNGE Viti Maalum Mkoa wa Pwani Mariam Ibrahim, amechangia Sh. milioni tano kwa ajili ya ujenzi wa Shule Mpya ya Msingi Kisutu iliyopo Jimbo la Bagamoyo mkoani humo. 

Ametoa mchango huo wakati aliposhiriki katika  tukio la upandaji wa miti 300 lililofanyika katika eneo la shule hiyo.
Akizungumza na wananchi, Mbunge Mariam amesema mchango huo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na wananchi pamoja na wadau mbalimbali katika kuhakikisha shule hiyo inakamilika. 

Pia amempongeza Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo CPA Subira  Mgalu, kwa juhudi zake za kusimamia maendeleo ya elimu na kuendelea kushirikiana na wananchi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Aidha, amempongeza  Diwani wa Kata ya Kisutu Awesu Muhidini, kwa uongozi wake na namna anavyoshirikiana na wananchi kuipambania shule hiyo hadi kufikia hatua ya sasa.

Mbunge Mariam pia amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha upatikanaji wa eneo lililojengwa shule hiyo, hatua ambayo imefungua fursa ya kuboresha huduma za elimu kwa watoto wa Kata ya Kisutu.

Katika hafla hiyo,amekabidhi sh. milioni 3 papo hapo, huku akiahidi kuwa Sh. milioni mbili zilizobaki atazikabidhi kupitia Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo CPA Mgalu, ili kukamilisha ahadi yake ya mchango wa Sh.Milioni 5.