Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN), Beda Msimbe (Kushoto) akizungumza mara baada ya kupokea timu ya maofisa wa PSSSF ilipotembelea Makao Makuu ya Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) yaliyopo Kijitonyama, Dar es Salaam. Kulia ni Mkuu wa Msafara wa PSSSF, Abdul Njaidi.

Na Mwandishi Wetu TBN, DAR ES SALAAM.

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umeeleza dhamira ya kutumia nguvu ya majukwaa ya kidijitali kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa elimu kuhusu hifadhi ya jamii, pensheni na uwekezaji, kupitia ushirikiano na Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN).

Ushirikiano huo umejadiliwa wakati timu ya maofisa wa PSSSF ilipotembelea Makao Makuu ya Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) yaliyopo Kijitonyama, Dar es Salaam, ambapo pande hizo zilikubaliana kuimarisha ushirikiano katika utoaji wa taarifa sahihi na uelimishaji wa umma.

Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, alisema mtandao huo wenye zaidi ya wanachama 200 nchini na Diaspora una nafasi kubwa ya kusaidia taasisi mbalimbali kuwafikia wananchi kupitia majukwaa ya kidijitali.

Msimbe alisema TBN iko tayari kutumia mtandao wake katika kuelimisha jamii kuhusu huduma na shughuli za PSSSF, huku akisisitiza umuhimu wa wanablogu kupata mafunzo ya kina kuhusu masuala ya hifadhi ya jamii ili taarifa wanazozifikisha kwa umma ziwe sahihi na zenye uelewa mpana.

Kwa upande wake, Mkuu wa Msafara wa PSSSF, Abdul Njaidi, alisema ushirikiano huo ni sehemu ya jitihada za mfuko kuimarisha uhusiano na wadau wa habari ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa elimu kwa jamii.

Njaidi alisema mapendekezo na hoja zilizowasilishwa na TBN zitafanyiwa kazi, akisisitiza kuwa PSSSF inalenga kuhakikisha wananchi wanaelewa kwa usahihi masuala ya pensheni, hifadhi ya jamii na uwekezaji unaofanywa na mfuko huo.
Naye Mdhamini wa TBN, Issa Michuzi, alisema mtandao huo una uzoefu mkubwa katika uandishi na usambazaji wa habari za kidijitali na uko tayari kushirikiana na PSSSF katika kuhakikisha elimu ya hifadhi ya jamii inawafikia wananchi kwa lugha rahisi na inayoeleweka.

Alisema TBN imejengwa kwa dhamira ya kukuza mazingira bora ya habari za kidijitali nchini, hivyo ushirikiano huo unaweza kuwa chachu ya kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala yanayogusa maisha na ustawi wao wa baadaye.
Katibu wa TBN, Rahel Pallangyo, alisema majukwaa ya wanachama wa mtandao huo yanaweza kuwa kiungo muhimu kati ya PSSSF na wananchi, hasa katika kipindi ambacho mitandao ya kidijitali imekuwa chanzo muhimu cha habari na maarifa.

Ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu hifadhi ya jamii, pensheni na fursa za uwekezaji, huku ukilenga kuwafikia wananchi wengi zaidi ndani na nje ya Tanzania.

Ujumbe wa PSSSF uliongozwa na Abdul Njaidi na kuwajumuisha Regina Kumba, Grayson Mgunda na Doreen Lyimo, huku upande wa TBN ukihudhuriwa na Mwenyekiti Beda Msimbe, Katibu Rahel Pallangyo, Mtaalamu wa Mawasiliano Cathbert Kajuna na Mdhamini Issa Michuzi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: