Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zinakutana jijini Dar es Salaam kujadili na kuweka mikakati ya kutatua changamoto na vikwazo vinavyokwamisha biashara ndani ya Jumuiya, hususan Vikwazo Visivyo vya Kikodi (Non-Tariff Barriers – NTBs).

Mkutano huo ni utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Mkutano wa 25 wa Wakuu wa Nchi za EAC, uliofanyika jijini Arusha Machi 7, 2026, ambao ulizitaka Nchi Wanachama kuchukua hatua za haraka za kuondoa vikwazo vyote vya biashara visivyo vya kodi vilivyoripotiwa ndani ya Jumuiya ifikapo Juni 30, 2026.
Sanjari na hayo, mkutano huo utajadili hatua za utekelezaji wa maelekezo ya Mkutano Maalum wa Pili wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Fedha na Uchumi (SCFEA) uliofanyika Novemba 25, 2025, ambao ulielekeza nchi wanachama kuondoa ushuru, ada, tozo na kodi za ndani zinazobagua bidhaa za Nchi Wanachama kinyume na matakwa ya Ibara ya 10 na 15 ya Itifaki ya Umoja wa Forodha ya EAC, ifikapo Juni 30, 2026 na kufanya marekebisho ya tafsiri ya baadhi ya maneno katika sheria za ndani ili kuendana na makubaliano ya Jumuiya.

Miongoni mwa ajenda muhimu zitakazojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na; tathmini ya utendaji wa Vituo vya Pamoja vya Huduma Mpakani (One Stop Border Posts – OSBPs), Mpango Kazi wa Kutatua Masuala Yanayoathiri Biashara ndani ya Jumuiya, pamoja na Jedwali la Utekelezaji wa Mpango Kazi huo.

Mkutano huo pia utajadili na kupitia Orodha ya Vikwazo Visivyo vya Kodi (Non-Tariff Barriers Index) ya EAC, ambayo ni miongoni mwa nyenzo zinazotumika kufuatilia, kutambua na kupima hatua zinazochukuliwa na Nchi Wanachama katika kushughulikia vikwazo vinavyoathiri biashara katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Hatua hizo ni muhimu katika kuimarisha utekelezaji wa Soko la Pamoja la EAC, ambalo linalenga kurahisisha usafirishaji bidhaa, watu, huduma na mitaji na haki ya kuanzisha shughuli za biashara katika Nchi Wanachama. Kuondolewa kwa vikwazo visivyo vya kodi na kurahisishwa kwa taratibu za mipakani kunatarajiwa kupunguza gharama na muda wa kufanya biashara, kuongeza ushindani na kukuza biashara ya ndani ya Jumuiya.

Mkutano huo unatarajiwa kutoa mapendekezo na hatua mahususi za utekelezaji zitakazosaidia kuharakisha uondoaji wa vikwazo vya biashara, kuboresha ufanisi mipakani na kuimarisha biashara ya kikanda, ikiwa ni sehemu ya jitihada za EAC kujenga Jumuiya yenye ushindani, jumuishi na inayotoa fursa zaidi kwa wananchi wake.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo ngazi ya Wataalamu unaongozwa na Mkurugenzi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Benjamini Mwesiga, akiongozana na Maafisa Waandamizi kutoka Wizara pamoja na taasisi mbalimbali za Serikali.
Na Oscar Assenga, Tanga

WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso, amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji wa hati fungani wenye thamani ya Sh bilioni 53.12 kuongeza nguvu kazi na kuhakikisha mradi huo unakamilika ifikapo Novemba 30, 2026, akisisitiza kuwa hakutakuwa na muda wa nyongeza.

Aweso ametoa agizo hilo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo, ikiwamo tanki kubwa la maji lililopo Mowe jijini Tanga, ambapo amesema serikali haitakubali visingizio kwa kuwa fedha za utekelezaji wa mradi huo zipo.

Amesema mradi huo umefikia zaidi ya asilimia 70 ya utekelezaji na kwamba mkandarasi anatakiwa kuongeza kasi kwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha wananchi wanaanza kunufaika na huduma hiyo kwa wakati uliopangwa.

“Nimekuja leo kukagua huu mradi nikiwa na Katibu Mkuu. Mradi huu sasa umefikia asilimia 75. Maelekezo ambayo nawaambia Tanga Uwasa na mkandarasi ni kwamba hatutakuwa na muda wa nyongeza,” amesema Aweso.
Ameongeza kuwa utendaji wa mradi huo unatakiwa kubadilika na mkandarasi kuongeza wafanyakazi ili kukamilisha kazi kwa wakati, akisisitiza kuwa hakuna sababu ya kuchelewesha mradi kwa kuwa fedha zipo.

“Tunataka mwisho wa mwezi huu wa 10 tukija kuona maendeleo yake, yatupatie picha kwamba ifikapo Novemba 30, 2026, mradi utakuwa umekamilika,” amesema.

Aweso amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi ya mfano inayotekelezwa na Wizara ya Maji kwa kutumia hati fungani kama chanzo mbadala cha fedha kwa ajili ya kuimarisha huduma ya maji.

Amesema lengo ni kuhakikisha kunakuwa na chanzo cha uhakika cha maji kitakachosaidia wananchi kupata huduma hata pale linapotokea tatizo la kiufundi au kukatika kwa umeme.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri, amesema wizara itaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga Uwasa) katika kumsimamia mkandarasi ili kuhakikisha anatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa mkataba.

Amesema timu ya wizara itafuatilia kwa karibu utekelezaji wa maelekezo ya Waziri Aweso, huku akisisitiza kuwa ifikapo Novemba 30, 2026, miundombinu yote inayohusika na mradi inapaswa kuwa imekamilika na wananchi kuanza kupata huduma.

Mkurugenzi wa Tanga Uwasa, Geoffrey Hilly, amesema mradi huo unaendelea vizuri na umefikia wastani wa asilimia 72 kwa ujumla, huku kazi zikiendelea katika maeneo mbalimbali kuanzia chanzo hadi usambazaji wa mabomba.

Amesema mradi huo unalenga kuboresha huduma ya maji katika Jiji la Tanga pamoja na Wilaya za Muheza na Mkinga, ambapo Mkinga ni miongoni mwa maeneo yatakayonufaika na maji yanayozalishwa katika mtambo wa Mowe.

Kwa mujibu wa Hilly, mradi huo unahusisha upanuzi wa mtambo wa uzalishaji maji kutoka uwezo wa kuzalisha lita milioni 45 hadi lita milioni 60 kwa siku.

Aidha, unahusisha ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita milioni 35, litakalosaidia kuhakikisha upatikanaji wa maji wakati wa changamoto za kiufundi.

Hilly amesema tanki hilo lina uwezo wa kuhifadhi maji ya kutosha kwa matumizi ya takribani saa 18, hatua inayotarajiwa kuongeza uhakika wa upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi.

Naye Meneja wa mradi huo kutoka kampuni ya China Railway Seventh Group, Dai Bin, ameahidi kuongeza nguvu kazi na muda wa kazi kwa kufanya shughuli za ujenzi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi huo unakamilika ndani ya muda uliowekwa.

Amesema kampuni hiyo imepokea maelekezo ya Waziri Aweso na itayatekeleza kwa kuongeza kasi ya ujenzi ili kufikia lengo la kukamilisha mradi ifikapo Novemba 30, 2026.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mama Fatma Karume, mjane wa Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika salamu zake za rambirambi, Rais Samia ametoa pole kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dkt. Amani Abeid Karume, pamoja na familia, ndugu, jamaa na wananchi wote wa Zanzibar kutokana na msiba huo.

Aidha, Rais Samia amewaombea wafiwa wote subira na faraja katika kipindi hiki cha majonzi, huku akimuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi.

“Inna lillahi waina ilayhi raajiun.”

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema watu watakaobainika kutupa taka hovyo jijini Dar es Salaam watachukuliwa hatua za kisheria, ikiwamo kutozwa faini ya Shilingi 300,000 hadi milioni moja au kifungo cha miezi 12 hadi 24.

Mpogolo amesema hatua hiyo inatokana na utekelezaji wa Kifungu cha 41 cha Sheria Ndogo ya Afya, Usafi na Usimamizi wa Mazingira ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ya mwaka 2024 (GN Na. 1011), ambayo amesema sasa inaanza kutekelezwa kikamilifu.

Akizungumza jana, Septemba 19, 2026, baada ya kuhitimisha zoezi la usafi wa mazingira jijini, Mpogolo amesema utekelezaji wa sheria hiyo unalenga kuhakikisha Dar es Salaam inakuwa safi, salama na yenye mazingira bora.

“Atakayekutwa anatupa uchafu hovyo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. Adhabu ni faini ya kuanzia Shilingi laki tatu hadi milioni moja au kifungo cha miezi 12 hadi 24. Kila mmoja anatakiwa kutambua wajibu wake na kuacha mara moja tabia ya kutupa uchafu hovyo,” amesema.

Amesema Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa usafi wa mazingira, huku hatua za kisheria zikichukuliwa dhidi ya watakaokiuka sheria kwa kutupa taka hovyo, kutiririsha maji au kufanya vitendo vingine vinavyohatarisha usafi na mazingira.
Kwa mujibu wa Mpogolo, utekelezaji wa sheria hiyo haulengi kutoa adhabu pekee, bali pia kujenga nidhamu, uwajibikaji na utamaduni wa usafi miongoni mwa wananchi.

Amesema Halmashauri itaendelea kuweka maeneo na vifaa vya kuhifadhia taka pamoja na kuhamasisha utenganishaji wa taka kulingana na aina zake ili kurahisisha ukusanyaji na utunzaji wa mazingira.

Katika kuimarisha ufuatiliaji wa usafi, Mpogolo amesema Jiji limejipanga kuajiri vijana waliomaliza mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kuwapatia vyombo vya usafiri kwa ajili ya kusimamia usafi katika mitaa mbalimbali.

“Tutakwenda mtaa kwa mtaa. Hatutaki kuona mtu anatupa taka popote anapotaka. Tutakuwa na mfumo wa ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha sheria inatekelezwa ipasavyo,” amesema.

Aidha, Mpogolo amesema barabara zote muhimu za Jiji, maarufu kama Smart Roads, zitasimamiwa kikamilifu ili zibaki safi, zipandwe miti rafiki na salama na ziendelee kulipamba Jiji.

Amesema biashara katika barabara hizo hazitaruhusiwa bila kibali cha Mkurugenzi wa Jiji, huku wafanyabiashara wakitakiwa kufanya shughuli zao katika maeneo yaliyopangwa.

Amesema hatua hiyo inalenga kupunguza msongamano, kuimarisha usalama wa watumiaji wa barabara na kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam linakuwa na mazingira safi na yanayovutia.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Waandishi wa Habari nchini wametakiwa kujiandaa kuripoti majanga yanayoweza kujitokeza katika msimu wa mvua za Vuli, huku wakitanguliza usalama wao, kutoa taarifa sahihi na kuwaelekeza wananchi hatua za kujikinga.

Wito huo umetolewa wakati Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ikitabiri kuwa msimu wa mvua za Vuli wa Oktoba hadi Desemba 2026 utaathiriwa kwa kiwango kikubwa na hali ya El Niño. Kwa mujibu wa TMA, mvua za juu ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya Pwani ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, ukanda wa Ziwa Viktoria na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Septemba 21, 2026, Mjumbe wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Bw. Mgaya Kingoba, amesema wananchi hutegemea taarifa za Waandishi wa Habari kufanya maamuzi ya kujilinda wakati wa majanga hivyo, utekelezaji wa jukumu hilo haupaswi kuhatarisha maisha ya Mwandishi.

“Wakati wa majanga, Mwandishi wa Habari anatakiwa kutimiza majukumu yake huku akilinda usalama wake na kuchukua tahadhari zote muhimu. Hakuna taarifa muhimu kuliko uhai wako,” amesema Kingoba.

Amesema Waandishi wa Habari wanapaswa kuthibitisha taarifa kabla ya kuzitoa kwa umma, akieleza kuwa taarifa zisizo sahihi zinaweza kusababisha hofu na taharuki. Amewataka kufuatilia utabiri na tahadhari za hali ya hewa kutoka TMA, pamoja na kupata taarifa za uokoaji na hatua za kukabiliana na maafa kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Idara ya Menejimenti ya Maafa ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Kamati za Usimamizi wa Maafa katika ngazi za mikoa na halmashauri.
Kwa mujibu wa mwelekeo wa msimu uliotolewa na TMA, mvua za Vuli zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya nne ya Septemba na wiki ya kwanza ya Oktoba katika ukanda wa Ziwa Viktoria, kisha kusambaa taratibu katika maeneo mengine mwezi Oktoba na ongezeko la mvua linatarajiwa mwezi Novemba.

Kingoba amesema wajibu wa Mwandishi wa Habari hauishii kueleza madhara yaliyotokea kwani unahusisha pia kuwafahamisha wananchi tahadhari za kuchukua, maeneo salama, mahali pa kupata msaada na hatua zinazochukuliwa na mamlaka.

“Mwandishi hatakiwi kuishia kueleza tatizo pekee, bali anapaswa pia kutoa taarifa za suluhisho; kwa mfano, kuwaeleza wananchi nini kifanyike, wapi wahamie, wapi wapate msaada na hatua zinazochukuliwa na Serikali,” amesema.

TMA imeeleza kuwa unyevu mwingi kwenye udongo na mafuriko vinaweza kujitokeza katika msimu huo na kina cha maji katika mito na mabwawa kinaweza kuongezeka, huku uchafuzi wa maji ukiweza kusababisha magonjwa.

Kingoba, ambaye pia ni Kaimu Meneja wa Huduma za Kiswahili wa Shirika la Magazeti ya Serikali (TSN), amevitaka vyombo vya habari kutumia lugha inayotoa mwongozo bila kuongeza taharuki akisema Waandishi wa Habari wanapaswa kutathmini hatari za maeneo wanayokwenda, kuvaa mavazi yanayofaa, kulinda vifaa vyao vya kazi dhidi ya maji na kuepuka maeneo yenye mafuriko makubwa au uwezekano wa maporomoko.

Aidha, amesema wakati wa kuchukua picha na kufanya mahojiano, Waandishi wa Habari wanapaswa kulinda faragha, heshima na utu wa watu walioathiriwa na majanga huku pia wakiangazia mahitaji ya watoto, wanawake na watu wenye uhitaji maalum ili sauti zao ziwafikie wanaohusika na utoaji wa msaada.

Kingoba amevitaka vyombo vya habari kuanza maandalizi mapema kwa kuwapatia Waandishi wa Habari vifaa vinavyofaa na maelekezo ya usalama, ili waweze kuihudumia jamii bila kuhatarisha maisha yao.

Na Mwandishi Wetu

DAR ES SALAAM: Wafanyakazi wa Puma Energy Tanzania wamekutana jijini Dar es Salaam kusherehekea hatua ya kampuni hiyo kufikisha vituo 100 vya mafuta na huduma za ziada nchini, huku wakitambua mchango wao katika mafanikio hayo.

Tukio hilo lililofanyika Septemba 19, 2026, liliwakutanisha wafanyakazi kutoka idara na maeneo mbalimbali ya kampuni, ambapo walipata fursa ya kuimarisha ushirikiano na mshikamano, pamoja na kujadili mwelekeo wa kampuni na mipango ya ukuaji wa biashara.

Hatua ya kufikisha vituo 100 imekuja wakati Puma Energy Tanzania ikiendelea kutambuliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kwa nafasi yake katika soko la mafuta nchini kwa miaka minne mfululizo.
Akizungumza katika tukio hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatma M. Abdallah, alisema mafanikio hayo ni matokeo ya juhudi na ushirikiano wa wafanyakazi katika maeneo mbalimbali ya kampuni.

“Kufikisha vituo 100 vya mafuta na huduma za ziada ni hatua muhimu katika ukuaji wa biashara yetu, lakini pia ni matokeo ya kazi ya watu walio nyuma ya mafanikio haya. Tumefikia hapa kutokana na kujituma na ushirikiano wa wafanyakazi katika maeneo mbalimbali ya kampuni,” alisema.

Alisema tukio hilo ni fursa ya kutambua mchango wa wafanyakazi, kuimarisha mahusiano ya kikazi na kuangalia kwa pamoja hatua inayofuata katika ukuaji wa kampuni.
 
“Tunapoadhimisha kufikisha vituo 100, tunatambua pia kuwa kila hatua ya mafanikio huleta majukumu mapya. Sasa tunalenga kujenga zaidi juu ya tulichokifikia, kuimarisha ushirikiano wetu na kuendelea kuwahudumia wateja kwa ufanisi. Wafanyakazi wetu wataendelea kuwa sehemu muhimu ya safari hii,” alisema.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kufikisha vituo 100 si tu ishara ya kupanuka kwa mtandao wa huduma za Puma Energy Tanzania, bali pia ni matokeo ya mchango wa wafanyakazi katika kuhakikisha shughuli za kampuni zinaendeshwa kwa ufanisi na huduma zinawafikia wateja katika maeneo mbalimbali nchini.

Katika tukio hilo, uongozi pia uliwashirikisha wafanyakazi kuhusu vipaumbele vya kampuni katika kipindi kijacho, hatua iliyowapa nafasi ya kuelewa mwelekeo wa biashara na nafasi yao katika kutekeleza mipango hiyo.
Puma Energy Tanzania inaendesha shughuli mbalimbali katika sekta ya nishati, ikiwemo uendeshaji wa vituo vya mafuta, usambazaji wa mafuta, huduma za mafuta ya ndege, vilainishi, LPG na lami, pamoja na nishati safi na suluhisho zinazolenga kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.

Puma Energy ni kampuni ya kimataifa inayojihusisha na huduma za nishati katika zaidi ya nchi 35, hasa Amerika ya Kati na Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Dar es Salaam, Tanzania: The Tanzania National Commission for UNESCO and UNESCO continue to strengthen their cooperation in advancing shared priorities in education, science, culture, communication and information, and sustainable development.
The photograph was taken during an official engagement at the UNESCO Office, UN House, PSSSF Tower Complex, Dar es Salaam, reflecting the continued collaboration between the two institutions in support of UNESCO’s mandate and Tanzania’s development priorities.

Pictured from left: Prof. Hamisi Masanja Malebo, Executive Secretary, Tanzania National Commission for UNESCO; and Mr Michel Toto, UNESCO Country Representative in Tanzania.
Photo: Tanzania National Commission for UNESCO

Na Mwandishi Wetu, Dodoma.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Christian Makonda, ametangaza kutoutambua mchakato wa kubadilisha jezi za timu za taifa, akisema umefanyika bila kuishirikisha Wizara licha ya maelekezo aliyoyatoa Februari 2026.

Sambamba na hatua hiyo, Waziri Makonda ameagiza kuundwa kwa kamati maalumu itakayochunguza mikataba ya wazabuni wa jezi hizo, manufaa yake kwa timu za taifa pamoja na mapato yanayotokana na mauzo yake.

Uamuzi huo umetangazwa siku mbili baada ya Waziri Makonda kukataa hadharani jezi mpya zilizoonekana zikivaliwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, akisema hazikuwa na ubora unaoendana na hadhi ya Taifa Stars.

“Hii siyo jezi ya Taifa Stars. Taifa Stars kwa ubora wake hatuwezi kuwa na jezi za kiwango cha chini hivi. Acheni kutumia picha za Naibu wangu huku ofisi yangu haina taarifa. Tuheshimiane,” alisema Waziri Makonda kupitia mitandao ya kijamii.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara leo, Septemba 18, 2026, uchunguzi huo unalenga kubaini iwapo mikataba iliyopo inanufaisha timu za taifa kwa kiwango kinacholingana na fedha nyingi zinazotolewa na Serikali kugharamia timu hizo.

Wizara imeeleza kuwa Februari 2026, Waziri Makonda alitoa maelekezo ya kuboresha jezi za timu za taifa ili ziakisi utambulisho wa Tanzania na kuzalisha manufaa mapana kwa nchi.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa muhimu kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika maandalizi ya timu za taifa zinazoshiriki mashindano ya kimataifa, pamoja na Tanzania kuwa mwenyeji mwenza wa Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2027 (AFCON 2027).

Kamati hiyo pia itachunguza mapato yanayotokana na mauzo ya jezi na mchango wake katika kugharamia uendeshaji wa timu za taifa.